Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya
Kikwete (JKCI) Profesa. Mohamed Janabi akipeana mkono na Kiongozi wa Msafara wa
baadhi ya Wabunge kutoka Uganda Mhe. Cecilia Barbara wakati wa ziara yao katika
Taasisi hiyo kwa lengo la kujifunza leo Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya
Kikwete (JKCI) Profesa. Mohamed Janabi akielezea jambo wakati wa ziara ya
Wajumbe wa Kamati ya Huduma za Jamii wa Bunge la Uganda waliotembelea Taasisi
hiyo leo Jijini Dar es Salaam. Wabunge hao wametembelea Taasisi hiyo ili
kujionea namna inavyofanya majukumu yake.
Mwenyekiti wa Kudumu wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Mussa Zungu akizungumza jambo mbele ya Wabunge kutoka
Uganda walipotembelea Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) leo Jijini Dar
es Salaam. Kutoka kushoto ni Kiongozi wa Msafara wa Wabunge kutoka Uganda Mhe.
Cecilia Barbara na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete
(JKCI) Profesa. Mohamed Janabi (katikati).
Baadhi ya Wabunge kutoka Uganda wakifuatilia
Maelezo kuhusu namna Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) inavyofanya kazi
wakati wa ziara yao katika Taasisi hiyo leo Jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya Wabunge kutoka Uganda wakiwa katika
sehemu ya mapokezi ya kuingia Wodi ya Watoto katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya
Kikwete (JKCI) leo Jijini Dar es Salaam.
Msajili wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete
Dkt. Zawadi Edward akielezea namna ambavyo wanawahudumia watoto wagonjwa
wanaolazwa katika Taasisi hiyo wakati wa ziara ya Wabunge kutoka Uganda
waliofika katika Taasisi hiyo kwa lengo la kujifunza.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI)
Profesa. Mohamed Janabi (mwenye tai nyekundu) akiwa katika picha ya pamoja na
baadhi ya Wabunge kutoka Uganda walipotembelea Taasisi ya Moyo ya Jakaya
Kikwete (JKCI) kwa lengo la kujifunza leo Jijini Dar es Salaam.
Picha zote: Frank Shija - MAELEZO
..................................
..................................
Na.Agness Moshi-MAELEZO
Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) imekua mkombozi kwa wagonjwa wa moyo Afrika Mashariki kufuatia
kupungua kwa gharama za matibabu ukilinganisha na ilivyokua hapo awali.
Akizungumza na
waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam,
Mbunge wa jimbo la Dokolo nchini Uganda Bi.Cecilia
Barbara alipotembelea taasisi hiyo ili kuona na kujifunza jinsi Serikali ya Tanzania inavyotoa huduma za
Afya kwa wananchi wake .
Bi.Cecilia amesema
taasisi hii ni msaada mkubwa kwa Afrika Mashariki kwasababu itasaidia
kupunguza idadi ya wagonjwa wa moyo wanaopelekwa nchini India au Afrika Kusini kwa matibabu kama ilivyo awali baadala yake
watatibiwa Tanzania au nchini kwao.
“Tunahitaji
kubadilishana mawazo kama wana Afrika Mashariki, kwasababu kwa kuja hapa
tumegundua tunavifaa na uwezo wa kupunguza gharama za matibabu ya moyo“ Alisema
Bi.Cecilia.
Bi Cecilia amesema kutokana na ubora huduma zinazotolewa na
taasisi hii tangu kuanzishwa kwake serikali ya Uganda imekubali kuja kutembelea Tanzania ili kujifunza na
kuanzisha mradi kama huu.
“Hatukujua kama Tanzania
kuna mradi mkubwa kama huu na unaofanya kazi nzuri lakini kwa kuja tumejua na tunategemea
kuanzisha mradi kama huu japo itatuchukua muda kufikia hatua iliyofikiwa na
Tanzania”aliongeza Bi.Cecilia .
Naye Afisa Mwandamizi Kitengo
cha Utafiti wa Bunge la Uganda Mhe. Jonathan Enamu amesema kuwa amejifunza mengi kwenye ziara hii
na ameona ni jinsi gani gharama za matibabu zimepungua kwa wagonjwa wa moyo. “Nimejifunza
mengi, ikiwemo jinsi ya kupunguza
gharama za matibabu na namna bima za afya zinavyoweza kutumika katika matibabu“
alisema Bw. Enamu.
Naye Mkurugenzi wa Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete Prof. Mohamed Janabi amesema kuwa , wanatoa huduma kwa watu wote
kuanzia daraja la chini na watu kutoka
nchi mbalimbali ikiwemo Uganda,comoro,Yemen na Kenya.
Prof.Janabi amesema kuwa taasisi hiyo
imefanikiwa kutumia shilingi bilioni 1.65 badala ya shilingi bilioni 4.72 ambayo
ni sawa na kupunguza takribani asilimia 65 ya gharama za matibabu ya magonjwa
ya moyo nchini kama wangewapeleka India kwa matibabu
Prof. Janabi alifafanua
kuwa kwa mgonjwa mmoja wa maradhi ya moyo anatibiwa kwa shilingi milioni 35-40 tofauti
na nchini India ambapo mgonjwa mmoja anatumia shilingi milioni 120.
Aidha Profesa Janabi
ameishukuru Serikali kwa kuipa ushirikiano taasisi hiyo kwani kwa mwaka huu wa
fedha Taasisi imepokea asilimia 100 ya bajeti itakayosaidia kuendesha shughuli
zao kwa kiwango cha kuridhisha.
Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma na
Maendeleo ya Jamii na Mbunge
wa ilala Mhe. Azzan Mussa Zungu (MB)
amesema kuwa wamewapeleka wageni hao kwenye taasisi ya moyo ili waweze kujifunza
na kuona ni jinsi gani Tanzania imefanikiwa kupunguza gharama za matibabu kwa
wagonjwa wa moyo
“wameona namna sisi
Tanzania tulivyopunguza gharama kutoka kuwapeleka watu 300 kwa mwaka nje kwa
matibabu ya moyo mpaka sasa watu wanne tu, ambao tunawapeleka si kwa sababu hatuna
uwezo bali ni kwa sababu ya vifaa havijakidhi “ alisema Mhe.Zungu.
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete ilianzishwa rasmi mwaka
2014 inashughulika na utoaji wa matibabu kwa wagonjwa wa moyo, kutoa mafunzo
kwa wanafunzi wa udaktari,ufamasia na uuguzi. Pia taasisi hii inashirikiana na
nchi nyingine duniani kwa kubadilishana maarifa,uzoefu na kufanya mafunzo
mbalimbali.






0 Comments