Mwenyekiti wa Chama chaTanzania Labour
Party (TLP) Augustine Lyatonga Mrema akisisitiza jambo kwa Waandishi wa Habari
(hawapo pichani) wakati akielezea utendaji kazi wa mihimili mitatu ya Bunge, Serikali
na Mahakama mapema hii leo jijini Dar es Salaam, kulia ni Katibu Mkuu wa chama
hicho Bi. Nancy Mrikaria na kushoto ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho
Bi. Rose Mrema.
Picha na Eliphace Marwa - Maelezo
...
...
Na.
Thobias Robert- MAELEZO
Mwenyekiti wa Chama cha
Tanzania Labour Party (TLP), Augusto Lyatonga Mrema ameeleza kuwa mihimili mitatu
ambayo ni Serikali, Bunge pamoja na Mahakama ipo huru katika utendaji kazi kinyume na inavyodaiwa na baadhi ya wanasiasa na
wanaharakati hapa nchini.
Mrema alieleza hayo leo
jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari juu ya
shutuma mbalimbali ambazo zimekuwa zikitolewa dhidi ya Serikali kuwa imekuwa
ikiingilia mamlaka ya mihimili Bunge na Mahakama.
“Nimeamua kulisema hili
kwa sababu kuna watu wanafikiri kuwa mihimili hii inatumiwa kinyume na katiba
kwa madai haiwezi kutenda haki na kwamba Tanzania hakuna mgawanyiko wa madaraka
jambo ambalo siyo la kweli,” alifafanua Mrema.
Aidha aliongeza kuwa,
mihimili yote mitatu ina watendaji wake na inategemeana kwa mujibu wa katiba
(check and balance). Pia amewaasa wananasiasa kuacha kuwapotosha na
kuwachonganisha Wananchi na Serikali yao kwa kuwaaminisha kuwa hakuna uhuru wa
mihimili hiyo.
“Mtu akisema kuwa
mihimili hii haijitegemei na kwamba Rais ana mamlaka juu ya mihimili hiyo
atakuwa anakosea kwani kila mhimili una watendaji wake hivyo makosa
yanapojitokeza Rais hapaswi kulaumiwa, ndiyo maana nimeona niwaeleze Watanzania kwamba Rais haingilii mihimili hiyo,” ameongeza
Mrema
Mrema alisisitiza uhuru
wa mihimili hiyo kwa kutolea mfano wa kesi ya ‘kubambikiza’ dhidi yake
aliyoshitakiwa na aliyekuwa Mkuu wa Polisi nchini IGP Omary Mahita juu ya kumkashifu
Rais wa Awamu ya Tatu Benjamini Mkapa kupokea mgawo wa rushwa ya Sh. Milioni
900 kesi ambayo haikuwa kweli na aliachiwa huru na mhimili wa mahakama.
“Kesi hiyo Namba CR
2/1997 ya kubambikiziwa ilinidhoofisha sana kisiasa lakini naishukuru mahakama
kwa kusimamia haki na kuniona sina hatia,” alisisitiza Mrema ambaye aliwahi
kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani na Naibu Waziri Mkuu.
Aidha Mrema aliwaomba watanzania
wasidanganywe na wanasiasa juu ya mambo yanayotokea nchini kuhusu Rais na
uendeshaji wa bunge.

0 Comments