Serikali
ya Tanzania imepata heshima kubwa katika mkutano wa 72 wa Baraza Kuu la Umoja
wa Mataifa (UN) unaoendelea jijini New York nchini Marekani kutokana na kuenea
kwa sifa za utendaji wa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Pombe
Magufuli.
Akizungumza
kutoka New York anakomwakilisha Rais, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga amesema Tanzania imekuwa kivutio katika
viunga vya UN kutokana na mtindo wa utendaji unaolenga kuwakomboa na kuwaletea
huduma bora wananchi.
“Nimekutana na wajumbe kutoka nchi za Afrika,
Asia, Ulaya na Marekani na wengi wanasema nchi zao ziko tayari kumualika Rais
Magufuli au viongozi wao wako tayari kuja Tanzania kupata uzoefu jinsi Rais
Magufuli anavyofanya mageuzi makubwa katika kipindi kifupi. Wanamuona ni mtu
jasiri na mwenye upeo mkubwa katika kuwatumikia watu wake.
“Nchi hizi
zinapishana kukutana na ujumbe wa Tanzania. Mpaka sasa, mbali na kuhutubia
kwenye Baraza Kuu la UN, nimeshafanya mikutano ya nchi na nchi au na taasisi mbalimbali
ipatayo 25 na wiki hii natarajia kufikisha mikutano 35,” anasema Waziri
Mahiga.
Aidha
kivutio kingine katika mkutano huo ni udogo wa ujumbe wa Tanzania. Mbali na
Dkt. Mahiga ujumbe wake una maafisa wengine watatu tu kutoka Wizarani kwake wakiungana
na Balozi wa Kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Modest Mero.
Akizungumzia
ukubwa wa ujumbe aliouongoza, Waziri Mahiga anasema hii ni historia nyingine
kwani katika mikutano ya UN, Tanzania imekuwa na ujumbe usiopungua watu 40 na
wakati fulani walipata kufikia wajumbe 100; lakini sasa maafisa wachache wametekeleza
kazi kwa ufanisi.
“Waandishi mbalimbali wa kimataifa walioko
hapa pia wamekuwa wakifuatilia habari za idadi ya wajumbe na sisi pia
walitufuata na kujua mpaka tulipofikia. Wameridhika na jinsi Tanzania inavyoenzi
matumizi makini ya fedha za walipakodi,” aliongeza Waziri Mahiga.
Akihutubia
Baraza Kuu, pamoja na kutoa salama maalum za Rais Magufuli, Waziri Mahiga amefafanua
mageuzi mbalimbali yanayoendelea nchini hasa mapambano dhidi ya rushwa na
kuimarisha uwajibikaji na akasisitiza utayari wa Tanzania kuendelea kushirikiana
na UN.


0 Comments