Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe
Magufuli (wa tano kulia) akikata utepe unaoashiria uzinduzi wa mradi wa
matrekta ya URSUS SA unaosimamiwa na Shirika la Taifa la Maendeleo la Taifa
(NDC) 21 Juni, 2017 katika eneo la TAMCO lililopo Kibaha, Mkoani Pwani.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe
Magufuli akiwasha moja ya matrekta mara baada ya kuzindua ya mradi wa matrekta
ya URSUS SA unaosimamiwa na Shirika la Taifa la Maendeleo la Taifa (NDC) 21
Juni, 2017 katika eneo la TAMCO lililopo Kibaha, Mkoani Pwani.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe
Magufuli akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa Kiwanda cha Kuunganisha Matrekta
lililopo eneo la TAMCO Kibaha Mkoani Pwani 21 Juni, 2017.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe
Magufuli akiwa (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Watendaji wa Shirika
la Taifa la Maendeleo (NDC) mara baada ya kuzindua ya mradi wa matrekta ya
URSUS SA unaosimamiwa na NDC 21 Juni, 2017 katika eneo la TAMCO lililopo
Kibaha, Mkoani Pwani.
Na Benedict
Liwenga-WHUSM
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amelipongeza
Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) kwa ufanisi mkubwa walioufanya wa kuanza
kuunganisha matrekta aina ya URSUS ambayo vifaa vyake hutengenezwa nchini
Poland.
Pongezi
hizo amezitoa leo Wilayani Kibaha Mkoani Pwani wakati akizindua mradi wa
matrekta hayo pamoja na uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa Kiwanda cha
Kuunganisha matrekta katika eneo la TAMCO, ambapo baadhi ya mambo aliyoyaongea ni
kuutetea mradi huo ili ulete maendeleo kwa Watanzania.
Rais
Magufuli ameeleza kuwa muda mwingi miradi ya NDC imekuwa ikikwama lakini amefurahishwa
na suala la uunganishaji matrekta na kuona kuwa sasa shirika hilo limekuwa
jipya huku akiwataka watendaji wa shirika hilo kuchapa kazi kwa bidii ili.
“Sasa
naiona NDC hii mpya, nawapongeza, naomba sasa msinirudishie mawazo yale mabaya
niliyokuwa nawazia kuhusu NDC. Sasa yale mawazo nayabadilisha, kwa hiyo tuwe na
NDC mpya yenye kutoa matunda. Anzeni sasa kubadilika na muwe Shirika kweli la Taifa”,
alisema Dkt. Magufuli.
Sambamba
na hayo, Rais Magufuli amewapongeza Marais Wastaafu, Mhe. Benjamini William
Mkapa pamoja na Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete huku akilitaka shirika hilo
kuendelea na mipango mingine ya baadaye ikiwemo ya kuunganisha magari makubwa
yakiwemo mabasi ili kukuza maendeleo ya viwanda nchini na kutengeneza ajira kwa
Watanzania.
Kuhusu
madai yanayodaiwa na Kampuni ya URSUS ya nchini Poland, Rais Magufuli ameitoa
wasiwasi kampuni hiyo kwamba madai hayo atayamaliza katika utawala wake na
kuwataka waendelee na awamu ya pili ya uunganishaji wa matrekta hayo.
“Huu
mradi mimi nimeshaubeba kikamilifu na wala hautakwama, na hii nataka niwaeleze
ukweli tu, labda nyie ndo muukwamishe, kwahiyo haya matrekta yatasaidia katika
kilimo”, alisema Dkt. Magufuli.
Amesema
kwamba, kuanza kutumika kwa matrekta hayo kutaisaidia sekta ya kilimo nchini
kusonga mbele kwani asilimia 80 ya Watanzania wanategemea kilimo lakini
kimekuwa hakiendi kwa haraka kutokana na matumizi ya jembe la mkono, hivyo
matumizi ya matrekta yataondoa adha hiyo kwa wakulima na kuleta ajira yenye
manufaa nchini.
Aidha,
Rais Magufuli amewataka Wizara ya Kilimo na wawekezaji wa Kampuni hiyo ya URSUS
kuangalia suala la bei za matrekta hayo ziwe nafuu ili kuwawezesha wakulima
kumudu bei na pia waruhusu kuyauza kwa mkopo utakaolipwa kidogo kidogo.
Kuhusu
suala la Kodi, amesema kwamba Serikali imetoa utitili wa kodi ambapo tayari
kodi na tozo zipatazo 80 katika kilimo zimeondolewa lengo likiwa kuwavutia watu
kuthamini kilimo.
“Suala
la pembejeo katika nchi hii ni hovyo, tumeanza kufuatilia na tumebaini kuwa kuna
pembejeo hewa nyingi, lakini hili tunalishughulikia na tayari kuna watu
wanalifanyia kazi”, alisema Dkt. Magufuli.
Kwa
upande wake Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Charles Mwijage
amesema kuwa, Serikali sasa inaleta viwanda vya nguo na vya kuunganisha magari
ambapo tayari Kampuni ya TATA imeshakubali kufanya hilo na kwamba tayari fedha
ya kutosha imetengea katika bajeti ya mwaka 2017/2018 kwa ajili ya kuweka
mazingira mazuri ya viwanda.
“Naibu
Balozi wa Poland amenieleza kuwa anataka kushirikiana na sisi ili katika
kipindi kisichizidi miaka miwili kuwe hakuna mtu anayelima kwa jembe la mkono”,
alisema Mwijage.
Naye
Naibu Mwenyekiti wa Bodi ya NDC, Bw. Peter Chisawillo alisema kuwa, kiwanda
hiko kitaunganisha jumla ya matrekta 2,400 ambapo kuna aina tatu za matrekta
yanayounganishwa kiwandani hapo yenye uwezo wa ‘horse power’ 50, 65, 75 na 85.
Ameongeza
kuwa, kiwanda hiko kinatarajia kuajiri wafanyakazi 100 na kwa kuanzia kiwanda
kimeajili wafanyakazi 18 na baadhi yao wanatarajiwa kupelekwa nchini Poland kwa
ajili ya kupatiwa mafunzo kuhusu masuala ya matrekta.
Mradi
wa matrekta ya URSUS ni mradi kati ya Serikali ya Tanzania kupitia Shirika la
Taifa la Maendeleo (NDC) na Serikali ya Poland, unahusisha mkopo wa riba nafuu wa
Dola za Kimarekani milioni 55 kutokana na mkataba uliosainiwa mwaka 2015 nchini
Poland wenye ushirikiano katika masuala ya kiuchumi ambapo Kampuni ya
Utengenezaji Matrekta ya URSUS SA ya nchini humo imedhamiria kuisaidia Tanzania
katika sekta ya kilimo.




0 Comments