Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Angellah J. Kairuki (Mb) akizungumza na viongozi na watumishi wa umma wa Halmashauri
ya Manispaa ya Ubungo - Kata ya Ubungo alipofanya ziara ya kikazi katika Kata hiyo ili kupokea maoni, ushauri na
kusikiliza kero za watumishi wa umma jana Jijini Dar es Salaam.
Sehemu
ya watumishi wa umma wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo - Kata ya Ubungo
wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma
na Utawala Bora, Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb) (Hayupo pichani) wakati wa kikao
kazi na watumishi hao kilichofanyika jana Jijini Dar es Salaam.
Afisa
TEHAMA wa Ofisi ya Rais-Utumishi, Bw. Dotto Namkaa akiwasilisha mada kuhusu
namna ya kujisajili katika Tovuti ya Watumishi (Watumishi Portal) wakati wa kikao kazi cha Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Angellah J.
Kairuki (Mb) na watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo -Kata ya Ubungo
kilichofanyika jana Jijini Dar es Salaam.
Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Maji (Water
Institute), Dkt. Shija Kazumba akiwasilisha hoja mbalimbali zinazowahusu
watumishi wa umma kutoka taasisi anayoiongoza wakati wa kikao kazi cha Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Angellah J. Kairuki (Mb) na watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo - Kata
ya Ubungo kilichofanyika jana Jijini Dar es Salaam.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais- Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Angellah J. Kairuki (Mb) akifafanua hoja mbalimbali alizopokea kutoka kwa watumishi wa umma wa Halmashauri ya Manispaa
ya Ubungo - Kata ya Ubungo (hawapo pichani) wakati wa kikao kazi na watumishi
hao jana Jijini Dar es Salaam. Kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Mhe.
Kisare Makori na kushoto kwake ni Meya wa Manispaa ya Ubungo, Mhe. Boniface
Jacob.
....................................
Mamlaka
za ajira katika utumishi wa umma nchini zimeelekezwa kufanya marekebisho ya taarifa
za watumishi wa umma wanaotarajiwa kustaafu ili waweze kupata stahili zao kwa
wakati kama inavyostahili.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe.
Angellah J. Kairuki (Mb) amesema hayo leo katika kikao kazi na Watumishi wa
Umma wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo - Kata ya Ubungo, jijini Dar es
Salaam.
Mhe.
Kairuki amesema wapo watumishi wa umma ambao walipandishwa vyeo lakini muda wao
wa kustaafu umekaribia na bado hawajafanyiwa mabadiliko yoyote katika taarifa
zao.
“Natumia
fursa hii kuwaelekeza waajiri wote katika utumishi wa umma warekebishe taarifa
za watumishi hawa wanaokaribia kustaafu ili waweze kupata haki na stahili zao,”
Mhe. Kairuki amesema serikali inawajali watumishi wa umma na kuongeza wale
ambao tayari wameshastaafu, watafutwe na wajaze fomu maalum za madai kupitia kwa
waajiri wao ili serikali iwalipe stahili zao kadri inavyostahili.
“Nawaagiza
waajiri kupitia kwa Maafisa Utumishi wao, wawatafute ili waweze kujaza fomu
maalumu na kuweza kupata haki zao kwani Serikali ipo kwa ajili ya watu wote
hivyo hakuna haki ya mtumishi wa umma yeyote itakayopotea,” Mhe. Kairuki amesema.
Mhe.
Kairuki amewata watumishi wa umma kutimiza wajibu wao kwa weledi ili kuboresha
utendaji kazi. “Serikali ni mimi na wewe hivyo ni jukumu la kila mmoja wetu kutimiza
wajibu wake ipasavyo ili kujenga uchumi wa nchi yetu”.
Awali,
akimkaribisha Mhe. Kairuki kuzungumza na Watumishi wa Kata ya Ubungo, Mkuu wa
Wilaya ya Ubungo, Mhe. Kisare Makori amempongeza Mhe. Waziri Kairuki kwa
utaratibu anaoufanya wa kukutana na watumishi wa umma kwa kusikiliza maoni
pamoja na changamoto wanazozikabili katika utendaji kazi na kuzifanyia kazi.
“Kinachofanyika
sasa ni jambo la kipekee sana kwa Waziri Kairuki mwenye majukumu mazito kutoka
ofisini kwake na kuja kuzungumza katika kikao kama hiki na watumishi wa umma,
kwa niaba ya viongozi wenzangu wa Wilaya ya Ubungo, nampongeza sana,” Mhe.
Makori amesema.
Mhe.
Makori amewataka watumishi wa umma wa Ubungo kuitendea haki ziara ya Waziri Kairuki
kwa kutekeleza maagizo yote yanayotolewa.
Mhe.
Kairuki yupo katika ziara ya kikazi katika mkoa wa Dar es salaama ambapo leo ni
siku ya saba akiwa katika Kata ya Ubungo kwa kukutana na watumishi wa umma wa
kada zote katika vikao kazi.
Lengo
la kukutana na watumishi wa umma ni kusikiliza malalamiko, ushauri na
changamoto zinazowakabili katika maeneo yao ya kazi ili kuweza kuzifanyia kazi
na kuleta mabadiliko katika Utumishi wa Umma nchini ili kufikia malengo
yaliyopangwa na Serikali.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO
SERIKALINI
OFISI YA RAIS-UTUMISHI
18.07.2017
0 Comments