Mkurugenzi wa Operesheni
wa Kampuni ya Zechy Africa Bw. Ally Nchahaga akifafanua jambo kuhusu tamasha la Chemichemi
Carnival litakalofanyika tarehe 9 na10 Septemba 2017 katika kijiji cha
Makumbusho wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam. Kutoka kulia ni Meneja Masoko wa Kampuni ya Zechy
Africa, Bi. Dorah Raymond na Mratibu wa
tamasha la Chemichemi Carnival Bi. Lena
Kimani.
Mratibu wa tamasha la
Chemichemi Carnival Bi. Lena Kimani akisisitiza juu ya tamasha litakalofanyika
tarehe 9 na 10 mwezi Septemba 2017 katika kijiji cha Makumbusho wakati akizungumza
na waandishi wa habari Jijini Dar es
Salaam leo. Kulia ni Meneja Masoko wa Kampuni ya Zechy Africa, Bi. Dorah
Raymond na Mkurugenzi wa Operesheni wa Kampuni ya Zechy Africa Bw. Ally
Nchahaga (kushoto).
Waandishi wa habari
wakimsikiliza Mratibu wa Tamasha la Chemichemi Carnival Bi. Lena Kimani wakati
akizungumza nao juu ya Tamasha la Chemichemi Carnival katika ukumbi wa Idara ya
Habari - Maelezo.
Picha na Alex John Mtazamo News -Dar es Salaam.
....................................
....................................
Na.
Thobias Robert - MAELEZO
Kampuni ya Zechy
Africa inayojihusisha na masoko imeandaa tamasha kwa ajili ya kusherehekea utamaduni wa Mtanzania linalotarajiwa kufanyika
mapema mwanzoni mwa mwezi wa tisa katika Kijiji cha Makumbusho Kijitonyama.
Hayo yamebainishwa leo
Jijini Dar es Salaam na Mratibu wa tamasha hilo Bi. Lena Kimani alipokuwa
akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu Tamasha hilo linaloitwa Chemichemi
Carnival na kusisitiza kuwa tamasha hilo litafanyika kwa siku mbili kuanzia Septemba
9 -10 mwaka huu.
“Tumeendaa tamasha hili la Chemichemi Carnival
kwa lengo la kuonesha utamaduni halisi wa Mtanzania, wananchi watumie fursa hii
kujitokeza kwa wingi kuja kujionea tamaduni mbalimbali za kitanzania,” alisema Bi.
Lena.
Aidha Bi. Lena aliongeza
kuwa utamaduni wa Mtanzania unazidi kupotea hasa kwa vijana wanaozaliwa na
kukulia Mijini hivyo tamasha hilo litaendeleza na kukuza utamaduni wa Mtanzania
ili vijana wasisahau tamaduni zao.
“Kutokana na utandawazi
na mwenendo wa maisha Watanzania wanaoishi mijini wengi wao hawana ukaribu na
vijiji wanakotoka na hili limewafanya vijana wengi wa sasa kuwa mtazamo hasi
kuhusu utamaduni ,” alieleza Bi. Lena.
Tamasha hilo linatarajia
kuonesha mambo mbalimbali ya kiutamaduni likijumuisha, maonesho ya mavazi,
vyakula, burudani kutoka ngoma za asili, wadau mbalimbali wa sanaa pamoja na
mashindano ya mitindo kwa washiriki.
Kwa upande wake Meneja
Masoko wa Kampuni hiyo Bi. Dorah Raymond amesema kuwa Tamasha hilo linatarajia
kuwakutanisha wadau kutoka ndani na nje ya nchi ili kukuza fursa ya kiuchumi
kupitia sanaa na tamaduni zitakazooneshwa katika tamasha hilo.
Alisema kuwa tamasha la hilo linaleta watu
wote pamoja katika kusherehekea tamaduni zetu lakini pia fursa za kukua
kiuchumi kupitia sanaa.
Naye Mkurugenzi wa
Kampuni ya Zechy Africa Bw. Ally Nchahaga ameongeza kuwa kufuatia umuhimu wa
kukuza utamaduni wa mtanzania tamasha la Chemichemi Carnival litakuwa
likifanyika mara mbili kwa mwaka.
“Tamasha hilo ambalo
litafayika kwa mara ya kwanza hapa nchini, halitakuwa na kiingilio, badala yake
wananchi wahamasishwa kujitokeza kwa wingi wakiwa wamevalia mavazi ya kitamaduni
ili kuongeza hamasa,” aliongeza Ally Nchahaga
Kampuni ya Zechy
Africa imeandaa Tamasha hilo ikiwa ni mara ya kwanza kwa tamasha hilo kufanyika
hapa nchini ambapo kupitia kampuni hiyo litakuwa likifanyika kila baada ya
miezi sita ili kutoa fursa kwa tamaduni mbalimbali kushiriki katika tamasha
hilo.
0 Comments