Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalim
(Jovina
Bujulu- MAELEZO)
Wizara
ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto kupitia Mpango wa Taifa wa
Chanjo imevuka lengo la kutoa chanjo na kuimarisha huduma nyingine za afya nchini.
Huduma hizo ni pamoja na udhibiti magonjwa
ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza, magonjwa yaliyokuwa hayapewi
kipaumbele,huduma ya afya ya uzazi na mtoto, lishe, pamoja na utoaji wa elimu
ya afya kwa umma.
Waziri
mwenye dhamana na wizara hiyo Mhe. Ummy Mwalimu amebainisha hayo hivi karibuni alipokuwa
akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa kipindi cha Mwaka
wa Fedha 2017/18 mjini Dodoma.
Aliendelea
kusema kuwa wizara yake imehakikisha
kuwepo kwa chanjo za kutosha ambapo jumla ya shilingi bilioni 18 zimetumika kununua
na kusambaza chanjo kwa watoto na makundi mengine katika mikoa na Halmashauri
zote nchini.
“Utoaji
wa huduma za uhakika wa chanjo umewezesha nchi yetu kuwa miongoni mwa nchi
zilizofanya vizuri kwa kipindi cha mwaka 2016, ambapo tumeweza kuvuka lengo kwa
kufikia kiwango cha chanjo cha asilimia 97” alisema Ummy.
Aidha,
Wizara imenunua magari tisa (09) kwa ajili ya kusambaza chanjo na majokofu 317
ya kutunzia chanjo hizo kwenye vituo vya
huduma za afya nchini.
Katika
kuhakikisha kuwa huduma kwa wananchi inaboresha, Wizara ya Afya kupitia Mpango
wa Taifa wa Kudhibiti Magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele imeendelea kugawa dawa za kingatiba. Dawa hizo ni pamoja
na za matende, mabusha, usubi, trakoma, kichocho na minyoo katika Halmashauri
71 zenye maambukizi ya magonjwa hayo.
Huduma
hiyo iliwezesha wananchi milioni 14.3 kufikiwa
na wagonjwa 805 katika Halmashauri za Temeke na Ilala, jijini Dar es salaam na
watu 100 kutoka mkoa wa Mwanza
walifanyiwa upasuaji wa mabusha na matende bila malipo.
Wizara
pia imeendelea na mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria kwa kusambaza dawa za
kutibu na vipimo vya kupima (MRDT) katika mikoa 26 ya Tanzania Bara, dozi za
dawa mseto na vitepe vya MRDT vya shiilingi milioni18 zimenunuliwa na
kusambazwa katika vituo vya afya.
Katika
kuhakikisha ugonjwa wa malaria unatokomezwa, wizara imeendelea kuhamasisha matumizi ya kipimo cha MRDT na kunyunyiza dawa ya ukoka katika mikoa
ya Kanda ya Ziwa ya Kgera, Mwanza, Mara
na Geita ambayo ina maambukizi makubwa ya malaria na kugawa vyandarua milioni
2.6 vyenye viuatilifu katika Halmashauri ya Kilombero mkoani Morogoro na Halmashauri zote za jijini
Dar es salaam.
Akizungumzia
hali ya ugonjwa wa kifua kikuu, Waziri Ummy alisema kuwa kwa sasa huduma za
matibabu ya ugonjwa huo zimeimarishwa na kusogezwa karibu na wananchi kutoka
hospitali moja ya Kibong’oto hadi kufikia vituo 18. Huduma za maabara pia
zimeboreshwa kwa kuimarisha maabara za Kandaya-Mbeya, Bugando-Mwanza, hospitali
ya rufaa mkoa wa Dodoma na Kibong’oto mkoani Kilimanjaro.
Kuhusu
hali ya ugonjwa wa UKIMWI nchini , Wazii Ummy alisema kuwa wizara yake imeendelea kutoa ushauri nasaha na
kuwahimiza wananchi kupima mara kwa mara ili kujua hali ya afya zao ambapo kwa kipindi
cha mwaka 2016 jumla ya watu milioni 7.4 walipata ushauri nasaha na kupima VVU.
Katika
kupambana na magonjwa yasiyoambukiza, waziri alisema kuwa wizara yake imeandaa
Mkakati wa Kitaifa wa kupambana na magonjwa hayo wa mwaka 2016-2020 ambao
ulizinduliwa Dodoma mwaka 2016.
Mkakati
huu unafuatia ongezeko kubwa la magonjwa hayo ambayo ni kisukari, shinikizo la
damu na magonjwa ya moyo. Ili wananchi waweze kukabiliana na magonjwa hayo, wizara
imeanzisha kampeni ya kitaifa ya kuhamasisha wananchi kufanya mazoezi, kupima
afya mara kwa mara na kuzingatia ulaji wa chakula unaofaa.
Katika
kipindi cha mwaka jana , huduma ya afya ya uzazi na mtoto imeimarishwa kwa
kuandaa Mpango Mkakati wa miaka mitano wa 2016-2020 unaolenga kuboresha afya ya uzazi, watoto na
vijana na kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi hadi kufikia 292 kwa kila vizazi
hai 100,000 ifikapo 2020. Kwa sasa vifo
hivyo ni 556 kwa kila vifo hai 100,000.
“Katika
kutekeleza mkakati huo, wizara imezingatia maeneo makuu matatu ambayo ni
hududma ya uzazi wa mpango, huduma wakati wa ujauzito na huduma wakati wa
kujifungua”. Alisema waziri Ummy.`
Akizungumzia
upatikanaji wa huduma ya uzazi wa mpango Waziri Ummy alisema wizara yake
imefanya jitihada za kuhakikisha huduma hiyo inapatikana kwa watu wote wanaostahili
ambapo kwa kipindi cha July mwaka 2016 na Machi 2017, jumla ya watu 357,244
wamefanikiwa kupita huduma kupitia hospitali za mikoa na watu 2,509,280 walifanikiwa kupata huduma hiyo kupitia
vituo vya afya.
Aidha,
Waziri alitoa wito kwa wakina mama wajawazito kuhudhuria kliniki angalau mara
nne katika kipindi cha ujauzito na kuzuia vifo vitakanavyo na uzazi
vinavyoepukika, lengo la Serikali ni kufikisha asilimia 70 ya wanawake
wajawazito kuhudhuria kliniki na kupata huduma ifikapo 2020 ili kunusuru maisha
ya mama na mtoto.

0 Comments