Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na
Michezo Mhe. Dkt. Harrison G. Mwakyembe amempongeza Mwenyekiti wa Baraza la
Michezo la Taifa (BMT) Bw. Dionis Malinzi kwa hatua kadhaa ambazo baraza lake
limeanza kuchukua katika kusimamia michezo nchini, likiwemo zuio kwa viongozi
kuwa na kofia mbili kwenye mchezo mmoja.
Katika salamu alizomtumia kiongozi huyo wa BMT jana jioni, Dk. Mwakyembe
amesema hatua hizo zimeonesha uhai, uhalali na hitaji la uwepo wa BMT kwa
maendeleo ya michezo nchini.
Dk. Mwakyembe amesema Wizara haitarajii tena kuona kiongozi katika mchezo
wowote ule nchini kuwa na kofia mbili kinyume na sheria na kanuni zilizopo,
huku BMT ikiangalia pembeni na kuinyamazia hali hiyo.
Waziri Mwakyembe vilevile amesema Wizara haitarajii kuona chombo chochote cha
michezo nchini kikikiuka Kanuni na Sheria za nchi bila kuchukuliwa hatua
stahiki kwa kisingizio kuwa kinawajibika kwa vyombo vya kimataifa, kwani
kisingizio hicho ni batili kikatiba na kisheria hivyo hakiwazuii BMT kutekeleza
wajibu wao kwa mujibu wa Sheria za nchi.
Aidha amewapa pole BMT kwa kuondokewa
na mwanamichezo maarufu nchini Ally Mohammed, a.k.a. Ally Yanga, aliyefariki
dunia jana (Jumanne) kwa ajali ya gari wilayani Mpwapwa.
"Tumepoteza kifaa muhimu katika
kuhamasisha michezo nchini na nifikishieni salamu zangu za rambirambi kwa
ndugu, jamaa, marafiki wa marehemu na wanamichezo wote nchini", Dk.
Mwakyembe amesema na kuwatakia BMT mafanikio katika utekelezaji wa majukumu
yao.
0 Comments