Serikali
imesitisha uchapishaji na usambazaji wa gazeti la kila wiki la RAIA MWEMA kwa muda wa siku 90 (miezi mitatu) kuanzia leo. Agizo hili pia
linahusu toleo la mtandaoni. Adhabu hii inatokana na toleo na. 529 la tarehe 27 Septemba–3 Oktoba, 2017 lililochapisha habari
ya uchambuzi inayosomeka “URAIS UTAMSHINDA
JOHN MAGUFULI.”
Serikali inasisitiza uchambuzi huu ni
maoni yao ya haki (fair comment), hata
hivyo, kwa bahati mbaya, na nia ovu, makala hiyo ilisheheni nukuu za kutunga na
zisizo za kweli zikimsingizia Rais John Pombe Magufuli. Gazeti hili pia
limepata kuonywa huko nyuma kwa makosa mbalimbali.
Nukuu za uongo, kutungwa na zenye nia
mbaya zikidai Rais alipata kusema: “Suruali za zamani msizitupe, mtazihitaji
baadae,” na “Watakaobaki
Dar es Salaam baada ya mwezi wa saba watakuwa wanaume kwelikweli.”
Walipotakiwa kuthibitisha wapi iwe ndani
au nje ya nchi Rais alipata kutoa kauli hizo, wahariri wa RAIA MWEMA waliomba muda, wakapewa. Wakarejea na kuthibitisha kuwa
hawana ushahidi huo, wakakiri kosa na kuomba radhi.
Bado Serikali inaamini kwamba Watanzania
tukiufanyia mzaha upotoshaji wa taarifa na uchochezi katika zama hizi za TEHAMA
amani na utulivu tulivyojivunia kwa miaka mingi vitapotea na kukaribisha maafa
kama ilivyotokea kwingineko duniani.
Serikali,
katika uamuzi huu, uliochukuliwa kwa mujibu wa mamlaka aliyonayo Waziri wa
Habari katika kifungu cha 59 cha Sheria ya Huduma za Habari Na. 12, 2016,
imetoa adhabu ndogo tofauti na ukubwa wa kosa kwa kuwa wahariri wa gazeti hili hawakufanya
tashtiti, wamekiri kosa.
Hata
hivyo katika suala hili tunajifunza tena mambo kadhaa kuhusu changamoto za
kiwango cha weledi wa uandishi wa habari nchini kiasi inatulazimu kutoa
ufafanuzi wa kina kwa faida ya umma na tasnia yenyewe; kwamba uandishi ni
taaluma adhimu na yenye haki na wajibu vinavyopaswa kufuatwa na si kufanyiwa
dhihaka.
Mintaarafu,
mmoja wa wanasiasa waasisi wa Taifa la Marekani wanaotambulika
kuwa waumini wakubwa wa uhuru wa habari, Thomas Jefferson, pamoja na kupigania
sana uhuru huo, katika barua kwenda kwa rafiki yake, James Madison,
wakati wa mjadala wa katiba mpya nchini humo alisisitiza wajibu wa vyombo vya
habari hasa katika “….kutodhalilisha heshima ya mtu au kuharibu
amani na utulivu….”
Kwa
upande wake, John Stuart Mills, Muingereza anayetajwa kuwa “Baba wa Haki ya Kujieleza”
ambaye katika kitabu chake mashuhuri cha “On
Liberty” alitetea sana uhuru wa habari, naye alitambua umuhimu wa
kutekeleza haki kwa kulinda haki za wengine alipoandika:
“The only freedom which
deserves the name is that of pursuing our own good in our own way, so long as
we do not attempt to deprive others of theirs, or impede their efforts to
obtain it.”
Aidha,
Mahatma Gandhi, Baba wa Taifa la India na mpigania uhuru na haki asiyetiliwa
shaka, naye aliamini katika uhuru wa habari lakini alionya vyombo vya habari
lazima vitimize wajibu wao wa kutoandika uongo na uzushi aliposema:
“I venture to suggest that rights that do not directly from duty well
performed are not worth having…. The superficiality, the one-sidedness, the
inaccuracy and often even dishonesty that have crept into modern journalism,
continuously mislead honest men who want to see nothing but justice done.”
Mitazamo
hii ya kifalsafa ya magalacha hawa mashuhuri duniani, imeenziwa na kutiliwa
nguvu katika mikataba na sheria mbalimbali za kimataifa za haki za binadamu
ambazo nchi yetu pia imeiridhia. Kifungu cha 19(3) cha Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kisiasa na Kiraia ambao Tanzania
imeuridhia tangu mwaka 1976, kinasisitiza wajibu huu kikisema:
“3. The exercise of the rights provided for in
paragraph 2 of this article carries
with it special duties and responsibilities. It may therefore be subject to certain restrictions, but
these shall only be such as are provided by law and are necessary: (a) For
respect of the rights or reputations of others; (b) For the protection of national security
or of public order (ordre public), or of public health or morals.
Vyombo
vya habari nchini vinasisitizwa kuendelea kutekeleza wajibu huo. Serikali
itaendelea kulinda uhuru wa habari unaosimama katika misingi iliyoainishwa katika
nukuu hizi za wanafalsafa na sheria za kimataifa. Tunawatakia Bodi ya
Wakurugenzi na wahariri wa gazeti la Raia
Mwema utekelezaji mwema wa agizo hili.


0 Comments