Na Husna Saidi na Nuru Juma- MAELEZO
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekusanya Trilioni 10.87 mpaka
kufikia Machi mwaka huu kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
Hayo yamesemwa na Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo Charles Edward
Kichere wakati wa mahojiano na
mtangazaji wa TBC1 Rashid Salum katika kipindi cha Tunatekeleza kinachorushwa kila siku za Jumatatu saa moja kamili jioni na
Alhamisi saa tatu na nusu usiku.
Kichere alisema, mwaka huu wa fedha 2016/2017 TRA inatakiwa kukusanya
Trilioni 15.105 na hadi kufikia Machi mwaka huu TRA imefanikiwa kukusanya Shilingi Trilioni 10.87.
Aliendelea kwa kusema kuwa mpaka kufikia Juni mwaka huu TRA itahakikisha inatimiza lengo la kukusanya
Shilingi Trilioni 15.105 ili kusaidia
Serikali kuleta maendeleo kwa wananchi wake.
Alisema kuwa TRA ina waajiriwa wapya ambao wamepewa mafuzo ya miezi
sita katika chuo cha kodi juu ya mifumo
mbalimbali ya ukusanyaji kodi ambao waliajiriwa moja kwa moja na mamlaka hiyo kwaajili ya kutekeleza majukumu ya ukusanyaji
kodi ndani ya nchi.
“Tunatumia mfumo wa Tehama kukusanya kodi na mifumo mingine
mbalimbasli kama vile Tigo Pesa , Airtel Money na MPesa ili
kurahisishia watu kulipa kodi wakiwa nyumbani na kuepuka usumbufu,” alisema
Kichere.
Kichere aliongeza kuwa kwa mwaka huu wa fedha mapato yameongezeka mpaka
kufikia asilimia 9.9 hadi 10 licha ya kuwa kuna baadhi ya maeneo hawakuweza
kukusanya.
Aidha Kichere alisema Mamlaka kwa sasa imejipanga kuwa na mahusiano
mazuri na wafanyabiashara ili kuhakikisha wafanyabiashara wanalipa kodi stahiki
na kwa mujibu wa sheria bila kutumia nguvu au uonevu wowote.
Hata hivyo mamlaka hiyo imekuwa ikitoa elimu kwa walipa kodi kwa kupitia vyombo
mbalimbali vya habari, kutoa semina kwa watumishi wa umma , kuandaa makongamano
ambayo yanatoa elimu, kupitia mitandao ya kijamii na ziara mbalimbali ambazo
wamekuwa wakizifanya ili kuhakikisha wafanyabiashara wanapata elimu pamoja na
kujua wajibu wao katika kulipa kodi ili kuleat maendeleo nchini.

0 Comments