Serikali imefafanua kuhusu uingizaji
wa mayai kutoka nje, mapambano
dhidi ya kifua kikuu na mashirika na
taasisi za umma kujiunga na Mfuko wa Bima wa Taifa na utaratibu wa michezo ya bahati nasibu hapa nchini. Ufafanuzi huo umetolewa leo
mjini hapa.
Zuio la Uingizaji
wa Mayai kutoka Nje.
Serikali imesema kuwa
hakuna mwekezaji yeyote aliyeruhusiwa kupewa kibali cha kuingiza vifaranga au
mayai ya kuku nchini kwa ajili ya biashara.
Katika kusimamia hili,
kuanzia mwaka 2013 hadi 2017 vifaranga 67500 vilivyoingizwa nchini kinyume na sheria viliteketezwa.
Akifafanua kuhusu
hoja hiyo, Naibu Waziri wa Kilimo,Mifugo
na Uvivu, Mhe.William Ole Nasha amesema
wako wawekezaji wachache ambao hupewa vibali maalum vya kuingiza mayai au vifaranga
wa kuku wazazi(Parent Stock) tu na ukaguzi kwa ajili ya kudhibiti uingizaji
vifaranga na mayai unaendelea na hatua kali zinachukuliwa kwa yeyote
anayekamatwa kwa kukiuka utaratibu.
Mapambano dhidi ya kifua kikuu na Silicosis
Serikali imesema kuwa
inafahamu changamoto ya uwepo wa magonjwa ya kifua kikuu na Silicosis katika
maeneo ya wachimbaji wa Madini. Kwa upande wa Kifua Kikuu inakadiriwa kuwa
tatizo hilo ni kubwa ikilinganishwa na hali halisi katika maeneo mengi.
Kwa upande wa Silicosis
kumekuwepo na ripoti za wagonjwa wachache katika hospitali za Serikali ikiwemo Kibong’oto
ambao ni wachimbaji wadogo wadogo wa madini.
Naibu Waziri wa
Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee
na Watoto, Dkt. Khamis Kingwangalla amesema Serikali kupitia Halmashauri zilizo
katika maeneo ya migodi imeanza kuweka mikakati ya kudhibiti magonjwa haya na
pia kutoa elimu kwa wachimbaji namna ya kujikinga na vumbi na kutumia njia
sahihi za uchimbaji.
Ameongeza kuwa Serikali
itaongeza wigo wa huduma katika vituo vya afya kwenye maeneo yaliyoathirika,
hususan Mkoa wa Geita ili vituo viwe na uwezo wa kuchunguza na kutibu magonjwa
hayo na kuwajengea uwezo wataalamu wa Afya katika kuhudumia wagonjwa katika
maeneo ya migodi.
Mashirika
na Taasisi za Umma kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.
Serikali imesema kuwa hadi
kufikia tarehe 31/12/2016, Idara za Serikali,Taasisi na Mashirika ya Umma
zinazotumia Huduma za Bima ya Afya za NHIF zimefikia 307.
Naibu Waziri wa
Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee
na Watoto, Dkt. Khamis Kingwangalla amesema Mashirika, Taasisi na Idara za Serikali ambazo
hazijajiunga na Mfuko huo zipo 23 zikiwemo
TRA, BOT, TANESCO, NHC, TPA,PSPF, LAPF, PPF, EWURA, NCA, na GEPF.
Ameongeza kuwa Mfuko huo unaendelea na jitihada za kukutana
na uongozi wa Mashirika hayo ya umma kwa lengo la kutoa elimu na kuwahimiza juu
ya umuhimu wa kujiunga kama ilivyoainishwa
katika Sheria ya Mfuko.
Aidha, hadi kufikia mwezi Machi,2017
idadi ya wanachama katika Mfuko huo imefikia wanachama 792987 kutoka wananchama
474760 mwaka 2012.
Imetolewa
na:
Idara
ya Habari-MAELEZO.


0 Comments