Mwenyekiti wa Kamati
ya Bunge ya Miundombinu Prof. Norman Sigallla King (aliyesimama) akizungumza na
wananchi wa kijiji cha Kizengi (hawapo pichani) kilichopo kata ya Kizengi
wilaya ya Uyui mkoani Tabora baada ya kukagua ufikishaji na upatikanaji wa
huduma za mawasiliano vijijini wakati wa ziara ya Kamati hiyo.
Mtendaji Mkuu wa Mfuko
wa Mawasiliano kwa Wote Eng. Peter Ulanga(aliyesimama mbele) akifafanua jambo
mbele ya Kamati ya Bunge ya Miundombinu wakati wa ziara ya Kamati hiyo ya
kukagua upatikanaji wa huduma za mawasiliano vijijini kwenye kijiji cha
Mayamaya kilichopo Kata ya Zanka wilaya ya Bahi mkoani Dodoma.
Meneja wa Kampuni ya
Simu ya TTCL Mkoa wa Tabora Bwana James Mlaguzi (wa kwanza kulia) akitoa taarifa
kwa wajumbe wa Kamati hiyo wakati wa ziara yao ya kukagua upatikanaji wa huduma
za mawasiliano viijini kwenye kijiji cha Kizengi kilichopo kata ya Kizengi
wilaya ya Uyui mkoani Tabora.
Mjumbe wa Kamati ya
Bunge ya Miundombinu Mhe. Mussa Ntimizi akisalimiana na wananchi wa kijiji cha
Kizengi kilichopo kata ya Kizengi wilaya ya Uyui mkoani Tabora wakati wa ziara
ya Kamati hiyo ya kukagua ufikishaji na upatikanaji wa huduma za mawasiliano
vijijini.
.....
Kamati ya Miundombinu
ya Bunge la Jamhuri ya Muungano Tanzania inaendelea na ziara ya kukagua ujenzi
wa minara ya simu, ufikishaji na upatikanaji wa huduma za mawasiliano vijijini
na kwenye maeneo yasiyo na mvuto wa kibiashara ili kuhakikisha kuwa wananchi
wanapata na kutumia huduma za mawasiliano kwenye maeneo mbali mbali nchini.
Kamti hiyo imeendelea na ziara yake kwenye mikoa ya Dodoma na Tabora ili kujiridhisha
na utendaji kazi wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) wa kufikisha
mawasiliano kwa wananchi.
Katika ziara hiyo, Mtendaji Mkuu wa UCSAF Eng.
Peter Ulanga amesema kuwa Mfuko umetoa ruzuku kwa Kampuni ya simu ya TIGO
kujenga mnara ili kufikisha huduma za mawasiliano kwa wananchi. Mfuko umetumia
zaidi ya dola za marekani elfu arobaini na moja na mia tano (41,500) ambapo ni
sawa na zaidi ya shilingi milioni 85 kuipatia kampuni ya TIGO kujenga mnara
ambao sasa unahudumia zaidi wa wakazi 4,000 wa kijiji cha Mayamaya na vijiji
vingine vya kata ya Zanka wilaya ya Bahi mkoani Dodoma ambapo walikuwa hawana
huduma za mawasiliano na sasa wananufaika na uwepo wa huu mnara na wanapata
huduma za mawasiliano. Mnara huu
ulikamilika mwezi Machi mwaka jana na kuanza kutoa huduma ya mawasiiano kwa
wananchi.
Naye mwakilishi wa
kampuni ya simu ya TIGO mkoa wa Dodoma mhandisi Hassan Said Gimbo wa kampuni hiyo
amewaeleza wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu waliofanya ziara ya
kukagua ujenzi wa minara, ufikishaji na upatikanaji wa huduma za mawasiliano
kuwa kampuni yao imekamilisha ujenzi wa mnara na sasa unatoa mawasiliano kwa
wananchi. Pia ameongeza kuwa kampuni ya TIGO inafuatilia mara kwa mara kwenye
eneo hilo na kuhakikisha kuwa mawasiliano yanapatikana. “Tunajitahidi kwa kiasi
kikubwa kukarabati na kuhakikisha kuwa pale mawasiliano yanapopotea au kuwa
hafifu tunafanya haraka kuyarudisha”, amesema mhandisi Gimbo.
