Jovina Bujulu na Benjamin
Sawe-MAELEZO
Baadhi ya wasomi na
wananchi wameisifu bajeti ya Serikali kwa mwaka 2017/18 wakisema kuwa imelenga
kumkomboa mwananchi na imeakisi ahadi za Rais za kusaidia Tanzania ya uchumi wa
viwanda.
Akizungumzia bajeti hiyo,
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Dk. Benson Bana amesema kuwa bajeti
hiyo inajibu maswali mengi yaliyo kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi na Mpango wa Maendeleo ya Miaka Mitano 2020/21 na Dira ya Taifa ya Mwaka 2020/25 na kwamba ni yenye kutegua
vitendawili vinavyowakabili wananchi katika kujiletea maendeleo.
‘’Kwa sura ya bajeti
ilivyo ni bajeti yenye ukombozi kwa mwananchi wa kawaida kwa sababu inagusa
masuala ya kupunguziwa kodi kwenye pembejeo, vyakula, kilimo, miundombinu,
umeme na maji’’, amesema Dk Bana.
Naye Dk Bashir Ally ambaye
ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ameipongeza bajeti hiyo na kushauri
kuwa baada ya kupitishwa, mchakato wa utekelezaji uanze kwa hamasa ya kisiasa,
kitaaluma na kijamii ili kufikia malengo yake.
‘’Unaweza kuwa na mpango
mzuri, lakini ikiwa watekelezaji ni wala rushwa, wazembe, na wasiofuata sheria,
wala kulipa kodi ni vigumu kufikia
malengo ya bajeti hiyo’’ alisema Dk. Bashir.
Aliongeza kusema kuwa
bajeti hii inajenga msingi wa uchumi wa viwanda kwa kuboresha miundombinu ya
reli ya kisasa, bandari, , kulinda
viwanda vyetu na kuwekeza kwenye mafunzo
ya vijana kutaongeza ari ya kujenga uchumi wa kati na wa viwanda.
Wakati huo huo Mtafiti na Mtaalam wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam Prof. Haji Semboja alisema kitendo cha Serikali kuondoa Kodi ya ngezeko
la Thamani (VAT) kwa wasafirishaji kutazivutia nchi ambazo hazina bandari kutumia
bandari na kuleta kuongeza ajira kwa Watanzania.
Alisema kuondoa kodi ya tozo
ya leseni ya barabarani kutairahisishia serikali ukusanyaji wa mapato na
gharama za ukusanyaji wa kodi hizo
utakuwa ni mdogo ila akaonya kuwa inaweza kuongeza gharama kwa yule ambaye
ataendesha gari mara kwa mara.
Akingea na Idara ya Habari
kwa njia ya simu, Mhadhiri wa ChuoKikuu Huria chaTanzania (OUT) Dkt. Damas
Ndumbaro ametaja uwekezaji katika miundombinu, kuondolewa kwa tozo ya kodi ya
leseni ya barabarani na punguzo la kodi katika mazao ni mambo muhimu
yanayopeleka faraja kwa wananchi na yatachochea maendeleo kwa kiwango kikubwa.
“Karibu asilimia 80 ya
watanzania wanaishi vijijini na wanategemea kilimo sasa nafuu ya kodi katika
mazao ya kilimo itasaidia sana kuwahamasisha wakulima na kuwainua kiuchumi
lakini pia mazao hayo yatatumika katika viwanda mbalimbali ambavyo vinaanzishwa
nchini na kuongeza ajira”, alieleza Dkt. Ndumbaro.
Kuhusu kodi ya leseni ya
barabarani, Dkt. Ndumbaro alisema kuwa hiyo ni nafuukubwa kwa watu wenye magari
na vyombo vingine vya moto kwani watalipia gharama katika mafuta na hivyo
kumfanya mtu alipe kwa kadiri ya anavyotumia chombo chake.
Kwa upande wake Shehe wa
Dar es Salaam, Alhaji Musa Salum alisema bajeti hiyo ni ya kizalendo na
kimaendeleo kwani imewapa watanzania unafuu na kuwasihi wananchi kuipokea na
kuitendea haki kwani imekuja kuboresha maisha yao.
Mmoja wa Wakulima wa
Tumbaku na mazao ya chakula, Bw. John Pinini kutoka Tabora ameeleza
kufurahishwa na bajeti na kutoa wito kwa Watanzania kuipokea na kuhakikisha
wanashirikikatika utekelezaji wakeikiwemo kuhakikisha wanalipa kodi stahili kwa
mujibu wa sharia na taratibu.
Waziri wa Fedha na
Mipango, Dkt. Philip Mpanga jana alisoma mapendekezoya bajeti kwa mwaka wa
fedha 2017/2018 yenye thamani ya shilingi trilioni 31.7 ambapo miongoni mwa
vipaumbele ni pamoja na kuendeleza ukuaji wa uchumi na kujenga uchumi wa kipato
cha kati, ujenzi wa miundombinu ya kiuchumi, kuboresha kilimo cha mazao, mifugo
na uvuvi na kuongeza ubora wa elimu, huduma za afya, maji na umeme.


0 Comments