Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga akiwasilisha
mada juu ya fursa zinazopatikana kwa ajili ya wakulima na wadau wa
kilimo cha karafuu wakati wa Kikao cha Wadau wa Karafuu visiwani
Zanzibar.
Wadau wa Zao la Karafuu wakifuatilia kwa makini wasilisho kutoka TADB.
Mwenyekiti
wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Taifa la Biashara Zanzibar (ZSTC),
Bw. Kassim
Maalim Suleiman (kushoto) akizungumza wakati wa Kikao cha Wadau wa
Karafuu ambapo TADB ilialikwa kuwasilisha mada juu ya fursa
zinazopatikana kwa ajili ya wakulima na wadau wa kilimo cha karafuu.
Wadau wa Zao la Karafuu wakifuatilia kwa makini wasilisho kutoka TADB.
Na mwandishi wetu, Zanzibar
Benki ya Maendeleo ya Kilimo ya Tanzania (TADB) imewahakikisha kuwapatia mikopo wakulima wa
Zao la Karafuu visiwani Zanzibar katika kuhakikisha inachangia kwa kiasi kikubwa katika
kuleta Mapinduzi yenye tija katika wakulima hao.
Hayo
yalielezwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga
wakati akitoa mada
juu ya fursa zinazopatikana kwa ajili ya wakulima na wadau wa kilimo
cha karafuu visiwani Zanzibar katika Kikao cha Wadau wa Karafuu
kilichokuwa kinafanyika mjini Unguja.
Bw. Assenga alisema kuwa Serikali inatambua changamoto wanazokutana nazo wakulima nchini na
hivyo uanzishwaji wa TADB unalenga kutekeleza hatua mbalimbali zikilenga kuharakisha
mapinduzi na maendeleo katika Sekta ya Kilimo ikiwemo uendelezaji
wa zao la karafuu ambalo ni zao kuu la biashara visiwani Zanzibar.
“Tunatambua kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) iliweka Mkakati
Maalum wa miaka 10 (2011 -2021) wa kuongeza uzalishaji,
usafirishaji, ubora na tija wa zao la karafuu kwa kutambua hilo Benki
inakuja kuongeza kasi juhudi hizi za Serikali,” alisema.
Alisema kwa kutambua juhudi za SMZ zao la karafuu lilipewa kipaumbele cha pekee
miongoni mwa minyororo ya thamani ya kwanza kuanza
kupatiwa mikopo na Benki hiyo kwa ajili ya uongezaji wa thamani mazao
mbalimbali nchini.
Aliongeza
kuwa maeneo yanayowekewa mkazo katika undelezaji wa kilimo cha karafuu
ni pamoja
na uongezaji tija wa kilimo cha karafuu ambapo TADB inatoa mikopo na
kusaidia shughuli mbali mbali za uongezaji tija wa mazao yatokanayo na
kilimo cha karafuu.
“Katika
kuhakikisha kuwa uongezaji tija wa kilimo cha karafuu unafanyika
ipasavyo Benki inashirikisha
wadau wa Kilimo, utafiti na huduma za ugani na ili kuwapatia wakulima
mafunzo ya kilimo cha kisasa cha karafuu na kutumia mbinu bora za kilimo
ili kuongeza mazao ya karafuu,” Bw. Assenga alisema.
Bw.
Assenga aliongeza pia Benki inatoa mikopo kwa ajili ya ununuzi wa
pembejeo za kilimo (mbegu
bora na miche ya karafuu yenye kuvumilia magonjwa, wadudu, na inayotoa
mazao mengi na kiwango kikubwa cha karafuu, mbolea, madawa na
mengineyo); na kugharamia teknolojia bora na nafuu ya umwagiliaji
(panapohitajika).
Aliyataja
maeneo mengine yanapatiwa mikopo ni pamoja na ununuzi wa vifaa, mashine
na mitambo
mbalimbali ya kilimo cha karafuu na mtaji kwa ajili ya uendeshaji wa
shamba, uongezaji wa thamani na gharama za uhifadhi na masoko
Bw.
Assenga alisema kuwa TADB pia inatoa mikopo kwa ajili ya uendelezaji wa
zao la karafuu
katika kusaidia uwekezaji kwa ajili ya ujenzi, ununuzi wa mitambo na
ufungaji wa mitambo ya usindikaji wa karafuu kwa ajili ya kuongeza
thamani mazao ya karafuu. Ikiwemo ununuzi wa mashine bora za uvunaji,
ukaushaji, usafirishaji na uhifadhi wa karafuu; ununuzi
wa vifaa vya teknolojia ya kisasa kwa ajili ya kupunguza upotevu wa
mazao baada ya mavuno.
Mikopo mingine ni kwa ajili ya ununuzi wa mitambo
ya usindikaji pamoja na vifungashio vya karafuu; uchambuzi wa madaraja
na ubora wa karafuu na uwekaji wa utambuzi wa
muuzaji; na kugharamia mahitaji mengineyo ili kuongezea karafuu
thamani.
Kwa
upande wa miundombinu ya masoko, Kaimu Mkurugenzi huyo alisema kuwa
Benki inatoa mikopo
kwa zao la karafuu kwa lengo la kuendeleza miundombinu ya masoko kama
vile ujenzi wa maghala/vifaa vya kuhifadhia karafu na mazao yake na
miundombinu ya masoko; kugharamia usafirishaji
wa karafuu na mazao yake yaliyo tayari kwenda
sokoni. Mikopo mingine ni kwa ajili ya uanzishaji wa mifumo ya
upatikanaji wa taarifa za masoko, kuwezesha uhusiano wa masoko ya ndani
na masoko ya kikanda na kugharamia
mahitaji mengineyo ya kuwezesha miundombinu ya masoko.
Naye,
Mkurugenzi wa Biashara na Mikopo wa TADB, Bw. Augustino Chacha amesema
kuwa TADB inatoa
mikopo ya aina tatu ambayo ni Mikopo ya Muda Mfupi (Hadi Miaka Miwili
(2)), Mikopo ya Muda wa Kati (Zaidi ya Miaka 2 hadi Miaka Mitano (5)) na
Mikopo ya Muda Mrefu (Zaidi ya Miaka 5 hadi Miaka Kumi na Mitano (15)).
“Mikopo hii ni ya riba nafuu ambayo inalenga katika kuchagiza na kusaidia Mapinduzi ya Kilimo
kutoka kilimo cha kujikimu kwenda cha kibiashara ili kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini,” alisema.
Karafuu
ni zao la kipaumbele katika uchumi wa Zanzibar ambapo Serikali ya
Mapinduzi kupitia
Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC) imekuwa ikifanya Mageuzi
makubwa katika Sekta nzima ya Karafuu ikiwa ni pamoja na kutengeneza
Sheria, Sera na Miongozo madhubuti ya kusimamia Sekta hii ambapo faida,
tija na ustawi wa maisha ya wanaotegemea kupata
kipato katika zao hili unaonekana.




0 Comments