WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa ngazi mbalimbali waweke utaratibu
utakaoruhusu huduma za afya kuendelea kutolewa kwa wananchi katika maeneo yao hata
kama zoezi la usafi la kila mwezi litakuwa linaendelea.
Serikali
imeweka utaratibu wa wananchi kushiriki katika shughuli za usafi wa mazingira
siku ya Jumamosi ya mwisho wa mwezi, zoezi ambalo linashirikisha watu wote
wakiwemo wafanyabiashara na watoa huduma nyingine zoezi linalofanyika kuanzia
saa 12.00 asubuhi hadi saa 4.00 asubuhi.
Waziri
Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Mei 11, 2017) Bungeni mjini Dodoma katika
kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu wakati akijibu swali la
Mheshimiwa Abdallah Ulega mbunge wa Mkuranga.
Mheshimiwa Ulega alitaka kupata kauli
ya Serikali kuhusu maeneo ya kutolea huduma mbalimbali zikiwemo za afya ambayo
hufungwa wakati wa zoezi la usafi linalofanyika kila mwezi nchini, jambo
linalosababisha kero kwa wagonjwa na wengine wenye dharula.
Waziri Mkuu amesema “Hospitali na
maeneo mengine ya kutolea huduma za afya hayawezi kufungwa, viongozi wa maeneo
husika waweke utaratibu mzuri utakaoruhusu huduma hizo ziendelee kutolewa bila
ya kuathiri zoezi la usafi wa mazingira,”.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu
amesema Serikali imeagiza tani 131,000 za sukari ili kukabiliana na upungufu
uliopo nchini. Amesema Serikali iko macho na inajua maeneo yanayohitaji
kuboreshwa kulingana na mahitaji.
“Mahitaji ya sukari nchini kwa mwaka
ni tani 420,000, ambapo tunazalisha tani 320,000, hivyo tunaupungufu wa tani
100,000 hata hivyo tumeagiza tani 131,000 na tayari tani 80,000 zimewasili
nchini, ambapo kati yake tani 35,000 zimeingizwa sokoni,” amesema.
Ametoa kauli hiyo wakati akijibu
swali lililoulizwa na Mheshimiwa Jaku Hashim Ayoub aliyetaka Serikali
iwahakikishie wananchi upatikanaji wa sukari hususan katika kipindi cha mwezi
Mtukufu wa Ramadhani unaotarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi huu.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
DODOMA.
ALHAMISI, MEI 11, 2017.

0 Comments