Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison
Mwakyembe (katikati) akionyesha Jarida la Mpango Mkakati la Shirikisho
la Masumbwi Tanzania (BFT) mara baada ya kufanya nao mazungumzo katika
Ofisi za Wizara 01 Agosti, 2017 Jijini Dar es Salaam.
(PICHA NA BENEDICT LIWENGA-WHUSM)
...................
Na Benedict
Liwenga-WHUSM.
Waziri wa Habari Utamaduni Sanaana Michezo, Mhe. Dkt.
Harrison Mwakyembe amewaahidi Shirikisho la Masumbwi Tanzania (BFT) kuwatatulia
kero ya eneo la kufanyia mafunzo pamoja na ofisi ambalo limekuwa likiwakabili
kwa muda mrefu zikiwemo na changamoto nyingine za Shirikisho hilo.
Mhe. Mwakyembe ameyasema hayo leo Jijini Dar es Salaam wakati
alipokutana na kufanya mazungumzo na baadhi ya Viongozi na wajumbe mbalimbali
wa shirikisho hilo ikiwa ni sehemu ya kutambua utendaji kazi wao na changamoto
zinazowakabili ili ziweze kutatuliwa.
Dkt. Mwakyembe amesema kwamba, kutokana na tatizo la ukosefu
wa eneo rasmi la ofisi na sehemu ya kufanyia mafunzo, yeye atawasiliana na
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi ili kuona
namna gani wanaweza kupata eneo kwa ajili ya kulisaidia shirikisho hilo kwa
ajili ya kujenga ofisi na eneo la kufanyia mazoezi.
Sambamba na hilo, ameupongeza uongozi wa shirikisho hilo kwa
kazi wanazozifanya na kuwataka wazidi kushirikiana na Baraza la Michezo la
Taifa (BMT) hususani katika kupeana taarifa zinazohusu maendeleo ya mchezo wa
masumbwi nchini.
“BFT jitahidini muwe na ushirikiano wa karibu na Baraza la
Michezo la Taifa (BMT) na msifanye mambo yenu kimya kimya, muwasiliane kwa
karibu na BMT kwani hii itasaidia Wizara kushughulikia kero zenu mbalimbali
kuliko mkichelewa kutoa taarifa mapema”, alisema Dkt. Mwakyembe.
Aidha, amewahakikishia kuwa, yupo tayari kutafuta wafadhili
ndani na nje ya nchi ili waweze kulisaidia shirikisho hilo kutatua kero za
uhaba wa vifaa, rasilimali fedha pamoja na ukosefu wa mafunzo kwa makocha.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Yusuph
Singo amelitaka shirikisho hilo kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu za Serikali
ikiwemo kujenga tabia ya ulipaji kodi, kuwaelimisha Wanamasumbwi kuachana na
tabia chafu wanapokuwa michezoni pamoja na kuachana na kujihusisha na madawa ya
kulevya.
Kwa upande wao Viongozi wanaounda shirikisho hilo pamoja na
wajumbe kwa pamoja wamemuahidi Waziri Mwakyembe na Wizara kwa ujumla kuzingatia
masuala mbalimbali ikiwemo kuboresha suala la mawasiliano kati ya Shirikisho na
Wizara, kufuatilia suala la mikataba mbalimbali na uwajibikaji yakinifu.

0 Comments