Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bi.Susan Mlawi akitoa ufafanuzi wa masuala ya kiutumishi kwa viongozi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Mbeya pamoja na viongozi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya na Halmashauri ya Wilaya ya mbeya alipofanya ziara ofisini hapo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kwa mwaka 2017
Mkurugenzi Idara ya Uchambuzi na Ushauri kazi Ofisi ya Rais-UTUMISHI Bw.Micky Kiliba,akitoa ufafanuzi kuhusu ujazaji wa fomu za OPRAS zinazopima utendaji kazi wa Mtumishi wa Umma.
Watendaji katika Mamlaka za Serikali za Mitaa wametakiwa kuhakikisha
suala la taarifa chafu za Watumishi linamalizika haraka iwezekanavyo ili
kurahisisha zoezi la uhakiki wa taarifa za kiutumishi kwenye Mfumo Shirikishi
wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara (HCMIS).
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora Bi.Susan Mlawi alisema hayo katika kikao kazi na watendaji wa
Halmashauri ya Jiji la Mbeya na
Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Wiki
ya Utumishi wa Umma kwa mwaka 2017.
“Sitegemei tena kusikia Halmashauri au Mkoa una taarifa chafu za
watumishi wake, hivyo nawaagiza Maafisa Utumishi na Watendaji katika Mikoa na
Halmashauri mhakikishe suala hili linafikia ukingoni” Bi.Susan alisema.
Aliongeza kuwa suala la uhakiki wa taarifa chafu za watumishi
limefanyika kwa muda mrefu sasa, hivyo halitakiwi kuzungumzwa tena katika
kipindi hiki.
Naye Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu ,Ofisi
ya Rais-UTUMISHI Bw.Leornad Mchau
aliongeza kuwa taarifa chafu za watumishi ni eneo ambalo linasabisha uwepo wa
watumishi hewa.
“Unakuta taarifa za mtumishi hazionyeshi cheo chake wala hazionyeshi
tarehe yake ya kuzaliwa, hili ni tatizo” Bw. Mchau alisema.
Alifafanua kuwa jitihada za kufanyia kazi taarifa chafu za Watumishi
wa Umma zilianza toka mwaka 2010 ambapo Maafisa Utumishi katika Mamlaka za
Serikali za Mitaa wanaohusika na Mfumo Shirikishi wa Taarifa za Kiutumishi na
Mishahara (HCMIS) baadhi yao
waliwajibishwa kwa kuzembea kufanyia kazi taarifa chafu.
Bw.Mchau alisisitiza kuwa Watumishi wa Umma watakaoonekana taarifa zao
hazieleweke kwenye Mfumo Shirikishi wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara
(HCMIS) watafutwa mara moja.
“Mwezi uliopita tuliondoa watumishi kadhaa ambao taarifa zao
hazieleweki kwenye mfumo wa HCMIS na hakuna mtumishi hata mmoja aliyekuja
kulalamika kuondolewa kwenye mfumo.” Bw. Mchau alisema na kuongeza kuwa kuanzia
mwezi Julai 2017 takriban watumishi 16,000 ambao vyeo vyao havijulikani kwenye
mfumo wa HCMIS wataondolewa.
Bw. Mchau alitoa rai kwa Watumishi wa Umma kuhakiki taarifa zao za
kiutumishi kwa kujisajili katika Tovuti ya Watumishi (Watumishi Portal) na
kuangalia kama zipo sahihi kabla hawajaondolewa kwenye mfumo na pia kila
mtumishi ahakikishe anajiandikisha na kupata kitambulisho cha Taifa ili
utambulisho wake wa Taifa ujulikane.
“Mtumishi wa Umma ambaye hana kitambulisho cha Taifa au namba ya
utambulisho wa Taifa tutamhesabu kuwa ni mtumishi hewa na yeyote ambaye ana
mshahara usioeleweka ifikapo Julai 15, 2017 mfumo wa HCMIS utamtoa kimfumo (Automatically).
Hatima ya Watumishi walioghushi vyeti
Akitoa ufafanuzi kuhusu hatma ya Watumishi wa Umma walioghushi vyeti
Naibu Katibu Mkuu,Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
Bi.Susan Mlawi alisema kuwa inasubiriwa taarifa kutoka Baraza la Mitihani Tanzania
ambayo itakuwa imejumuisha matokeo ya rufaa za Watumishi walio kwenye orodha ya
vyeti vya kughushi.
Katika hatua nyingine Bi. Susan
aliainisha kuwa Ofisi ya Rais-UTUMISHI imeandaa mapendekezo ya namna ya
kushughulikia suala la watumishi walioghushi vyeti.
Upungufu wa Watumishi
Naibu Katibu Mkuu,Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora Bi.Susan Mlawi alisema Serikali inaangalia namna ya kukabiliana na
changamoto ya upungufu wa watumishi katika baadhi ya Halmashauri na Mikoa.
“Zipo baadhi ya ofisi ambazo zina watumishi wa ziada na nyingine zina
watumishi wachache kwa maana hiyo ofisi yenye watumishi wa ziada itatakiwa
iwahamishie kwenye ofisi nyingine yenye upungufu wa watumishi”Bi. Susan
alisema.
Mfumo wa Wazi wa Tathmini ya Utendaji Kazi
(OPRAS)
Mkurugenzi Idara ya Uchambuzi na Ushauri Kazi Ofisi ya Rais-UTUMISHI
Bw.Micky Kiliba alisema UTUMISHI inaangalia namna ya kufanyia marekebisho fomu
za OPRAS za walimu, makatibu muhtasi na madereva ili kuhakikisha kuwa
zinaendana na mipango mikakati yao ya kazi kwa mwaka mzima.
Wiki ya Utumishi wa Umma inatarajia kufikia kilele tarehe 23 Juni,
ambapo nchi wanachama wa Umoja wa Afrika huitumia kutambua mchango wa watumishi
katika utendaji kazi, na kuhudumia jamii. Ofisi ya Rais-UTUMISHI mwaka huu 2017
imepanga kuadhimisha kwa kukutana na Watendaji katika Mamlaka za Serikali za
Mitaa kujua changamoto wanazokutana nazo katika kutatua kero za Watumishi wa
Umma.


0 Comments