Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Ayoub Mohamed Mahmoud akimtunuku cheti Meneja wa kampuni
ya Bima Jubilee Zanzibar Abdulrauf Suleiman kwa kuthamini mchango wake wa
kampeni ya mimi na wewe katika hafla iliyofanyika skuli ya msingi Jang’ombe mjini
Zanzibar.
Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Ayoub Mohamed Mahmoud akikata utepe kuashiria
uzinduzi wa madarasa sita yaliyofanyiwa ukarabati na kampuni ya Jubilee katika
skuli ya Jang’ombe ‘B’. Wa kwanza kushoto ni Kamishna wa mamlaka ya usimamizi wa Bima Zanzibar Mohammed Ameir,
akifuatiwa na Meneja wa Bima Jubilee Zanzibar Abdulrauf Suleiman pamoja na Mwenyekiti
wa kamati ya skuli ya Jang’ombe ‘B’ Taifani Vuai Makame.
Meneja wa Kampuni ya Bima Jubilee Zanzibar Abdulrauf Suleiman (katikati) katika
picha maalum na Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Ayoub Mohamed Mahmoud pamoja na
Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Jang’ombe ‘B’ Bi. Salila Adam Sadik.
Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Ayoub Mohamed Mahmoud akikagua madarasa ya skuli
ya msingi Jang’ombe ‘B’ yaliyofanyiwa ukarabati na kampuni ya Bima Jubilee
ikiwa ni sherehe ya kutimiza miaka 80 tokea kuanzishwa. Kulia, ni Mwalim Mkuu
wa skuli hiyo Bi. Salila Adam Sadik.
................
Na Miza Kona-MAELEZO
ZANZIBAR
Mkuu wa Mkoa
Mjini magharibi Ayoub Mohamed Mahmoud, ameitaka
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuweka mpango maalum wa kuyafanyia
matengenezo madarasa na madawati pale yanapoharika ili kuepusha hasara.
Ameyasema
hayo huko Skuli ya Msingi Jang’ombe katika hafla ya Uzinduzi wa Madarasa sita yaliyofanyiwa
matengenezo na Kampuni ya Bima ya Jubilee katika kusheherekea miaka 80 tangu
kuanzishwa kwake.
Alisema
mpango huo mbadala utasaidia kupunguza gharama za matengenezo na kuweka majengo
katika mazingira mazuri yatayomwezesha mwanafunzi kusoma katika hali ya
kuridhisha.
Alisema kuwepo
utaratibu wa kuwatoza fidia kwa mwanafunzi au raia yeyote atakaharibu kitu ili
kuweza kudhibiti majengo na vifaa vya skuli na kuiepushia serikali hasara ya
kuyafanyia matengenezo kwa gharama kubwa.
Alieleza
kuwa serikali inachukua jitihada ili kuhakikisha skuli zote zake zote zinapatiwa
madawati ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.
“Tatizo la
madawati katika skuli litafikia ukomo wake mwishoni mwa mwaka huu,”
alifahamisha Mhe. Ayoub.
Mkuu
huyo wa
Mkoa amewaomba wazazi na walezi kujiunga na bima ya elimu kwa ajili ya
watoto wao ili kuwekeza katika elimu na kuwajengea mazingira mazuri
ya maisha yao ya baadae.
Aidha alieleza
kuwa kuna changamoto nyingi katika jamii hasa kwenye sekta ya elimu na afya,
hivyo jamii inatakiwa kushirikiana ili kuzipatia ufumbuzi wa pamoja kasoro
zinazojitokeza.
Ayoub pia ameipongeza
kampuni ya Bima ya Jubilee kwa mchango wake huo wa kiunga mkono serikali katika
sekta ya elimu na kuwataka wadau wengine kutoa michango yao katika huduma za
kijamii ili kuleta maendeleo nchini.
Alikabidhi
cheti kampuni hiyo kwa kuwa mdau mkuu wa kutoa mchango katika huduma za jamii
na kuunga mkono kampeni ya Mimi na Wewe.
Akisoma
risala, Meneja wa kampuni ya Bima Jubilee Zanzibar Abdulrauf Suleiman alisema kampuni
yake imejitolea kukarabati madarasa sita katika sehemu zilizobomoka, sakafu
pamoja na kuta, kuweka madirisha, milango na kupaka rangi ndani na nje ili kuwaondoshea watoto kero zinazowakabili na
kujali afya zao wakati wa masomo.
Aidha
ameitaka jamii kuzitunza mali za serikali kwa kuzingatia kwamba skuli ni mali ya jamii hivyo ni wajibu kuzienzi na
kuzilinda ili ziweze kunufaisha vizazi vya sasa na vijavyo.
Mapema
akimkaribisha mgeni rasmi, Mwenyekiti wa Kamati ya skuli ya Jang’ombe Taifani
Vuai Makame, alisema tatizo kubwa la skuli hiyo ni kuvuja kwa paa lake wakati
wa mvua, hali inayofanya wanafunzi wasiweze kuendelea na masomo.




0 Comments