Mwenyekiti wa Umoja wa Kilimo cha Mbogamboga Wilaya
ya Temeke, Joseph Kunguru (katikati) akizungumza na waandishi wa habari kuhusu
Kampeni ya kuwahamasisha Vijana kujihusisha na kilimo cha kisasa cha Mbogamboga
na Matunda leo Jijini Dar es Salaam. Kutoka kushoto ni Diwani wa Kata ya Buza, Manispaa ya Temeke,
James Raphael Mkude na Makamu Mwenyekiti
wa Umoja huo Waziri Pembe Waziri.
Diwani wa Kata ya Buza Manispaa ya Temeke James
Raphael Mkude akifafanua jambo mbele ya waandishi wa habari kuhusiana Kampeni
ya kuwahamasisha vijana kujihusisha na kilimo cha kisasa cha Mbogamboga na Matunda
leo Jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya waandishi wa habari wakifatilia kwa
umakini mkutano baina yao na viongozi wa Umoja wa Kilimo cha Mbogamboga na Matunda
leo Jijini Dar es Salaam.
Picha na: Husna Saidi - MAELEZO
..........
Na Nuru Juma na Husna
Saidi-MAELEZO
Umoja wa Kilimo cha
Mbogamboga, Matunda na Nafaka umeanzisha Kampeni ya Kijana Inuka na Kilimo cha
Mbogamboga na Matunda kwa lengo la kuepukana na kilimo cha mvua na vijana
waweze kujiajiri wenyewe.
Hayo yamesemwa na
Mwenyekiti wa Umoja huo Wilaya ya Temeke Joseph Kunguru alipokutana na
waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam.
Kunguru alisema kuwa
kilimo hicho ni kilimo biashara na
kinahitaji maji na miundombinu ya uhakika ili kuwafanya wananchi kulima kilimo
chenye tija badala ya kulima kwa kutegemea mvua.
“Kilimo hiki
kinaonekana ni kilimo ghari sana kwani ujenzi wa Green House unaonekana ni
kilimo cha watu wenye pesa lakini ukweli ni kwamba wananchi wakiungana pamoja
katika kilimo hiki wanaweza kufanikiwa badala ya kulima kwa kutegemea mvua,”
alisema Kunguru.
Aidha alisema kuwa
vijana wengi mtaani hawana ajira hivyo viongozi kupitia kampeni hii watumie
fursa hiyo kuwaelimisha kuhusiana na kilimo hiki cha umwagiliaji ili waweze
kujiajiri wenyewe.
Umoja huo wa kilimo
cha Mbogamboga na Matunda na Nafaka umesajiliwa kisheria na ulianza na
wanachama 17 mpaka sasa wapo 100 ila wanachama hai wapo 74 hivyo wanawasihi
wananchi waendelee kujitokeza kujiunga.
Kwa upande wake mmoja
wa wanakikundi hicho Sifa Karuka alisema alihamasika kujiunga na kikundi hicho
baada ya kupata taarifa kuhusu kilimo hicho cha kisasa licha ya kuwa na shughuli zake binafsi hivyo
anawasihi wakinamama na wasichana wajitokeze kwa wingi ili waweze kujiendeleza kiuchumi.
Nae Diwani wa Kata ya
Buza James Raphael Mkude aliwahamasisha madiwani wenzie kuweza kuunda vikundi
kama hivyo katika kata zao ili wananchi wao hasa vijana wasiokuwa na ajira
waweze kujikwamua kiuchumi.
Kikundi hicho
kimeiomba Serikali kupitia Maofisa Ugani kutoa mafunzo kwa vijana ambao hawana
ajira kuhusiana nakilimo hicho ili kupunguza ukosefu wa ajira kwa kujitegemea
wao wenyewe.



0 Comments