NA IS-HAKA OMAR, PEMBA.
BAADHI ya wananchi kisiwani Pemba
wameshauriwa kuacha siasa za visasi na chuki zinazochangia kuongezeka
vitendo vya uhalifu wa mali na kuharibu heshima ya nchi kitaifa na
kimataifa.
Ushauri huo umetolewa na Naibu
Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt. Abdalla Juma Saadala katika mwendelezo
wa ziara zake za kuimarisha uhai wa chama huko Tawi la CCM Kengeja,
Mkoa kusini Pemba.
Alifafanua kwamba hali hiyo sio
kwamba inaishia kuathiri uchumi na siasa za nchi peke yake bali vinaenda
mbali kwa kuathiri maisha na undugu wa damu uliopo hata kabla ya
kuanzishwa kwa mifumo ya kisiasa nchini.
Nasaha hizo alizitoa baada ya
kuwepo kwa malalamiko ya uharibifu wa miundombinu ya maji safi na salama
katika shehia hiyo, iliyoharibiwa na baadhi ya watu kwa kujenga zenge
la kuzua maji yasiwafikie wananchi wa eneo hilo.
“ Serikali inarahisha huduma kwa
wananchi kwa kuwajengea miundombinu rafiki ya upatikanaji wa maji safi
na salama pamoja na huduma nyingine muhimu lakini baadhi yenu wanaharibu
kwa makusudi kutokana na masuala ya UCCM na UCUF, hilo sio sahihi
kabisa lazima tubadilike kwa kuacha tabia hizo.”, alisema Dkt. Mabodi.
Hata hivyo alitoa wito kwa vyombo
vya Dola kutoa taarifa na ripoti za kudhibiti vitendo hivyo kwa vyombo
vya habari ili jamii ijue utekelezaji wake.
Aliwambia wanachama wa chama
hicho kwamba waendelee kushikamana na kuwa watulivu na wasilipize
visasi na badala yake waendelee kutenda wema na kuwaelimisha watu
waohusika na hujuma hizo ili waweze kubadilika na kujiunga na chama
hicho.
Aliwataka baadhi ya vijana
wanashutumiwa kujihusisha na vitendo hivyo kuacha, na kutafakari kwa
kina athari zake kwani zinawaumiza Watu wenye ulemavu, Wazee pamoja na
wagonjwa waliopo hospitalini wanaohitaji huduma hizo wakati wote.
Pamoja na hayo alisisitiza umuhimu
wa wanachama kushiriki katika zoezi la uchaguzi wa ndani ya chama na
Jumuiya katika zoezi linaloendelea hivi sasa ili wapatikane viongozi
wenye uwezo wa kukiletea chama ushindi wa ngazi zote za uchaguzi mwaka
2020.
Wakati huo huo, Naibu Katibu Mkuu
huyo alipongeza Mwakilishi wa Jimbo la Ole, Mussa Ali Mussa kwa juhudi
zake katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020
kwa wananchi wote licha ya kukabiliwa na vikwazo vya kisiasa kutoka kwa
wapinzani.
Akitoa tathimini ya masuala ya
ulinzi na usalama Mkuu wa Wilaya ya Chake Chake, Salama Mbarouk Khatib
alisema toka kumeanzishwa doria za mara kwa mara ndani ya eneo hilo
vitendo vya uhujumu mali na miundombinu ya umma vimepungua.
Hata hivyo alisema na kutoa onyo
kali kwa baadhi ya wananchi wanaoendelea na tabia ya kufunga Ng’ombe
katika mifereji ya maji safi na kusababisha uharibifu, na kuongeza kuwa
serikali itachukua hatua za kisheria kwa yeyote atakayebainika kuhusika
na uhalifu huo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti
wanachama hao, waliwataka viongozi wa majimbo, jumuiya na chama kwa
ujumla kufanya ziara za mara kwa mara katika mashina na Matawi ili kujua
matatizo yanayowakabili wananchi pamoja na ufanisi na udhaifu wa
utekelezaji wa shughuli za kisiasa katika ngazi hizo.

0 Comments