- Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Sara Msafiri Ally ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Hanang akizindua jengo la tawi la NMB lililopo katika mji mdogo wa Haydom.
- Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Sara Msafiri Ally ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Hanang (wa tatu kulia) kikata utepe kuashiria uzindua wa jengo la tawi la NMB lililopo katika mji mdogo wa Haydom. Wa pili kulia ni Meneja wa NMB Kanda ya Kati, Straton Chilongola.
KILIO cha
wakazi wa jimbo la Haydom wilaya ya Mbulu mkoani Manyara cha kukosa
huduma za kibenki toka Tanzania ipate uhuru,kimepata ufumbuzi wa kudumu
baada ya NMB benki, kufungua tawi katika mji mdogo wa Haydom. Kwa mujibu
wa mbunge wa jimbo la Haydom, Flatei Massay, katika kipindi chote
hicho, wananchi wa jimbo hilo wamekuwa wakilazimika kufuata huduma za
kibenki Mbulu mjini, umbali wa zaidi ya kilometa 90. Mbunge Massy
alisema kitendo cha kufuata huduma za kibenki umbali mrefu kiasi hicho,
kumekuwa na madhara mengi na makubwa, ikiwemo gharama kubwa ya usafiri
na pia usalama wa fedha.
“Umbali
huo umesababisha wakulima, wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla,
kutunza fedha zao majumbani. Miaka ya nyuma majambazi yalitumia bomu
kubomoa kasiri (sefu) la kutunzia fedha mali ya hospitali ya rufaa ya
misioni Haydom na yalifanikiwa kuiba fedha, Pia fedha nyingi ziliungua
kwa moto wa bomu”, alisema na kuongeza;
“Zipo
hisia kwamba majambazi hayo yalihisi hospitali hiyo haipeleki fedha
benki kwa wakati kutokana na umbali mrefu benki ilipo, kwa hali hiyo
yalitarajia kupata fedha za kutosha”.
Mbunge
huyo alisema kufunguliwa kwa benki hiyo yenye mashine mbili za kutolea
fedha, wananchi na wafanyabiashara, wanapaswa kuitumia kikamilifu, ili
kupanua kilimo na biashara zao.
Kwa
upande wake mgeni rasmi katika ufunguzi huo, kaimu mkuu wa mkoa wa
Manyara, Sara Msafiri Ally, ameihimiza benki ya NMB kuongeza juhudi
zaidi katika kuendelea kutoa mikopo na huduma zingine kwa wakazi wa
vitongoji vyote mkoani Manyara. Alisema serikali ya awamu ya tano
imeweka mikakati mizuri ya kupunguza umaskini, hivyo mikopo inayotolewa
na mabenki ikiwemo NMB, itasaidia kuendeleza kukuza uchumi na kuongeza
ajira.
Ameongeza
kwa kuwahimiza wananchi wa Haydom, kuchangamkia uwepo wa benki ya NMB,
ili kutumia huduma zao za kibenki kupata maendeleo yao binafsi, wilaya
ya Mbulu na mkoa wa Manyara kwa ujumla.
“Serikali
inawapongeza NMB kwa kutambua umuhimu wa kusaidia jamii. Ni ulweli
usiofichika kuwa faida mnayopata katika huduma zenu za kibenki,
inatokana na wananchi. Hivyo kusaidia jamii ni njia nzuri ya kurudisha
shukrani kwa waliosaidia mkapata faida”, alifafanua Sara.
Awali
meneja wa NMB kanda ya kati, Straton Chilongola, alisema NMB tawi la
Haydom, litahudumia vijiji na viitongoji vya Maghani, Labai, Maritadu,
Endamilayi, Getanyamba na Dongobeshi. Aidha, alisema benki hiyo
imeendelea kubuni bidhaa mbalimbali na zenye kuzingatia mahitaji halisi
ya soko kwa wakati husika.
“Moja
ya bidhaa hizo, ni kampeni ya ‘FANIKIWA’ akaunti ambayo ni mahususi
kabisa kwa wajasiriamali wadogo wadogo. Wajasiriamali hao ni pamoja na
baba/mama lishe, wauza chipis, wenye maduka ya biashara yakiwemo ya
nguo”, alifafanua Chilongola.
Akifafanua
zaidi,alisema akaunti hiyo inampa fursa mteja kupata mkopo wa shilingi
laki tano hadi shilingi 30 milioni. Pia meneja huyo, alisema wanayo
akaunti nyingine ya ‘Wajibu’ ambayo ni mahususi kwa ajili ya watoto
wenye umri wa miaka 0-18.
“Kwa
upande wa teknolojia, tuna akaunti ya ‘Chap Chap’. Akaunti hii mteja
anaweza kufungua akaunti kwa muda mfupi na papo hapo kupata kadi yake ya
ATM, na kuanza kufanya miamala wo wote”, alisema Chilongola.
Benki
ya NMB, ina matawi zaidi ya 200 na mashine za kutolea fedha zaidi ya
700 nchi nzima.Ina wateja zaidi ya milioni mbili jambo linaloifanya kuwa
benki pekee nchini yenye hazina ya wateja wengi kuliko benki zingine
zilizopo nchini.
Burudani zikiendelea.
- Meneja wa NMB kanda ya kati, Straton Chilongola, akitoa taarifa yake kwenye hafla ya uzinduzi wa tawi la NMB Haydom mkoani Manyara. Hafla hiyo imefanyika katika mji mdogo wa Haydom.
- Baadhi ya wakazi wa mji mdogo wa Haydom,waliohudhuria uzinduzi wa tawi la NMB katika mji mdogo wa Haydom wilaya ya Mbulu mkoani Manyara juzi.
- Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Sara Msafiri Ally ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Hanang akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa tawi la NMB tawi la Haydom wilaya ya Mbulu uliofanyika juzi katika mji mdogo wa Haydom.Wa kwanza kushoto (waliokaa) ni meneja NMB kanda ya kati, Straton Chilongola na mbunge wa jimbo la Haydom, Flatei Massy.
0 Comments