Naye Mjumbe wa Kamati ya
Bunge ya Miundombinu akizungumza kwa niaba ya Kamati hiyo Mhe. Mussa Ntimizi
ameipongeza Serikali kwa kutoa ruzuku kwa kampuni za simu za mkononi kupitia UCSAF
ili kufikisha huduma za mawasiliano vijijini. Mhe. Ntimizi ameongeza kuwa kwa
sisi wawakilishi wa wananchi tunaotoka vijijini tunaelewa mahitaji na kiu ya
wananchi ya kupata mawasiliano kwenye makazi yao na umuhimu wa huduma nyingine
za mawasiliano. “Ukiangalia eneo kama hili halivutii kibiashara hivyo sio
rahisi kwa kampuni za simu kama hii ya TIGO kuja kuweka mnara wa simu hapa”
amesema Mhe. Ntimizi.
Tumepata taarifa kuwa
zaidi ya vijiji vitano vyenye wakazi zaidi ya watu 4,000 wanapata mawasiliano
kupitia mnara huu wa TIGO. “Kwa wananchi zaidi ya 4,000 kukosa mawasiliano sio
kitu kidogo na Mfuko huu unafanya kazi kubwa ya kufikisha mawasiliano vijijini
na Serikali inatumia gharama kubwa kujenga minara ya simu za mkononi na kutoa
huduma za mawasiliano vijjijini, hivyo wahakikishe kuwa huduma za mawasiliano
zinapatikana muda wote”, amesema Mhe. Ntimizi.
Pia, ametoa rai kwa
kampuni za simu nchini kuboresha na kukarabati miundombinu ya mawasiliano na
minara yao ili wananchi waendelee kupata mawasiliano muda wote kwa kuwa
serikali inatoa fedha nyingi kwa maana ya ruzuku na kuwapatia kampuni za simu
ili ziweze kufikisha huduma za mawasiliano kwa wanachi muda wote.
Amesema kuwa huduma
hizi zina gharama kubwa sana na wananchi hawajui gharama kubwa ambayo Serikali
imeingia kutengeneza mnara huu ambazo ni kodi zao na hawaoni thamani ya
Serikali kuwaletea huduma hii. Wananchi muendelee kulinda miundombinu ya
mawasiliano na kusiwepo na wizi wa mafuta ya dizeli, mitambo na vitu vingine kwa kuwa Serikali inatumia
gharama kubwa kufikisha huduma za mawasiliano vijijini ambapo ujenzi wa mnara
mmoja unagharimu zaidi ya shilingi milioni 200, hivyo kila mwananchi awe mlinzi
wa mwenzake ili kulinda miundombinu hii ya mawasiliano.
Tunaipongeza Serikali
kwa kujenga mnara kwenye kijiji chetu kwa kuwa tunapata mawasiliano na pale
yanapokuwa hayapatikani yanakatika wataalamu wa kampuni ya TIGO wanafika na
kurekebisha hali hii, “hakuna mawasiliano ya kampuni nyingine yoyote zaidi ya hii
ya TIGO kwenye eneo hili”, amesema mkazi wa kijiji cha Mayamaya, Bwana Emmanuel Konyanza kilichopo kata ya
Zanka wilaya ya Bahi mkoani Dodoma.
Katika ziara hiyo ya
Kamati kwenye kijiji cha Kizengi kata ya Kizengi iliyopo wilaya ya Uyui mkoani
Tabora, Meneja wa TTCL mkoa wa Tabora Bwana James Mlaguzi ameihaidi Kamati hiyo
kuwa wataongeza upana wa masafa ya TTCL ili yaweze kufika kwenye vijiji vya
mbali zaidi kwenye kata ya Kizengi ndani ya kipindi cha miezi miwili kuanzia
sasa. Naye Diwani wa Kata hiyo Bwana Magindika Lugaira Masaga akizungumza kwa
niaba ya wananchi mbele ya wajumbe wa Kamati hiyo amesema kuwa hapo mwanzo
wananchi walikuwa na shida kubwa ya mawasiliano.
Bwana Masaga anawashukuru wajumbe
wa Kamati hiyo kufanya ziara na wanategemea kuwa huduma za mawasiliano
zitaongezeka na kuwa bora zaidi kwa kuwa mawasiliano ya minara ya kampuni
nyingine sio mazuri sana bali wanategemea mnara wa Halotel pekee ambao una
masafa marefu na kufikia wananchi walio wengi zaidi.
hivyo mnara wa TTCL ukikamilika utasaidia
kuwafikia wananchi wengi zaidi wa kata hii yenye vijiji saba na wakazi 23,534.
Imetolewa na Kitengo
cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
0 Comments