![]() |
| Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga na Waziri wa Nishati na Madini wa Uganda, Mhe. Mhandisi Irene Muloni wakiweka saini Mkataba ambapo Tanzania na Uganda zitashirikiana kuendeleza mradi wa umeme wa kutumia maji wa MW 14 katika eneo la Kikagati/Murongo. |
Tanzania
na Uganda zimefungua sura mpya ya ushirikiano baada ya Mawaziri wa Mambo ya Nje
wa nchi hizo kusaini nyaraka inayoainisha maeneo mbalimbali ambayo nchi hizo
zimekubali kushirikiana kwa pamoja ili kuinua uchumi wa mataifa yao.
Nyaraka
hiyo iliyosainiwa leo jijini Arusha imetokana na Kikao cha Tume ya Kudumu ya
Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya
Tanzania na Uganda kilichofanyika kwa siku tatu kuanzia tarehe 03 Aprili 2017.
"Makubaliano
haya yataongeza chachu ya uhusiano na ushirikiano wetu na Uganda, japokuwa tulichelewa
kufanya kikao cha JPC tokea mkataba uliposainiwa mwaka 2007 nchini
Uganda". Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe.
Dkt. Augustine Mahiga alisema alipokuwa akisoma hotuba ya kufunga.
Kikao cha
JPC kilifanyika kwa kuzingatia makundi ya kisekta ambapo katika kila kundi,
wajumbe waliainisha maeneo yenye maslahi kwa pande zote ambayo yanajumuisha
pamoja na mambo mengine: uendelezaji wa miundombinu; kilimo; viwanda; biashara;
uwekezaji; nishati; utalii; utunzaji wa mazingira; uvuvi; ufugaji; afya; elimu;
utangazaji; madini na masuala ya kijamii.
Kikao
hicho kilitarajiwa kuhitimishwa kwa kusainiwa mikataba sita lakini kutokana na
mashauriano ya ndani ya baadhi ya mikataba kutokamilika, mikataba miwili ndio
iliweza kusainiwa. Mikataba hiyo ni ushirikiano katika kuendeleza mradi wa
Umeme wa kutumia maji wa MW 14 katika eneo la Kikagati/Murongo na huduma za
usafiri wa anga.
Mikataba minne iliyosalia ambayo inahusu ushirikiano
katika usafiri wa reli, usafiri wa majini; utangazaji na ulinzi wa raia
itasainiwa wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
(EAC) utakaofanyika hivi karibuni hapa nchini.
Waziri
Mahiga alieleza kuwa kusainiwa kwa mikataba
hiyo ni muhimu kwa kuwa itaimarisha zaidi misingi ya mahusiano yetu, hivyo
alizihimiza pande zote kukamilisha mashauriano hayo ili mikataba hiyo iweze
kusainiwa katika muda uliopangwa.
Kwa
upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda, Mhe. Sam Kutesa alisisitiza
umuhimu wa Tanzania na Uganda kufanya kazi kwa pamoja ili kuinua uchumi kwa
madhumuni ya kuwaondolea umasikini wananchi.
Alisema
mradi wa ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Uganda hadi
Tanzania ni moja ya miradi itakayosaidia kuboresha maisha ya wananchi, hivyo
alisisitiza umuhimu wa kukamilisha taratibu zote zilizosalia ili ujenzi huo
uweze kuanza.
Alihitimisha
hotuba yake kwa kuzipongeza Tanzania na Uganda kwa kufanikisha uwekaji saini wa
mikataba miwili ukiwemo wa kuendeleza mradi wa Umeme wa kutumia maji wa MW 14
katika eneo la Kikagati/Murongo ambao ulikuwa katika majadiliano kwa zaidi ya
miaka minane.
Kikao
hicho cha JPC kimefanyika kufuatia maelekezo ya Marais wa nchi hizo waliyoyatoa
wakati wa ziara ya Rais wa Uganda nchini mwezi Februari 2017. Viongozi hao
waliagiza kikao cha JPC kifanyike kabla ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya
ya Afrika Mashariki (EAC) ambao ulipangwa kufanyika jijini Dar Es Salaam tarehe
06 Aprili 2017.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya
Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar Es Salaam, 05 Aprili, 2017

0 Comments