Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imekataa ombi la Mawakili
wanaomtetea mfanyabiashara Harbinder Singh Seth la kumruhusu mteja wao
kwenda nje ya nchi kutibiwa uvimbe uliopo tumboni na badala yake apatiwe
tiba kwenye hospitali ya Taifa Muhimbili.
Wakili wa kujitegemea, Alex Balomi aliifahamisha Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu jana kuwa Harbinder Singh Sethi anaumwa, hali yake
imeendelea kubadilika na hii ni wiki ya nne sasa hawezi kupata
usingizi.
Wakili Balomi aliiambia mahakama hiyo kuwa Sethi anasumbuliwa na
uvimbe tumboni ambao unahitaji uangalizi wa karibu wa madaktari.
“Kutokana na hali yake kuwa mbaya hii ni wiki ya nne sasa hawezi
kupata usingizi hivyo anahitaji ungalizi wa karibu wa madaktari na
kwamba wamebahatika kupata nyaraka kadhaa kutoka kwa daktari,”Balomi aliifahamisha mahakama.
Balomi aliongeza kuwa hata siku aliyokamatwa alikuwa akienda kwenye matibabu Afrika Kusini.
Mwendesha Mashtaka Mwandamizi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa, Leonard Swai alisema nyaraka ambazo Wakili Balomi anataka
kuziwasilisha mahakamani hapo kuhusiana na Sethi hazijakidhi vigezo vya
kisheria na kwamba alitegemea daktari ambaye anamtibu angefika
mahakamani kueleza hali halisi ya ugonjwa husika.
Kutokana na hoja hizo, Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi alisema
suala la ugonjwa si la kufumbiwa macho, linapaswa kuchukuliwa kwa uzito
na kuelekeza magereza kufanya kila linalowezekana kuhakikisha hali ya
mshtakiwa huyo inabaki katika hali nzuri na inapobidi wawasiliane na
wataalam wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Kesi imeahirishwa hadi Julai 28, 2017 kwa ajili ya kutajwa ili kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika ama la.
Katika kesi hiyo, Sethi na James Rugemalira wanakabiliwa na
mashtaka 12 ya uhujumu uchumi kwa kula njama, kujihusisha na mtandao wa
uhalifu, kughushi, kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia
za udanganyifu, kutakatisha fedha na kusababisha hasara ya Dola 22,
198,544.60 sawa na Sh 309,461,300,158.27.

0 Comments