Waziri
wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe.
Dkt. Harrison Mwakyembe akiongea na wageni waalikwa pamoja na Viongozi mbalimbali waliohudhulia hafla
ya kumuaga balozi wa China nchini Tanzania, Mhe. Lu Youking iliyofanyika katika mgahawa wa Great Wall Jijini
Dar es Salaam.
Balozi wa China nchini Tanzania, Mhe. Lu Youking akiongea na wageni waalikwa pamoja na Viongozi mbalimbali waliohudhulia hafla
ya kuagwa kwake iliyofanyika katika mgahawa wa Great Wall Jijini
Dar es Salaam.
Mwenyekiti
wa Chama cha Ushirikiano wa Urafiki baina ya Tanzania na China, Dkt.
Salim Ahmed Salim (kushoto) akimpongeza Balozi wa China nchini Tanzania,
Mhe. Lu Youking mara baada ya kumalizika kwa hafla ya kumuaga balozi
huyo iliyofanyika katika mgahawa wa Great Wall Jijini Dar es Salaam.
Waziri
wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe.
Dkt. Harrison Mwakyembe(kulia) akimpongeza Balozi wa China nchini
Tanzania, Mhe. Lu Youking wakati alipowasili kwa ajili ya kushiriki
hafla ya kumuaga balozi huyo iliyofanyika katika mgahawa wa Great Wall
Jijini Dar es Salaam.
(PICHA ZOTE NA BENEDICT LIWENGA-WHUSM)
..
Na. Benedict
Liwenga-WHUSM.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt.
Harrison Mwakyembe ametoa pongezi za dhati kwa Balozi wa China nchini Tanzania,
Mhe. Lu Youking kutokana na utendaji kazi wake uliotukuka katika kudumisha
ushirikiano baina ya Tanzania na China hususani katika nyanja za masuala ya
habari, utamaduni, sanaa na michezo.
Pongezi hizo amezitoa hivi karibuni wakati wa hafla ya
kumuaga balozi huyo iliyowakutanisha baadhi ya Viongozi wa Chama cha
Ushirikiano wa Rafiki wa Tanzania na China wakiwemo Waandishi wa habari.
Moja ya mambo makubwa muhimu yaliyofanyika chini wakati wa
kipindi cha Balozi Lu Youking ni tukio la utiaji saini mwezi Machi mwaka huu ambapo
Serikali ya Tanzania na China zilitiliana saini Mkataba wa Ushirikiano wa
Kiutamaduni wa Miaka mitatu ambao utawapa fursa vijana 200 kutoka Tanzania kila
mmoja kwenda China kwa ajili ya kupata mafunzo katika nyanja mbalimbali za
habari, sanaa na utamaduni.
"Balozi Lu Youking umetuachia zawadi kubwa sana sisi
Wanahabari wa Tanzania, sasa hivi mimi na wenzangiu Wizarani tunakamilisha
utaratibu wa utekelezaji wa Mkataba huu ili tuanze kuutekeleza mapema
iwezekenavyo", alisema Dkt. Mwakyembe.
Aliongeza kuwa, Balozi Lu Youking hivi karibuni ameshirikiana
na Balozi wa Tanzania nchini China, Mhe. Balozi Mbelwa Kairuki katika kuhakikisha
kwamba Waandishi wa habari 10 kutoka Tanzania wanaondoka mwezi ujao kuelekea
nchini China kwa ajili ya kubadilishana uzoefu katika masuala ya habari.
Kwa upande wake Balozi Lu Youking alisema kwamba, urafiki
kati ya Tanzania na China umekuwa wa afya na imara zaidi ya nusu karne
akikumbushia kuwa, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere enzi za uhai
wake aliwahi kusema kwamba, Tanzania ina marafiki wengi, lakini China ni zaidi
ndiyo maana Rais wa China, Mhe. Xi Jinping alichagua Tanzania kuwa kituo chake
cha kwanza Afrika wakati wa ziara yake ya kwanza nje ya nchi tangu kuwa mkuu wa
nchi.
Aliongeza kuwa, kila mwaka zaidi ya Wanafunzi 700 kutoka
Tanzania huenda China kwa ajili ya masomo zaidi na kutokana na hilo, matokeo ya
ushirikiano wa China na Tanzania umekuwa wa manufaa katika maeneo yote ya
uchumi wa Tanzania na maendeleo ya jamii na kwa kila maisha ya Mtanzania.
“Uhusiano wa China na Tanzania umetoa mwongozo kwa Ushirikiano
wa Kusini na Kusini yaani South-South Cooperation, hivyo kutokana na maendeleo
ya ushirikiano huu katika uwezo wa uzalishaji kati ya China na Tanzania na mpango
wa Ukanda mmoja njia moja, tunaamini ushirikiano huu utakuwa na matunda zaidi”,
alisema Balozi Youking.
Urafiki baina ya Tanzania na China ulianzishwa na Waasisi
Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti
wa Chama cha Kikomunisti cha China, Bw. Mao Tse-Tung (Mao Zedong) ambapo uhusiano baina wa nchi hizi mbili kwa
sasa umekuwa kwa kasi na kuleta maendeleo baina ya pande zote mbili.




0 Comments