WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imefuta baadhi
ya tozo katika mazao ya pamba, chai na kahawa ambazo ni kero kwa wakulima
ikiwemo ya sh. 450,000 iliyokuwa inatolewa na kila kiwanda cha kuchambua pamba
kwa ajili ya kuchangia mbio za Mwenge.
Amesema tozo nyingine iliyofutwa kwa zao la pamba ni ada ya
vikao vya Halmashauri za Wilaya ambayo ni sh. 250,000, ambapo katika zao la
chai kodi ya moto na uokoaji imeondolewa na kwenye zao la kahawa, ada ya leseni
ya kusindika kahawa ya Dola za Marekani 250 imefutwa.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Aprili 6, 2017)
katika hotuba yake ya mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya
mapato na matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka
2017/2018 Bungeni mjini Dodoma.
Amesema kufutwa kwa tozo hizo ni utekelezaji wa ahadi ya
Serikali kwa wakulima nchini ili kuwapunguza kodi, tozo na ada mbalimbali
zinazochangia kuwapunguzia faida.
“Serikali pia imeboresha mfumo wa stakabadhi ghalani kwa
kuanzisha utaratibu wa wazi wa ununuzi wa mazao kupitia minada na katika msimu
wa mwaka 2016/2017 kwenye zao la korosho, utaratibu huo umechangia kwa kiasi
kikubwa kuongezeka kwa bei ya korosho kwa kilo kutoka sh 1,200 hadi sh 3,800, bei ambayo haijawahi kufikiwa
katika historia ya zao la korosho nchini,” amesema.
Amesema mfumo huo wa stakabadhi ghalani na utaratibu wa
minada umeongeza ushindani na kuvutia wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi
hususan nchi ya Vietnam na nchi nyingine kuja wenyewe kununua korosho badala ya
kutegemea soko la India pekee.
Waziri Mkuu amesema katika mwaka 2017/2018, Serikali
itaendelea na uchambuzi wa kina wa kodi, tozo na ada zilizobaki katika sekta za
kilimo, mifugo na uvuvi kwa lengo la kuziondoa au kuzipunguza ili kumwezesha
mkulima kunufaika zaidi na jasho lake na kuongeza mapato ya Halmashauri.
Katika hatua
nyingine Waziri Mkuu amesema Bunge lilipitisha Sheria ya Huduma za Habari Na. 12 ya
mwaka 2016, ambayo ni muhimu katika kuimarisha usimamizi na uwajibikaji katika Sekta
ya Habari nchini, ambapo Kanuni za Sheria hiyo
zimeandaliwa na tayari zimeanza kutumika.
“Natoa wito kwa wadau wa sekta
ya habari kuzingatia sheria na kanuni hizo ili kuimarisha weledi katika tasnia
ya habari. Aidha, nashauri wadau wa habari kujikita zaidi katika kuandika na
kutangaza habari za masuala ya maendeleo na uchumi ili kuwasaidia wananchi
kutekeleza azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kujenga uchumi wa viwanda na
kuboresha huduma za kijamii,” amesema.
Pia
Waziri Mkuu amevikumbusha vituo vya televisheni kuweka wakalimani wa lugha
katika vituo vyao. Amesema katika mwaka 2017/2018, Serikali itaendelea kutoa
huduma kwa watu wenye ulemavu ikiwa ni pamoja na kutoa vifaa saidizi kwa
wanafunzi wenye ulemavu shuleni na vifaa vya kufundishia.
Hata
hivyo, Waziri Mkuu amesema kwamba Serikali imeendelea kutoa huduma pamoja na
kuongeza upatikanaji wa haki na fursa kwa watu wenye ulemavu na katika kutimiza
azma hiyo, amewaagiza Wakuu wa Mikoa kuhakikisha kuwa Kamati za Watu wenye
Ulemavu zinaanzishwa katika ngazi za Mikoa, Wilaya, Mitaa na Vijiji.
Pia Serikali
imeanzisha kampeni za kupinga unyanyapaa na vitendo vya kikatili dhidi ya watu
wenye ualbino katika mikoa ya Shinyanga, Mwanza, Geita, Simiyu, Kagera, Tabora,
Kigoma, Mara, Mbeya, Katavi na Rukwa na kampeni hiyo itaendelea nchi nzima.
IMETOLEWA
NA:
OFISI
YA WAZIRI MKUU,
S.L.P
980, DODOMA
ALHAMISI,
APRILI 6, 2017.

0 Comments