Msafiri Mmassy kutoka Ofisi ya Kamishna msaidizi nyanda za
juu Kusini Magharibi akieleza umuhimu wa kulipa kodi ya pango la Ardhi kwa
waandishi wa habari (hawako pichani) akiwa na Shenya Magori.
Ofisi ya Kamishna wa
Ardhi Msaidizi Kanda ya nyanda za juu Kusini imekusanya jumla ya Tsh. 5.8
bilioni kodi ya pango la ardhi kwa kipindi cha kuanzi Julai 2016 hadi mei 2017 ikishirikiana
na Halmashauri 34 zilizopo katika Kanda.
Makusanyo hayo
yameongezeka baada ya kusambaza hati za madai kwa wadaiwa sugu wa kodi ya pango
la ardhi 51 na kuwafikisha mahakamani. Jumla ya Tsh. 1.2 bilioni imekusanywa
kutoka kwa baadhi ya wadaiwa waliofikishwa mahakani na hivyo kufanya makusanyo
hayo kuongezeka.
Pamoja na hatua hizo za
kuwafikisha wadaiwa sugu mahakamani, ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi nyanda
za juu Kusini imetoa rai kwa wadaiwa wote wa kodi ya pango la ardhi kulipa kodi
kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni.
Kodi ya pango la ardhi
hulipwa kila mwaka kuanzia tarehe 01 Julai hadi tarehe 31 Disemba bila tozo.
Endapo kodi hii haitalipwa kwa wakati, kuanzia tarehe 01 Januari italipwa na
tozo ya asilimia moja (1%) ya kodi husika.
Ni vyema wananchi
wakatambua kwamba, Ardhi yote ya Tanzani ni mali ya Umma na msimamizi ni Raisi
wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania. Hivyo, wananchi ni wapangaji wa ardhi na
wanamiliki kwa mkataba wa miaka 33, 66 au 99 ambao ni Hati miliki ya kiwanja husika.
Kipengele cha kwanza
kabisa cha Hati miliki kimeeleza masharti mbalimbali ya umiliki wa ardhi. Mojawapo
ni kulipa kodi ya pango la ardhi kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu. Kodi
hiyo italipwa kulingana na ukubwa wa kiwanja, matumizi yake pamoja na eneo
kiwanja kilipo.
Kutokulipa kodi ya
Pango la Ardhi ni kosa kisheria. Adhabu inayoweza kuchukuliwa kwa kosa hili
pamoja na kupelekwa mahakamani ni kukamatiwa mali au kufutiwa umiliki. Kodi ya
pango la ardhi ni kwa kwa maendeleo ya taifa letu hivyo, hatuna budi kulipa kwa
wakati ili kuepuka usumbufu.

0 Comments