Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia
Suluhu Hassan akihutubia kwenye shughuli za mazingira ambapo nyavu
zilizotumika kwenye uvuvi haramu zimeteketezwa katika dampo la Buhongwa,
wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan ameagiza vyombo vya dola
nchini kuwakamata bila kuwaonea huruma viongozi watakaobainika
kujihusisha au kuhujumu kazi ya kupambana na uvuvi haramu nchini.
Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu
Hassan ametoa agizo hilo wakati akishiriki katika zoezi la uchomaji wa
zana haramu za uvuvi 5,662 kwenye eneo la Buhongwa wilayani Nyamagana
mkoani Mwanza zilizokamatwa katika Ziwa Victoria.
Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu
Hassan amesema kumekuwa na tabia ya baadhi ya viongozi kushiriki katika
shughuli za uvuvi haramu hivyo inabidi wachukuliwe hatua ili kukomesha
kabisa tatizo la uvuvi haramu katika Ziwa Victoria na maeneo mengine
nchini.
Ameeleza kuwa uvuvi haramu katika
Ziwa Victoria umekuwa ni tatizo sugu na hali ambayo imesababisha
kupungua kwa samaki na mapato kwa Serikali ambayo ni muhimu kwa ajili ya
shughuli maendeleo.
Amesema licha ya uvuvi haramu
kupunguza mapato ya Serikali kutoka kwenye viwanda hali ya ajira nayo
sio nzuri zilizokuwa zinatoka kwenye viwanda ambazo zimepungua kwa
asilimi 49.
Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu
Hassan amepongeza kazi kubwa iliyofanyika ya ukamataji wa zana haramu za
uvuvi katika Ziwa Victoria na amewahakikishia viongozi wa mkoa wa
Mwanza kuwa Serikali ipo pamoja nao katika kazi hiyo.
“Serikali yenu itaendelea
kushirikiana nayi katika kuhakikisha kuwa rasilimali za uvuvi katika
Ziwa Victoria zinaendelea kuwepo kwa kuendelea kutoa fedha na vitendea
kazi ili kuongeza ufanisi katika utendaji wa kazi kwa lengo la kuhifadhi
ziwa Victoria” Amesisitiza Makamu wa Rais.
Kwa upande wake, Mkuu wa mkoa wa
Mwanza John Mongela amesema oparesheni za uvuvi haramu katika Ziwa
Victoria zitaendelea kuimarishwa ipasavyo mkoani Mwanza mpaka vitendo
hivyo vikomeshwa.
Amesema mkoa wa Mwanza ulikuwa
na viwanda Sita vya kuchakata samaki lakini kutokana na kupungua kwa
samaki katika Ziwa Victoria ni viwanda Vinne tu mpaka sasa ndio
vinafanya kazi hali ambayo imepunguza kwa kiasi kikubwa mapato kwa
Serikali na ajira kwa vijana mkoani huo.
Mkuu huyo wa Mkoa wa Mwanza John
Mongela ameeleza kuwa kutokana na viwanda hivyo kusitisha shughuli za
uzalishaji zaidi ya watu mamia ya watu wamekosa ajira.



0 Comments