Random Posts

Mradi wa uboreshaji mfumo wa kielektroniki wa kukatia tiketi vivuko vya magogoni-kigamboni kugharimu bilioni 1.37

 Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Dkt. Mussa Mgwatu (kulia), akimuelekeza jambo Mkuu wa Kivuko cha Magogoni-Kigamboni Mhandisi King’ombe Lukombe, wakati akikagua mashine za mfumo wa kielektroniki wakukatia tiketi zitakazo wawezesha abiria wenye tiketi sahihi kuingia kwenye jumba la abiria kwa ajili ya kusubiria vivuko.
 Mkuu wa Kivuko cha Magogoni- Kigamboni Mhandisi Kingómbe Lukombe (kushoto) akimuelekeza jambo Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) wakati wa ukaguzi wa mradi wa uboreshaji mfumo wa mashine za kielektroniki za kukatia tiketi, katika Kivuko cha Magogoni-Kigamboni.
 Kibanda kipya cha kukatia tiketi kilichojengwa katika kivuko cha Magogoni-Kigamboni upande wa Kigamboni, baada ya kubomolewa kile cha awali, kilichokuwa karibu na jumba la kusubiria abiria, ili kupisha mradi wa uboreshaji wa mfumo wa mashine za kielektroniki za kukatia tiketi na baadae mradi wa upanuzi wa eneo hilo la abiria kusubiria vivuko.
Wafanyakazi wa Kivuko cha Magogoni- Kigamboni wakimsikiliza Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Dkt. Mussa Mgwatu (aliesimama) alipofika kivukoni hapo kukagua mradi wa uboreshaji wa mfumo wa kielektroniki wa kukatia tiketi na kupata fursa ya kuongea nao, baada ya kumaliza mafunzo yao ya utoaji huduma bora kwa Mteja.


Picha na Theresia Mwami – TEMESA
.....

Na Theresia Mwami- TEMESA

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Dkt. Mussa Mgwatu, ametembelea na kukagua mradi wa maboresho ya mfumo wa kielektroniki wa kukatia tiketi unaofanywa katika vivuko vya Magogoni-Kigamboni.

 Mfumo huo utawezesha TEMESA kudhibiti ukusanyaji wa mapato kwa kuhakikisha kuwa kila abiria analipa nauli kamili kabla ya kupatiwa huduma ya kuvuka. Mradi huo umeigharimu TEMESA jumla ya shilingi za kitanzania Bilioni 1.37 na unafanywa na kampuni ya Maxicom Africa ya jijini Dar es Salaam.

 Awamu ya pili ya Mradi itakuwa ni upanuzi wa jumba la kusubiria abiria upande wa Kigamboni, mradi ambao tayari uko kwenye hatua za ununuzi. Mradi wa kuboresha mfumo wa kukatia tiketi unatarajia kukamilika mapema mwezi Oktoba, 2017.

Sambamba na ukaguzi wa mradi huo, Dkt. Mgwatu aliweza pia kuhudhuria mafunzo ya awamu ya pili kuhusu utoaji huduma bora kwa wateja, yaliyokuwa yakitolewa kwa watumishi wa kivuko hicho, na kuwataka watumishi waliohudhuria mafunzo hayo kuzingatia uadilifu katika utendaji kazi wao wa kila siku pamoja na kudumisha ushirikiano miongoni mwao ili kuweza kufikia malengo ambayo TEMESA imejiwekea.

 Watumishi waliokuwa wakipatiwa mafunzo hayo ni pamoja na wakaguzi wa tiketi, mabaharia, mafundi wa vivuko, manahodha wa vivuko pamoja na wakusanya mapato.

Nae Mkuu wa Kivuko cha Magogoni, Mhandisi King’ombe Lukombe aliwaambia waandishi wa habari kuwa mafunzo hayo ya huduma bora kwa mteja (customer care) yanatolewa kwa watumishi wote wa kivuko hicho, wakiwemo walinzi kutoka SUMA JKT wanaotoa huduma ya ulinzi kivukoni hapo, lengo likiwa ni kuboresha zaidi huduma kwa wateja wanaotumia huduma ya vivuko vya Magogoni-Kigamboni na kuondoa malalamiko kwa watumiaji wa huduma hiyo.

Katika eneo la Magogoni, kuna jumla ya vivuko vitatu yaani MV. Magogoni, MV. Kigamboni na MV. KAZI vinavyotoa huduma ya uvushaji wa abiria, magari na mizigo na kwa wastani abiria zaidi ya elfu hamsini huvuka kwa kutumia vivuko hivyo.

Post a Comment

0 Comments