Meneja
wa Arsenal Arsene Wenger amesema hatima yake katika klabu hiyo
itaamuliwa katika mkutano wa bodi ya klabu hiyo baada ya fainali ya
Kombe la FA mnamo 27 Mei.
Mfaransa huyo wa miaka 67 amekuwa na Gunners tangu 1996 na mkataba wake wa sasa unafikia kikomo mwisho wa msimu huu.
Wenger amekuwa akishutumiwa sana
na baadhi ya mashabiki wa klabu hiyo, na kunao ambao wamekuwa wakiweka
mabango kumtaka ajiuzulu.
“Kuna mambo mengi ambayo yatajadiliwa katika mkutano wa bodi. Moja, ni nini kitamtendekea meneja,” amesema.
“Bila shaka nitakuwepo. Kwa sasa
tunafaa kuangazia yaliyopo sasa na ni kwamba tunacheza Jumapili na tuna
fainali ya Kombe la FA.”
Klabu hiyo ya London kaskazini
itakutana na mabingwa wa ligi Chelsea uwanjani Wembley, tumaini pekee la
Arsenal kushinda kikombe msimu huu.
Arsenal wamesalia kucheza mechi
moja pekee ligini, ambapo wana kibarua cha kujaribu kufuzu kwa Ligi ya
Klabu Bingwa Ulaya kwani wamo nafasi ya tano, alama moja nyuma ya
Liverpool walio nafasi ya nne na tatu nyuma ya Manchester City, lakini
wanapungukiwa na mabao.
Arsenal watakuwa wenyeji wa
Everton mechi ya mwisho Jumapili (15:00 GMT), nao Liverpool watakuwa
wenyeji wa Middlesbrough uwanjani Anfield nao Manchester City wasafiri
Watford.
Wenger aliongeza: “Lazima tufanye
kazi yetu, sisi ni wataalamu na tunataka kushinda. Tumekuwa katika mbio
nzuri na tunachoweza kufanya kwa sasa ni kushinda mechi yetu ya
Jumapili. Baada ya hapo, kitakachotendeka kunihusu si muhimu.”
“Niko hapa kuitumikia klabu na njia bora zaidi ya kufanya hivyo ni kushinda mechi ijayo.”

0 Comments