Mkadiriaji majenzi kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Kitengo maalum cha ushirikishwaji wa wanawake
katika masuala ya barabara, Qs. Judith Aron, akizungumza na wanafunzi wa
kidato cha Tano na Sita wa Shule ya Sekondari Mahiwa iliyopo kata ya
Nyango mkoani Lindi, kuhusu faida za usomaji wa masomo ya Sayansi na Hisabati.
Wanafunzi wa kidato cha Tano na Sita wa Shule ya Sekondari
Mahiwa iliyopo kata ya Nyango mkoani Lindi, wakimsikiliza mhandisi kutoka
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Kitengo maalum cha
ushirikishwaji wa wanawake katika masuala ya barabara, Bi Liberatha Alphonce
(hayupo pichani), wakati akiwasilisha mada ya umuhimu wa masomo ya sayansi na
hisabati kwa Taifa na Dunia kwa ujumla.
Mhandisi kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta
ya Ujenzi), Kitengo maalum cha ushirikishwaji wa wanawake katika masuala ya
barabara, Bi. Liberatha Alphonce, akifafanua jambo kwa wanafunzi wa shule ya
Sekondari Mtama iliyopo mkoani Lindi wakati akitoa mada kuhusu uhamasishaji wa
masomo ya Sayansi na Hisabati kwa wasichana.
Mwanafunzi pekee wa kike wa kidato cha nne anayesoma masomo ya
Sayansi, Saumu Abdallah, akitoa maoni yake kwa
Wahandisi wa kike kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya
Ujenzi), Kitengo maalum cha ushirikishwaji wa wanawake katika masuala ya
barabara kuhusu changamoto zinazokabili shule yao.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Mtama mkoani Lindi, Bi. Asha
Namjupa, akisisitiza jambo kwa Wahandisi wa kike kutoka Wizara ya
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Kitengo maalum cha
ushirikishwaji wa wanawake katika masuala ya barabara kuhusu mipango walionao
katika kuhamasisha wanafunzi wa kike kusoma masomo ya Sayansi na Hisabati.
Wahandisi
wa kike wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), kupitia
Kitengo maalum cha ushirikishwaji wa wanawake katika masuala ya barabara
wamewataka wanafunzi wa kike mkoani Lindi kutokata tamaa na badala yake kutumia
mbinu mbadala za usomaji wa masomo ya Sayansi na Hisabati ili kuweza kufikia
malengo yao.
Akizungumza kwa niaba ya wahandisi hao katika shule ya Sekondari ya Mahiwa kata
ya Nyingo mkoani Lindi, Mhandisi Liberatha Alphonce , amesema kuwa ufaulu
wa masomo hayo utategemea ufanyaji wa maswali na mazoezi ya
kujipima mara kwa mara ambayo yatajenga uelewa na hivyo kupelekea ufaulu mzuri.
"Sayansi
si ngumu kama ambavyo mnadhani, hakikisha unapanga ratiba yako vizuri na
kuzingatia yale unayofundishwa na walimu darasani, kamwe usikate tamaa kwani
ndoto zako zitatimia endapo ukifanya juhudi", amesema Mhandisi Alphonce.
Aidha,
wahandisi hao wamefafanua kuwa sekta hiyo bado ina uhaba wa wataalamu wa kike
hivyo inahitaji wanafunzi kusoma masomo hayo ili kuongeza idadi ya wataalamu
hao na kuweza kufikia uchumi wa viwanda ifikapo 2025.
Kwa
upande wake Mwalimu wa Shule ya Sekondari Mahiwa Bi. Emaculathe Mallya, kwa
niaba ya walimu wenzake ameishauri Serikali kutembelea mara kwa mara shule
mbalimbali nchini ili kuhamasisha usomaji wa masomo ya Sayansi na Hisabati.
Ameongeza
kuwa ipo haja ya Serikali kuandaa vipeperushi vitakavyobainisha dhana na faida
za masomo hayo ili kumsaidia mwanafunzi kupata uelewa wa namna ya kupambana na
soko la ushindani mapema.
Naye,
Fundi Sanifu wa maabara ya shule hiyo, Mwalimu Kili Mbwanji, ameiomba
Serikali kuongeza walimu wa kike wa sayansi shuleni hapo kwani kwa sasa shule
hiyo ina mwalimu mmoja tu wa jinsia hiyo hali inayowakatisha tamaa wanafunzi wa
kike kujiunga na masomo hayo.
Mwanafunzi
Happiness Isack, kutoka shule hiyo ameiomba Serikali kuongeza walimu wa sayansi
na hisabati, vitabu na kuboreshea miundombinu ya maabara ikiwemo vifaa vya
kupimia kemikali.
Ziara
ya wahandisi hao katika shule mbalimbali za Sekondari za mkoa huo inalenga
kuhamasisha usomaji wa masomo ya Sayansi na Hisabati kwa watoto wa kike ambapo
leo shule zaidi ya Tano ikiwemo shule ya Mtama, Mahiwa, Ruangwa, Mbekenyera na
Chinongwe zimeweza kufikiwa na huduma hiyo.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano.





0 Comments