Mwenyekiti wa RIVACO, Bw. Lohay Langai (kushoto)
akizungumza
katika kikao cha pamoja kati ya TADB na Bodi ya RIVACO, kilichokuwa
kinajadili namna ya kukiwezesha chama hiko kuweza kununua nafaka kutoka
kwa wakulima wa mkoa wa Manyara. Wengine pichani ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga (katikati) na
Meneja wa Uendelezaji wa Biashara wa TADB, Bw. Geofrey Mtawa (kulia).
Na Mwandishi wetu, Manyara
Benki
ya Maendeleo ya Kilimo ya Tanzania (TADB) na Chama Kikuu cha Ushirika
Mkoani Manyara (Rift
Valley Cooperative Union - RIVACO) wapo kwenye mazungumzo
yatakayowezesha uhakika wa masoko kwa wakulima wa mahindi wa mkoani
Manyara ili kuboresha usalama wa chakula nchini.
Katika kikao cha pamoja kati ya uongozi wa TADB na Bodi ya RIVACO pande hizo mbili zinajadiliana
uwezekano wa kukiwezesha Chama hicho cha Ushirika kuweza kununua mahindi kutoka kwa wakulima wa
mkoani Manyara.
Akizungumza wakati wa kikao hicho cha pamoja,
Kaimu
Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga anasema kuwa katika
kuhakikisha usalama wa chakula nchini, TADB ipo kwenye mpango wa
kuikopesha RIVACO ili waweze kununua mahindi kutoka kwa
wakulima mkoani humo.
“Kwa kuzingatia malengo ya kuanzishwa kwetu, TADB tuna madhumuni ya kuisaidia RIVACO ili kuhakikisha
na kusaidia upatikanaji wa utoshelezi na usalama wa chakula ambao ni endelevu nchini Tanzania,” alisema.
Kwa
upande wake Bw. Lohay Langai ambaye ni Mwenyekiti wa RIVACO amesema
Chama chake kinataka kutumia
fursa za mikopo nafuu kutoka TADB ili waweze kutimiza lengo la Serikali
la kuhakikisha chakula kinabaki nchini ili kuongeza usala wa chakula.
“Fursa
za mikopo ya TADB inatupa nafasi ya kupewa mkopo kwa ajili ya kupata
mtaji kwa ajili ya uendeshaji,
uongezaji wa thamani na gharama za uhifadhi na masoko zitakazotuwezesha
kununua mahindi kutoka kwa wakulima hali itakayochagiza usalama wa
chakula nchini,” alisema.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi wa Biashara na Mikopo wa TADB, Bw. Augustino
Chacha amesema kuwa kwa
upande wa miundombinu ya masoko, TADB inatoa mikopo kwa minyororo ya
thamani kwa ajili ya maendeleo ya miundombinu ya masoko kama vile ujenzi
wa maghala ya kuhifadhi mahindi na miundombinu ya masoko na kugharamia
usafirishaji
wa malighafi na unga ulio tayari kwenda sokoni.
“Pia
Benki inagharamia uanzishaji wa mifumo ya upatikanaji wa taarifa za
masoko pamoja na kuwezesha
uhusiano wa masoko ya ndani na masoko ya kikanda na kugharamia mahitaji
mengineyo ya kuwezesha miundombinu ya masoko,” alisema Bw. Chacha.
Kwa muda mrefu sasa ukosefu wa mtaji kwa vyama vya ushirika nchini kumesababisha wafanyabiashara
kununua mazao mbalimbali na kuyauza nchi za nje hasa nchi za jirani hali inayosababisha usalama wa chakula nchini.

0 Comments