Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima Dkt. Fidelis Mafumiko akizungumza na wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Taasisi hiyo katika mkutano uliofanyika jana Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Naibu Mkurugenzi wa Taasisi hiyo Dkt. Kassim Nihuka na kulia ni watumishi wa taasisi hiyo.
Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima wakimsikiliza Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo wakati wa mkutano wa baraza hilo uliofanyika jana Jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt.
Leonard Akwilapo akiwa kwenye picha ya pamoja na wajumbe wa Baraza la
Wafanyakazi wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima baada ya kufungua mkutano wa
Baraza hilo jana Jijini Dar es Salaam.
Picha zote na Fatma Salum (MAELEZO)
Na Fatma Salum - MAELEZO
Serikali imetoa rai kwa Taasisi ya Elimu
ya Watu Wazima nchini (TEWW) kuandaa mkakati wa kusaidia kupunguza idadi ya
watu wasiojua kusoma na kuandika.
Rai hiyo imetolewa jana Jijini Dar
es Salaam na Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Leonard Akwilapo
wakati akifungua mkutano wa nane wa Baraza la Wafanyakazi la Taasisi hiyo.
Akizungumza na wajumbe wa Baraza
hilo, Dkt. Akwilapo aliitaka TEWW kuandaa utaratibu mzuri wa kuwafikia wananchi
wengi ambao hawajui kusoma na kuandika ili waweze kupata elimu kupitia taasisi
hiyo.
“Ongezeko la wasiojua kusoma na
kuandika linaelekea kuwa tatizo kubwa hapa nchini, hivyo natoa rai kwa taasisi
hii kujadili namna ya kuendeleza kampeni za kisomo na kutoa mafunzo kwa
wawezeshaji wa programu za kisomo ili kukabiliana na tatizo hilo.” Alisema
Akwilapo.
Sambamba na hilo Dkt. Akwilapo aliwasisitiza
watumishi wa taasisi hiyo kufuata sheria, kanuni na taratibu za uendeshaji wa
shughuli zake ili kufikia malengo waliyojiwekea na kuleta matokeo chanya kwenye
sekta ya elimu nchini.
Aidha Katibu Mkuu huyo aliIshauri TEWW
kuandaa utaratibu mzuri wa kuwasaidia kielimu wanafunzi wa kike walioshindwa
kuendelea na masomo kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo kulazimishwa kuolewa
au kupata ujauzito.
Kwa upande
wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima Dkt. Fidelis Mafumiko
alisema kuwa taasisi hiyo inashirikiana na wadau mbalimbali katika kuendesha
programu za elimu kwa vijana na watu wazima walikosa elimu kupitia mfumo rasmi.
Alieleza kuwa program hizo ni
pamoja na programu ya kuzuia ndoa za kulazimishwa za utotoni (Child Early and
Forced Marriages) inayoendeshwa kwa kushirikiana na Taasisi ya Commonwealth of
Learning ambayo imepanga kuwafikia walengwa 3000 katika mikoa ya Lindi, Rukwa
na Dodoma.
Pia Dkt. Mafumiko alisema kuwa TEWW
kwa kushirikiana na UNICEF wanaandaa programu kwa ajili ya vijana walio nje ya
mfumo rasmi wa shule ikilenga kuwafikia vijana wapatao laki tano ndani ya miaka
mitatu katika mikoa ya Tabora, Katavi, Geita, Rukwa, Dodoma, Simiyu, Shinyanga,
Singida, Lindi na Manyara.
Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima
ilianza mwaka 1975 na ipo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na
ina jukumu la kutoa mafunzo kwa wataalamu wa Elimu ya Watu Wazima na kutoa
elimu kwa makundi mbalimbali ya watu katika jamii wakiwemo waliokosa fursa ya
kupata elimu katika mfumo rasmi.





0 Comments