Kaimu Meneja wa Mawasiliano toka Mamlaka
ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Semu Mwakyanjala akifafanua jambo kwa waandishi
wa habari (hawapo pichani) wakati akielezea matumizi sahihi na salama ya
mitandao ya kompyuta na intaneti mapema hii leo jijini Dar es Salaam, kulia ni
Afisa Habari wa Idara ya habari (MAELEZO) Bi. Fatma Salum.
Picha na Eliphace Marwa - Maelezo
.....
.....
Na
Fatma Salum – MAELEZO
Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania
(TCRA) imetoa rai kwa Watanzania kuacha kutumia vibaya mitandao ya simu na
intaneti badala yake waitumie kwa ajili ya kurahisisha harakati zao za kujiletea
maendeleo.
Rai hiyo imetolewa leo na Kaimu Meneja Mawasiliano
wa Mamlaka hiyo Bw. Semu Mwakyanjala wakati akizungumza kwenye mkutano na
Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam.
Mwakyanjala alisema kuwa licha ya teknolojia ya mawasiliano
kukua na kuleta faida kwenye jamii yetu, bado kuna changamoto nyingi hivyo ni
wajibu wa kila mmoja kuhakikisha anatumia vizuri mitandao hiyo kwa faida yake
na taifa kwa ujumla.
“Kutokana na mabadiliko ya kila siku ya teknolojia
hasa kwenye sekta ya mawasiliano imesababisha baadhi ya watu kutumia vibaya teknolojia
hiyo kupitia mitandao ya kompyuta na intaneti kufanya uhalifu wa aina
mbalimbali ikiwemo wizi, utapeli, ulaghai na uchochezi,” alieleza Mwakyanjala.
Pia alibainisha kuwa wapo baadhi ya watu wasiokuwa
wazalendo ambao hutumia mitandao hiyo kusambaza taarifa zenye maudhui ya chuki au
uchochezi na kuongeza kuwa Serikali haitasita kuwachukulia hatua kali za
kisheria .
Mwakyanjala alisema kuwa Serikali inaendelea na
jitihada za kusimamia usalama mitandaoni kupitia Kitengo cha Dharura cha
Kuitikia Matukio ya Usalama Kwenye Mitandao (TZ-CERT) ambacho kinafanya kazi ya
kuratibu matukio ya usalama katika mitandao ya kompyuta na intaneti kwa
kushirikiana na vyombo vingine husika vya kikanda na kimataifa.
Akieleza mambo muhimu ya kuzingatia kwa watumiaji wa
huduma za mitandao, aliwataka watumiaji hao kuwa makini na taarifa zao binafsi
wanazoweka kwenye mitandao ya kijamii pamoja na kutumia program za kujikinga na
virusi hatarishi katika kompyuta na simu zao.
“Ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha kwamba
anajilinda na uhalifu wa mitandaoni na kuepuka kumtajia mtu mwingine taarifa
zake binafsi kama vile neno la siri (password) kwani kufanya hivyo
kunawarahisishia watu wenye nia mbaya kufanya uhalifu,” alisisitiza
Mwakyanjala.
Aidha alibainisha kuwa matumizi ya mtandao
yamepanuka sana nchini ambapo kwa sasa
Tanzania kuna watumiaji wa mtandao wanaokadiriwa kufikia milioni 18
ukilinganisha na mwaka 2011 ambapo kulikuwa na watumiaji milioni 5 tu.
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ilianzishwa
mwaka 2003 kwa sheria na. 12 kwa lengo la kusimamia na kudhibiti mawasiliano ya
kielektroniki na huduma za posta.

0 Comments