MAKAMU MKUU wa
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Prof. Rwekaza Mukandala amewataka vijana
wanaohitimu kidato cha sita nchini wawe makini na wasikubali kusombwa na
mawimbi ya dunia.
Ametoa wito huo
jana (Jumamosi, Mei 14, 2017) wakati akizungumza na wahitimu 237 wa kidato cha sita
wa shule ya sekondari ya St. Joseph Cathedral kwenye mahafali ya sita ya shule
hiyo yaliyofanyika shuleni hapo, jijini Dar es Salaam.
Prof. Mukandala
alisema: “Kwa hatua mliyofikia kila mmoja anapaswa atafakari kwa kina wito wake
kimaisha. Kuweni makini, msisukumwe na mawimbi ya dunia na kujikuta mmepoteza
ndoto zenu,” alisisitiza.
“Kuhitimu
kidato cha sita si jambo dogo. Ni hatua ya kuwaongiza kujiandaa na utu uzima
ikiwemo kujiunga na elimu ya vyuo vya juu na kuingia kwenye ndoa. Ni muda wa kutathmini
yale uliyopitia na kutafakari maisha yako ya baadaye. Ni fursa ya kutoa
shukrani kwa Mungu, kwa wazazi na walimu ambao walifanya kazi kwa umakini na
kujitoa ili mfikie hatua nzuri mliyopo sasa,” alisema.
Alisema kuanzia
sasa kila mmoja wao anapaswa kujiamini, kujituma zaidi na kujiona kuwa ana
wajibu wa kujiletea maendeleo binafsi. “Mnapaswa kuepuka mwenendo wa kujiona mnyonge,
au mtu asiyeweza kutimiza ndoto zake. Jenga tabia ya kuwa makini na maisha
yako, jali mazingira yako na maendeleo yako,” alisisitiza.
Aliwataka
wahakikishe wanakuchukua hatua mahsusi na kupata taarifa sahihi kuhusu taaluma
wanazozitaka. Aliwataka wawe waadilifu na wenye heshima kwa watu wote lakini
pia akawaasa juu ya maisha ya kutaka kupata fedha kwa haraka na kujilimbikizia
mali.
“Epukeni rushwa
na ufisadi. Mnatakiwa kujua kuwa utu, maendeleo na maisha bora havipatikani kwa
fedha ingawa nayo ni muhimu katika maisha. Msitegemee kuishi kwa kuzingatia
mambo makubwa yanayopimika kwa fedha,” alisema.
Akitoa mfano,
Prof. Mukandala alisema: “Msikimbilie kuwa na magari mengi bila kujua nani
atayatumia, au kujenga nyumba kubwa bila kujua nani atahitaji nafasi hiyo
kubwa. Unanunua simu mbili au tatu bila kufikia athari zake kwa afya na
mahusiano yako. Kabla hujachukua hatua ni lazima ujiulize, je unakihitaji kitu
hicho? Kuweni makini na matumizi ya fedha badala kujilimbikiza vitu vya anasa,”
alisema.
Aliwataka
wazazi waendelee kuwalea vema vijana hao kwa sababu bado wanahitaji usimamizi wa
wazazi kwa kila hatua wanayosonga mbele. “Tuendelee kuwaunga mkono watoto wetu kwa
sababu jukumu letu kama wazazi bado liko palepale,” alisema.
Mapema, akimkaribisha mgeni rasmi kuzungumza na hadhira
iliyokuwepo, Mkuu wa Shule ya St. Joseph Cathedral, Sista Theodora Faustine
alisema St. wanafunzi waliohitimu jana ni 237 ambao kati yao wavulana ni 140 na
wasichana ni 97 waliokuwa wakichukua michepuo ya ECA, EGM, CBG, HGE, HGL, PCM, PCB
na PGM.
Alisema anaamini
kwamba wahitimu wote watakuwa na sifa za kujiunga na vyuo vikuu mwaka huu kwa
sababu shule hiyo imekuwa ni ya kwanza yenye wingi wa ufaulu kuliko shule
yoyote mkoani Dar es Salaam. “Tumekuwa tukipata wanafunzi bora kitaifa mara kwa
mara na mwaka jana tulipata wanafunzi bora kutoka michepuo ya PCB na ECA,” alisema.
Sista Theodora
alisema wamekuwa wakifaulisha wanafunzi zaidi ya 250 kwa mwaka na kwa maana
hiyo, wameweza kuandaa vijana 250 kuingia kwenye vyuo vikuu vya ndani na nje ya
nchi. Akifafanua kuhusu malengo ya shule, Mkuu huyo wa shule alisema lengo lao
ni kutoa elimu bora kwa watoto wa Kitanzania na kuwandaa kuwa wawajibikaji kwa
Mungu na kwa Taifa lao.
Kwa upande wake, mwakilishi wa wazazi wenye watoto
waliohitimu kwenye mahafali hayo, bw. Eric Shigongo alisema kila mhitimu anayo
ndoto yake ambayo anapaswa kufanya kila awezalo kuhakikisha ndoto yake
inatimia.
“Unao uwezo wa
kuchagua (power of choice) kilicho chema kwa ajili ya maisha yako ya baadaye.
Nasisitiza kwa sababu najua kila mmoja wenu ana ndoto yake ya kufika mahali
fulani. Hakikisha unatimiza ndoto hiyo, haijalishi utapitia mazingira gani,”
alisema.
Alisema kwake
yeye anawaona vijana waliohitimu kwamba ni washindi (champions) na aliwaeleza
hivyo wiki tatu kabla ya kuanza mitihani yao. Hata hivyo, aliwaasa kwamba wawe
tayari kukosa mambo mengine kama kweli wanataka kufanikiwa maishani mwao.
“kama unataka
kufanikiwa maishani, huna budi kujinyima mambo mengi ili uweze kupata kile
unachokitaka. Najua mmemaliza kidato cha sita lakini safari yenu ya maisha
ndiyo kwanza imeanza. Ninaamini wako watu hapa watakaotusaidia kutatua
changamoto za nchi hii, wako madaktari hapa, wako wahandisi, wako
wafanyabiashara na yuko Rais ajaye wa Tanzania, tena Rais mwanamke kutoka
katika kundi hili,” alisema.
Katika mahafali
hayo, mwanafunzi Kauthar Said aliibuka mwanafunzi bora na kupewa zawadi ya
kompyuta mpakato (laptop) na wanafunzi wa mchepuo wa PCM, walipewa zawadi ya
keki na Mkuu wa Shule kwa kuwa ni darasa ambalo halijawahi kuwa na kesi yoyote ya
utovu wa nidhamu katika kipindi cha miaka miwili waliyoakaa shuleni hapo.
IMETOLEWA:
JUMAPILI, MEI 14,
2017.

0 Comments