Baadhi ya waratibu elimu kata na waganga wafawidhi wa vituo vya afya kutoka Manispaa ya Lindi na halmashauri ya wilaya ya Lindi wakimsikiliza Mkurugenzi wa Manispaa ya Lindi bwana Jomaary Satura wakati alipoyafungua mafunzo hayo katika mkoa wa Lindi.
Baadhi ya waratibu elimu kata na waganga wafawidhi wa vituo vya afya kutoka Manispaa ya Lindi na halmashauri ya wilaya ya Lindi wakimsikiliza Mkurugenzi wa Manispaa ya Lindi bwana Jomaary Satura wakati alipoyafungua mafunzo hayo katika mkoa wa Lindi
Baadhi ya watoa mada ambao ni wahasibu kutoka Manispaa ya Lindi na halmashauri ya wilaya ya Lindi wakimsikiliza Mkurugenzi wa Manispaa ya Lindi bwana Jomaary Satura wakati alipoyafungua mafunzo hayo katika mkoa wa Lindi.
Na Mathew Kwembe, Lindi
Jumla ya watendaji wa Mamlaka za
Serikali za Mitaa 10,931 kutoka Halmashauri 93 za Mikoa 13 inayotekeleza
Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma (PS3) wamepewa mafunzo
ya uhasibu na utoaji wa taarifa za fedha katika awamu ya kwanza na ya
pili ya mafunzo hayo yaliyofanyika katika mikoa hiyo.
Mkuu wa Mifumo ya Mawasiliano PS3
bwana Desderi Wengaa ameyasema hayo jana mjini Lindi kabla ya kumalizika
kwa awamu ya pili ya mafunzo hayo ambayo yaliwahusisha waratibu wa
elimu kata na waganga wafawidhi wa vituo vya afya kutoka mikoa 13 iliyo
chini ya Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma (PS3).
Bwana Wengaa amefafanua kuwa
katika awamu ya kwanza ya mafunzo ambayo yalitolewa kwa wakufunzi
waliowafundisha watumishi kutoka Mamlaka za Serikali za Mitaa, jumla ya
wakufunzi 2883 walipewa mafunzo hayo kwenye mikoa hiyo.
Akizungumza kabla ya kuhitimishwa
kwa awamu ya pili ya mafunzo hayo yanayoendelea katika mkoa wa Lindi
bwana Wengaa amesema kuwa katika awamu ya pili ya mafunzo jumla ya
watumishi Mamlaka za Serikali za Mitaa 10,048 kutoka Mikoa 13
inayotekeleza Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma (PS3)
walifaidika na mafunzo ya uhasibu na utoaji wa taarifa za fedha.
Ameongeza kuwa mara baada ya
Waratibu wa Elimu kata na Waganga wafawidhi wa vituo vya afya kupewa
mafunzo ya aina hiyo, watumishi hao watapaswa kwenda kuwapa mafunzo kama
hayo kwa wahasibu katika ngazi ya shule na Zahanati.
“Lengo ni kuufanya mfumo wetu
unaojulikana kwa Kiingereza kama Facility Financial Accounting and
Reporting System (FFARS) uanze kutumika ifikapo julai mosi, 2017 kama
Serikali ilivyokusudia,” alisema.
Alisema kuwa mfumo huo umeundwa
kuweza kukidhi changamoto mbalimbali za miundombinu, ikiwemo umeme, na
kutokuwa na upatikanaji wa mtandao kwa baadhi ya vituo vya kutolea
huduma katika halmashauri mbalimbali na hivyo mfumo huo hautakuwa tu
katika muundo wa kielektroniki, lakini pia kutakuwa na muundo wa kujaza
kwenye vitabu.
“Mfumo wa kujaza katika vitabu na
wenyewe umeboreshwa na kuwa rahisi kwa mtumiaji kujaza taarifa sahihi,
na huu utatumika kwa vile vituo ambavyo changamoto ya upatikanaji wa
miundombinu wezeshi katika matumizi ya kielektroniki,” alisema na
kuongeza kuwa mara baada ya kujaza katika vitabu, takwimu hizo
zitaingizwa katika mfumo kwenye ngazi ya halmashauri na vituo kupatiwa
taarifa ya vituo vyao.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa
Manispaa ya Lindi bwana Jomaary Satura aliwataka washiriki wa mafunzo
hayo kuhakikisha kuwa wanatumia fursa hiyo kujipatia ujuzi ambao
watakwenda kuutumia ili kuwezesha malengo ya serikali kufikiwa.
Bwana Satura aliongeza kuwa
watumishi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa hawana budi kujifunza kwa
bidii mafunzo hayo ili waweze kuandaa taarifa sahihi na kufunga mahesabu
yao vizuri.
“Bila kufanya hivyo halmashauri zitaendelea kupata hati chafu na huku watendaji ake wakiitwa mchwa,” alisema.
Mfumo huo wa FFARS unatekelezwa
kwa ushirikiano baina ya Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (OR-TAMISEMI); Wizara ya Fedha na Mipango; Wizara ya Elimu,
Sayansi, Teknolojia na Ufundi; na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto, pamoja na USAID.
Mikoa 13 inayotekeleza Mradi wa
Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma (PS3) ni Mtwara, Lindi, Dodoma,
Iringa, Mbeya, Njombe na Morogoro. Mikoa mingine ni Mara, Mwanza, Rukwa,
Shinyanga, Kigoma, na Kagera.





0 Comments