Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais- Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Angellah J. Kairuki (Mb) akizungumza na viongozi na watumishi wa umma wa Halmashauri
ya Manispaa ya Kinondoni-Kata ya Kawe (hawapo pichani) leo alipofanya ziara ya
kikazi katika Kata hiyo ili kupokea
maoni, ushauri na kusikiliza kero za watumishi wa umma Jijini Dar es Salaam.
Sehemu
ya watumishi wa umma wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni-Kata ya Kawe
wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma
na Utawala Bora, Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb) wakati wa kikao kazi na
watumishi hao kilichofanyika leo Jijini Dar es Salaam.
Mhudumu
wa Afya kutoka Hospitali ya Magomeni Bii. Rukia Mkapa akitoa malalamiko yake
wakati wa ziara ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb) wakati wa kikao kazi na
watumishi wa Kata ya Kawe kilichofanyika leo Jijini Dar es Salaam.
Mwalimu
Paschal Mugayana kutoka shule ya Sekondari ya Njechele akitoa malalamiko yake wakati wa ziara ya
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora, Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb) wakati wa kikao kazi na watumishi wa umma
wa Kata ya Kawe kilichofanyika leo Jijini Dar es Salaam.
..............................................
Ofisi
ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora inaendelea kusanifu
na kuboresha Mfumo wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara (HCIMS) ili uweze
kutumika kutoa taarifa za msingi kwa watumishi
wa umma wengi zaidi kwa lengo la kuleta mabadiliko ya utendaji kazi
katika sekta ya umma nchini.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Angellah J. Kairuki (Mb) amesema hayo leo katika kikao kazi na Watumishi wa
Umma wa Halmashauri ya Manispaa ya
Kinondoni – Kata ya Kawe, jijini Dar es Salaam.
Mhe.
Kairuki amesema Mfumo wa HCIMS awali ulikuwa unapatikana Ofisi ya Rais–Utumishi
pekee, lakini baadae ukakasimishwa kwa Maafisa Utumishi lakini sasa lengo ni
kuwafikia watumishi wa umma waweze kuona taarifa zao ili kupata taarifa sahihi
na za uhakika katika kanzidata. Amesema Tovuti ya Watumishi, Watumishi Portal, imeanzishwa maalum ili
watumishi wa umma wajisajili kupitia tovuti ya Ofisi ya Rais-Utumishi yenye
anuani www.utumishi.go.tz na kuona
taarifa zao za msingi.
Waziri
Kairuki, pamoja na hilo, amesema mfumo wa HCIMS umegatuliwa katika Mamlaka za
Serikali za Mitaa hivi sasa ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa na kufanya
maamuzi kwa haraka zaidi.
“Kwa kuwa mahitaji ya watumishi wa umma ni
mengi hivyo tumeona ni vema tukakasimu Mfumo huu na kwa watumishi wa umma
katika kada nyingine ili kurahisisha utendaji kazi na kuleta mabadiliko” Mhe.
Kairuki amesema.
Waziri
Kairuki ameongeza kuwa tayari mafunzo kuhusu namna ya kutumia mfumo yalikwishatolewa
kwa Maafisa Elimu na Makatibu wa Afya wapatao 633.
“Tumeamua kuanza na sekta hizi kwa sababu ni
sekta zenye watumishi wa umma wengi zaidi ukilinganisha na sekta nyingine lakini
tutaendelea kugatua mfumo wa HCIMS ili ufike katika sehemu nyingi zaidi za
kutolea huduma (Service Delivery Points).”
Mhe. Kairuki ameongeza.
Mhe,
Kairuki yuko katika ziara ya kikazi katika mkoa wa Dar es Salaam, ambapo leo ni
siku yake ya tano aliyoitumia kukutana na Watendaji na watumishi wa umma wa
Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni-Kata ya Kawe.
Lengo
la ziara ni kukutana na watumishi wa umma na kusikiliza malalamiko, ushauri na
changamoto zinazowakabili katika maeneo yao ya kazi ili kuweza kuzifanyia kazi
na kuleta mabadiliko katika Utumishi wa Umma nchini.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO
SERIKALINI
OFISI YA RAIS-UTUMISHI
14.07.2017
0 Comments