Naibu Katibu Mkuu
wa CCM Zanzibar akizungumza na wazee
pamoja na wamiliki wa mashamba ya uchimbwaji wa mchanga katika jimbo la Donge
Wilaya ya Kaskazini “B” Unguja.
Baadhi ya Wazee wa
CCM wa Jimbo hilo wakifuatilia kwa makini mazungumzo ya kutafuta suluhu katika
mgogoro wa wananchi na serikali katika maeneo ya kuchimbwa mchanga kwenye eneo
hilo.
Baadhi ya Wazee wa
CCM wa Jimbo hilo wakitoa ushauri wao mbele ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar,
Dkt. Abdalla Juma Saadala “ Mabodi” katika kikao hicho.
NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
BAADHI ya Wazee wa Chama
Cha
Mapinduzi pamoja na wamiliki wa mashamba ya kuchimbwa rasilimali ya
mchanga Jimbo la Donge Wilaya ya Kaskazini “B” wamekishauri Chama
hicho kuingilia kati
mgogoro wa serikali kuwazuia wananchi wasichimbe mchanga katika maeneo
ya
wilaya hiyo.
Ushauri huo wameutoa kwa nyakati
tofauti mbele ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt. Abdalla Juma Saadala “
Mabodi” katika kikao cha kutafuta suluhu ya kutatua mzozo huo huko Tawi la CCM
la Donge Mbiji Unguja.
Mkaazi wa Kijiji hicho, Bw. Bakar
Juma Nahoda alisema kitendo cha Serikali kuzuwazuia wananchi wasichimbe mchanga
kwa baadhi ya maeneo huku serikali hiyo ikiruhusu na kusimamia zoezi hilo
liendelee kwa malipo maalum katika maeneo mengine, hatua hiyo imehatarisha
ajira za baadhi ya vijana na wananchi waliokuwa wakitegemea sekta hiyo kama
eneo la kujipatia kipato.
Bw. Juma alifafanua kwamba baada
ya serikali kuwakata wananchi wasiendelee kuchimba mchanga katika maeneo hayo
kwa madai ya kuepuka uharibifu wa mazingira, lakini zoezi hilo liliendelea kwa
njia nyingine ya kuchimbwa mchanga kwa gharama maalum ya fedha zinazoingia
serikalini.
Alisema toka serikali
ilipotangaza rasmi utaratibu wa kuchimbwa kwa rasilimali hiyo na kuweka ulinzi
mkali kwa baadhi ya maeneo wananchi wengi wa jimbo la Donge na Vijiji vyake
wamekuwa na changamoto za ukali wa maisha hivyo aliiomba CCM iingilie kati
mgogoro huo kwa lengo la kuupatia ufumbuzi wa kudumu.
Naye Ibrahim Mohamed Khamis alisema mbali na
tatizo hilo pia kumeibuka changamoto nyingine ya baadhi ya wanasiasa wa vyama vya upinzani
kutumia mgogoro huo kujinufaisha kisiasa kwa kuwashawishi baadhi ya vijana
warudishe kadi za CCM bila kujali athari za baadae zinazotokana na uamuzi huo.
Aidha ameituhumu Kamati iliyoundwa na Rais wa
Zanzibar na mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein kwa ajili
ya kushughulikia mgogoro huo kuwa iliwapuuza wananchi na kushindwa kufuata ushauri wa Wazee wa CCM wa jimbo hilo
waliotaka shughuli zote za uchimbaji wa mchanga katika eneo hilo zisitishwe
hadi hapo itakapopatikana suluhu ya kudumu.
“ Kama kweli serikali ina nia
safi ya kuzuia athari za mazingira zinazotokana na uchimbaji mchanga basi na
wao wasingeendelea kusimamia uchimbaji wa mchanga kwa baadhi ya maeneo
waliowaondosha wananchi.
Pia tunaamini CCM, serikali kuu
na wananchi wakikaa meza moja kujadiliana juu ya suala hili basi kila upande
utaridhika juu ya maamuzi yatakayopatikana hapo lakini yawe na suluhu ya
kuwapatia wananchi sehemu nyingine ya ajira ya kujipatia kipato chetu cha kila
siku.”, alisema Mohamed miongoni mwa wakaazi wa kijiji hicho.
Akizungumza Naibu Katibu Mkuu wa
CCM Zanzibar, Dkt. Abdalla Juma Saadala “Mabodi” aliahidi kuyafanyia kazi
mapendekezo na ushauri uliotolewa na Wazee pamoja na wamiliki wa mashamba
yaliyozuiliwa kuchimbwa mchanga katika eneo hilo ili wananchi wapate haki zao
huku eneo lililofanyiwa tathimini za kitaalamu juu ya uchimbwaji wa mchanga
nalo libaki salama.
Nimesikia kwamba wapinzani tayari
wameshajipenyeza katika mgogoro huu kwa kushawishi wananchi waigomee serikali, jambo
ambalo sio sahihi kama kweli wana nia wangeonyesha njia ya kutatua jambo hili
kupitia njia ya mazungumzo na sio kukuza mgogoro.”, alieleza Dkt. Mabodi na
kuongeza kwamba serikali iliyopo madarakani Chini ya Dkt. Shein ipo makini na inajali
na kuheshimu mawazo ya wananchi wote na mzozo huo utamalizika kwa amani hivi
karibuni.
Naibu Katibu Mkuu huyo, alisema
alisema lengo la serikali sio kuwaumiza wananchi bali ni kuwaongoza katika
mambo mema hasa ya maendeleo, hivyo waendelee kuvumilia wakati CCM ikitafuta ufumbuzi
wa kudumu juu ya tatizo hilo.
Hata hivyo Dkt. Mabodi katika
Kikao hicho alifuatana na viongozi na wajumbe wa Baraza la Wazee wa CCM
Zanzibar wakiongozwa na Mwenyekiti wa Baraza hilo Bi. Khadija Jabir.
0 Comments