Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (wa kwanza kushoto), akikagua
jenereta linalowezesha mnara wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), katika eneo la
eneo la Gairo Hill,wilayani Gairo, Mkoani Morogoro. Wa kwanza kulia ni Mkuu wa
Wilaya ya Gairo, Bibi. Siriel Mchembe.
Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (kulia), akijadiliana jambo na
Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Bibi. Siriel Mchembe, kabla ya kuzungumza na wananchi
wa kata ya Leshata, wilayani Gairo, Mkoani Morogoro.
Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (wa kwanza kushoto), akimsikiliza
Mtendaji mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa wote (UCSAF), Mhandisi Peter Ulanga (kulia)
alipokagua minara ya simu wilayani Gairo, Mkoani Morogoro.
Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (wa kwanza kushoto), akitoa
maelekezo kwa Wafanyakazi wa Kampuni ya Vodacom Tanzania mara baada ya kufungua
mnara wao katika kijiji cha Chakwale wilayani Gairo, Mkoani Morogoro.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ameyataka makampuni ya simu nchini
kuhakikisha mawasiliano ya simu yanapatikana wakati wote katika ubora
unaotakiwa ili kuwawezesha wananchi kupata huduma inayowiana na thamani ya
fedha wanayolipa.
Akikagua na kuzindua
minara ya simu ya kampuni za TTCL, VODACOM, HALOTEL, na TIGO katika Wilaya ya
Gairo mkoani Morogoro, Profesa Mbarawa amesema Serikali itaendelea kushirikiana
na kampuni za simu kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa wote UCSAF ili katika
kipindi cha miaka mitatu ijayo sehemu zote za Tanzania ziwe zimefikiwa na
huduma ya mawasiliano ya simu ya uhakika.
"Tumieni
mawasiliano ya simu kufanya biashara, kuboresha huduma za jamii kama elimu na
habari ili kukuza ustawi wa maisha yenu", amesema Profesa Mbarawa.
Waziri Prof. Mbarawa amewaonya
wananchi kujiepusha na matumizi mabaya ya mitandao ya simu kwani ipo sheria
kali inayodhibiti matumizi mabaya ya simu.
Amezungumzia umuhimu
wa kampuni za simu kujenga minara katika maeneo mapya na kukarabati minara ya
zamani ili kuwezesha mawasiliano kuwa katika ubora maeneo yote ya nchi.
Amewataka wakazi wa vijiji
vya Letugunya, Leshata na Chakwale kutumia fursa ya upatikanaji wa mawasiliano
kuongeza uzalishaji wa mazao na kuyauza kwa bei nzuri na hivyo kukuza uchumi
wao.
Kwa upande wake
Mtendaji mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa wote Mhandisi Peter Ulanga
amemhakikishia Waziri Profesa Mbarawa kuwa mfuko huo umejipanga kukamilisha miradi yote
kwa wakati na kufanya uhakiki wa takwimu za mawasiliano nchi nzima ili kubaini
maeneo ambayo yana changamoto kubwa ya mawasiliano na kuyatatua.
Mkuu wa Wilaya ya
Gairo Siriel Mchembe amemshukuru Waziri
Mbarawa kwa kuboresha huduma za mawasiliano katika Wilaya hiyo na kumhakikishia
wananchi watailinda miundombinu hiyo ili idumu kwa muda mrefu.
IMETOLEWA
NA KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI WIZARA YA UJENZI,UCHUKUZI NA MAWASILIANO.
No comments:
Post a Comment