Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Tizeba.
.....
Na Jovina Bujulu-MAELEZO
Hivi karibuni,
Serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Ubora wa Mbolea (TFRA) imeingiza nchini
mbolea yenye uzito wa tani 55,000 kwa mfumo mpya wa ununuzi wa mbolea kwa
pamoja bila kuwepo malipo ya ziada bandarini.
Mfumo huo utasaidia
kupunguza bei na kuhamasisha matumizi ya mbolea kwa wakulima wengi nchini.
Uingizwaji wa mbolea
hiyo ni utekelezaji wa ahadi iliyotolewa na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi,
Dkt. Charles Tizeba alipokuwa akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na
matumizi ya fedha ya wizara hiyo kwa mwaka 2017/18, mjini Dodoma.
DKt. Tizeba alisema kuwa
kuanzia msimu wa 2017/18 Serikali
itaanza kuagiza mbolea kwa mfumo wa pamoja kwa kuanza kuagiza aina mbili za
mbolea ambazo ni mbolea ya kupandia (DAP) na ya kukuzia (UREA), kwa kuwa
ndizo zinatumika sana nchini.
Alitaja sababu za
kutumia mfumo huo kuwa ni pamoja na kuongeza matumizi ya mbolea nchini kwa
kuhakikisha kuwa wadau wote wanapata uhakika wa upatikanaji wa mbolea kwa bei
ya ushindani.
Aidha, mfumo huo
unawawezesha wafanyabiashara wadogo wanapata nafasi ya kuagiza mbolea na
kuimarisha mtandao wa usambazaji hadi ngazi ya mkulima.
Vilevile utaratibu
huo unawawezesha waagizaji kununua mbolea wakati bei ikiwa ndogo na TFRA kufuatilia bei hiyo ili kuepuka mwanya wa
waagizaji kuongeza bei zaidi ya ile iliyonunuliwa kwa bei ndogo.
Kabla ya uamuzi wa Serikali
wa kuagiza mbolea kwa kutumia mfumo huu matumizi ya mbolea hayakuwa ya
kuridhisha kutokana na mbolea kuwa na
bei kubwa jambo ambalo liliwafanya wakulima, hasa wadogo kushindwa kumudu bei
hiyo.
Hivyo baada ya
Serikali kupitia tafiti mbalimbali zilizofanywa na wataalamu waelekezi wa ndani
na nje ya nchi kwa kutumia uzoefu wa taasisi nyingine zinazofanya ununuzi wa
bidhaa kwa pamoja,ikaamua kutumia njia ambayo inawapa wakulima unafuu wa bei
wakati wa kununua mbolea hizo.
Kaimu Mkurugenzi wa
mamlaka hiyo, Lazaro Kitandu amesema kuwa mbolea iliyoletwa nchini imegharimu
zaidi ya shilingi bilioni 10, ambapo wafanyabiashara wa Morocco kupitia kampuni
ya OCPSA wameingiza tani 23,000 za mbolea ya kupandia (DAP) na kampuni ya
Premium Agro Chem ya Tanzania wameingiza tani 32,000 za mbolea ya kukuzia
(UREA).
Mamlaka imehakiki
vyombo vya kupimia mbolea hiyo ili iwe na viwango vinavyokidhi ikiwa ni pamoja
na kusimamia ugawaji bila kuwepo uchakachuaji.
Kitandu amesema kuwa
Serikali imepanga kutoa mbolea hiyo kwa bei nafuu ambapo mamlaka itasimamia
katika kila ngazi ili kusaidia wakulima kufikia malengo ikiwa ni pamoja na
kudhibiti bei toka kule inapotoka na kuhakikisha inauzwa kulingana na bei ya
soko la dunia.
Kuhusu namna mbolea
itakavyowafikia wakulima, Kitandu alisema kuwa mbolea hiyo inatarajiwa
kusambazwa zaidi kwa kutumia usafiri wa treni ili kupunguza gharama za
usafirishaji.
Waziri wa Kilimo,
Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Tizeba alisema kuwa bei elekezi ya mbolea
itatangazwa kupitia vyombo vya habari na kutoa onyo kwa mawakala kujipangia bei
kwa kuuza mbolea nje ya bei elekezi na kwamba ikibainika hatua za kisheria kama
vile kunyang’anywa leseni,kufungiwa, faini au hatua zote kwa pamoja
zitachukuliwa.
Aidha, alisema kuwa
bei hizo zitasimamiwa katika kila ngazi na kuzitaka mamlaka husika kuanzia
Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na vijiji kuhakikisha kuwa bei elekezi
itakayotolewa na Serikali inafuatwa kwa sababu mamlaka ya mbolea pekee haiwezi
kuwa na wasimamizi kila mahali.
“Ununuzi wa mbolea
kwa pamoja utasaidia kudhibiti bei, iwapo iwapo kutajitokeza ongezeko
lisilokuwa na sababu (soko holela), kwa kuwa bei itatangazwa kwa kuzingatia bei
halisi ya mbolea na gharama halisi za usafirishaji ikiwemo kiwango stahiki cha
faida kwa mfanyabiashara” alisema Kitandu.
Utaratibu huu utawainua
wakulima katika uzalishaji wa mazao kwa kuwa watakuwa na uwezo wa kununua
mbolea kwa bei nafuu pia wakati huo huo watakuwa
na uhakika mbolea hiyo ina viwango vinavyokidhi kwa kuwa inaingizwa nchini na
kusambazwa na mamlaka yenye dhamana.
Pamoja na uhakika wa
mbolea yenye bei nafuu na yenye viwango stahiki, wakulima wanatarajiwa kupata
faida ya kupatiwa mafunzo kuhusu matumizi ya mbolea hizo kutoka kwa wataalamu
wa mamlaka ya udhibiti, hivyo kuwa na matumizi sahihi ya mbolea. Ikiwa wakulima
watatumia nafasi hii vizuri, sekta ya kilimo nchini inategemewa kuwa na manufaa
wakulima na taifa kwa ujumla.
Mfumo huo
utawawezesha wafanyabiashara wadogo kukua na kushiriki katika biashara ya
mbolea na kuimarisha mtandao wa usambazaji kuanzia ngazi ya wakulima wakubwa
hadi kwa mkulima mdogo.
Serikali inatarajia
matokeo chanya katika kupunguza bei ya mbolea kwa wakulima itakayosaidia kuongeza
matumizi ya mbolea na uzalishaji wenye tija ambao utachochea na kuimarisha
uchumi wa viwanda.

0 Comments