Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Chakula na Dawa
Tanzania (TFDA) Hiiti Sillo akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani)
kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Taasisi yake leo Jijini Dar es Salaam.
Picha zote na: Frank Mvungi - MAELEZO
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Chakula na Dawa
Tanzania (TFDA) Hiiti Sillo akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani)
kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Taasisi yake leo Jijini Dar es Salaam. Kulia
ni Meneja Majaribio ya Dawa na Ufuatiliaji kutoka Mamlaka hiyo Bi. Kissa
Mwamwitwa.
Frank Mvungi-Maelezo
Serikali
imewahakikishia wananchi kuwa dawa zilizopo katika soko zina ubora kwa asilimia
98 na itahakiksha zinaendelea kukidhi vigezo vya ubora kama zilivyokuwa wakati
zinasajiliwa kwa mujibu wa sheria, kanuni,miongozo na taratibu za udhibiti.
Kauli hiyo imetolewa
leo Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya chakula na Dawa
(TFDA) Bw. Hiiti Sillo wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliolenga
kueleza mikakati ya Mamlaka hiyo katika kudhibiti ubora na usalama wa chakula,dawa,vipodozi
na vifaa tiba ili kulinda afya za wananchi.
“Katika maabara ya
TFDA inayokidhi ithibati ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kati ya sampuli za
dawa 199 za Binadamu zilizochunguzwa,sampuli 184 sawa na asilimia 92.5 zilikidhi
vigezo vya ubora na sampuli za dawa 10 aina ya Ergometrine ya sindano ambayo ni
sampuli 5 sawa na asilimia 2.5 hazikufikia ubora kwa kuwa na kiasi cha kiambata
hai chini ya kiwango kinachokubalika.”Alisisitiza Sillo
Akifafanua Sillo
amesema kabla ya dawa kusajiliwa na TFDA na hatimaye kuruhusiwa kuingia katika
Soko,zinafanyiwa tathmini ya Ubora,Usalama na ufanisi sanjari na ukaguzi wa
mifumo ya utengenezaji bora Kiwandani na hizo ni hatua za awali za mifumo ya
udhibiti wa dawa duniani.
Pia Sillo aliongeza
kuwa dawa zinapokuwa katika soko zinafuatiliwa na TFDA kuona kama zinaendelea
kukidhi vigezo vya ubora hadi tarehe ya mwisho ya matumizi (expiry date) ambapo
utaratibu huu hujulikana kama Post- Marketing Surveillance au Market Control
kwa mujibu wa mwongozo wa shirika la Afya Duniani (WHO) na ulianza kuwekwa na
TFDA tangu mwaka 2007.
Katika utaratibu huo
kila mwaka sampuli za dawa za aina tofauti zinachukuliwa na wakaguzi kutoka
katika soko Zahanati,Vituo vya Afya, Hospitali,maduka ya dawa na maghala ya
kuhifadhia dawa ya umma na binafsi na kufanyiwa uchunguzi wa kimaabara.
Vigezo vinavyotumika
kuchagua dawa zinazofanyiwa ufuatiliaji ni pamoja na dawa zenye matumizi
makubwa,dawa za kutibu magonjwa ya makundi maalum kama watoto na akina mama
wajawazito,dawa zenye historia ya kushindwa kustahili mazingira mbalimbali ya
usafirishaji na utunzaji (unstable products)
Kwa kipindi cha mwaka
2012/2015 Sillo alibainisha kuwa dawa
zilizofanyiwa ufuatiliaji ili kuona ubora wake ni pamoja na dawa za kutibu
malaria,dawa aina ya vijiua sumu (Antibiotics) Dawa za kufubaza virusi vya
Ukimwi,dawa za kupunguza maumivu,dawa za kutibu kisukari,dawa za kutibu
magonjwa ya moyo,dawa za kuzuia kutoka damu nyingi wakati wa kujifungua aina ya
misoprostol.
Katika kipindi cha mwaka
2016/2017 hadi machi 2017, TFDA ilifuatilia katika soko,ubora wa dawa za
binadamu aina ya Albendazole vidonge,mchnaganyiko wa dawa ya vidonge aina ya
Diclofenac na paracetamol,dawa ya macho yenye mchanganyiko wa Dexamethazone na
Neomycin,dawa za mifugo aina ya Oxytetracycline 10% na 20 ambazo uchunguzi wake
uko katika hatua za mwisho na matokeo yatatolewa mara yatakapokuwa tayari.
Aidha Sillo
amesema kuwa mfumo wa kufuatilia usalama wa dawa katika soko unafanya kazi
vizuri hapa nchini tangu mwaka 1989 na umeendelea kuboreshwa ambapo oktoba 2016
tulianzisha mfumo wa utoaji taarifa za madhara ya dawa kielekroniki kwa kutumia
simu ya kiganjani.
Mamlaka ya Chakula
na Dawa Tanzania(TFDA) kwa mujibu wa Sheria ya Chakula,Dawa na Vipodozi,sura ya
219 ina jukumu la kudhibiti ubora na usalama wa chakula,dawa, vipodozi na vifaa
tiba ili kulinda Afya za wananchi.


0 Comments