Mwenyekiti wa
Kamati ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Prof. Norman Sigala King (katikati),
akiongoza kikao cha Kamati yake na Shirika la Posta Tanzania (TPC),
kilichofanyika mjini Dodoma. Kulia ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
Eng. Edwin Ngonyani na kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Moshi
S. Kakoso.
Naibu Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng.
Edwin Ngonyani, akifafanua jambo kwa Kamati ya Bunge ya Miundombinu katika kikao chao na Shirika la Posta
Tanzania (TPC), kilichofanyika mjini Dodoma. Kulia ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo
Mhe. Prof. Norman Sigala King na kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo,
Sekta ya Mawasiliano Eng. Angelina Madete.
Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Posta Tanzania
(TPC), Luteni Kanali mstaafu Haruni Kondo, akitoa taarifa ya Shirika hilo
kwenye kikao chao na Kamati ya Bunge ya Miundombinu kilichofanyika mjini
Dodoma. Kulia kwake ni mjumbe wa Kamati hiyo Mhe. Anna Lupembe
Mjumbe wa
Kamati ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Anna Lupembe (wa kwanza kulia), akichangia
hoja katika kikao cha Kamati hiyo na Shirika la Posta Tanzania (TPC),
kilichofanyika mjini Dodoma. Kushoto kwake anayesikiliza ni Mwenyekiti wa Bodi
ya Shirika hilo Luteni Kanali mstaafu Haruni Kondo.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
..................
Shirika la Posta
Tanzania (TPC), limefanikiwa kukusanya madeni ya muda mrefu kutoka kwa taasisi
za Serikali, mashirika ya umma na sekta binafsi kiasi cha shilingi bilioni 7.6.
Hayo yameelezwa na Naibu
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani katika kikao cha
Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Miundombinu kuhusu utekelezaji wa majukumu ya
Shirika hilo kilichofanyika mjini Dodoma ambapo amesema makusanyo hayo ni kati
ya jumla ya shilingi bilioni 12 ambazo Shirika hilo linadai wateja wake kuanzia
mwaka 2011 hadi mwezi Juni mwaka huu.
"Hakikisheni
mnamalizia makusanyo ya deni lililobaki, kwani Shirika linahitaji kuendelea na
kupata faida kupitia makusanyo haya”, amesema Naibu Waziri Ngonyani.
Naye Mwenyekiti wa
Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Miundombinu Mhe. Prof. Norman Sigala King ameiomba
Serikali kuliondoa Shirika hilo kwenye orodha ya mashirika yanayotaka
kubinafsishwa.
Ameongeza kuwa
Serikali ikitekeleza jambo hilo, italiwezesha Shirika hilo kujiendesha
kibiashara, kuzalisha faida na kukabiliana na changamoto za ushindani kwenye
soko.
Aidha, amelitaka
Shirika hilo kuwa wabunifu katika utoaji wa huduma zake kwa wananchi kwa
kutumia Teknolojia za kisasa zaidi badala ya kutumia mifumo ya kizamani.
Kwa upande wake
Mwenyekiti wa Bodi wa Shirika hilo Luteni Kanali mstaafu Bw. Haruni Kondo,
ameiomba Kamati hiyo kuendelea kushirikiana na Shirika hilo na kulisaidia ili
liweze kutoa huduma kwa wananchi kwa wakati na kwa ufanisi.
Taasisi za Serikali na
Mashirika ya Umma yanaendelea na utekelezaji wa agizo la Rais wa Awamu ya Tano
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ya kuhakikisha
kuwa yanajiendesha kwa faida, kuongeza ukusanyaji wa mapato na kudai madeni ya muda
mrefu ili fedha hizo ziweze kutumika kuwahudumia wananchi katika nyanja mbalimbali
kama vile za elimu, afya na ujenzi wa miundombinu.
0 Comments