Mkuu wa wilaya ya Mbulu Chelestino Mofuga akimkaribisha Naibu
Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Anastazia Wambura kuongea na wananchi waliokuwa katika tamasha la
utamaduni katika Kituo cha Pembe Nne za Utamaduni (4CCP) Haydom
mara baada ya kuwasili Wilayani humo kwa ziara ya kikazi ya siku mbili wilayani
humo.
Baadhi ya Washiriki wa tamasha la utamaduni katika Kituo cha Pembe
Nne za Utamaduni (4CCP) Haydom, wilaya ya Mbullu wakimsikiliza Naibu
Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Anastazia Wambura
(hayupo pichani) alipotembelea kituo hicho.
Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo Anastazia Wambura akitoka ndani kujionea moja ya nyumba za
asili ya Wabantu Wanyiramba na Wanyisanzu iliyopo Kituo cha Pembe Nne za
Utamaduni (4CCP) kilichopo Haydom.
Naibu
Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Anastazia Wambura akicheza
ngoma na washiriki wa tamasha la utamaduni alipotembelea Kituo cha Pembe Nne za
Utamaduni (4CCP) kilichopo Haydom.
Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa
na Michezo Anastazia Wambura (wa pili kulia) akipata maelezo ya utamaduni wa
kabila la Wadatoga katika Kituo cha Pembe Nne za Utamaduni (4CCP) kilichopo
Haydom.
Naibu Waziri wa
Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Anastazia Wambura (wa nne kulia)
akiwa katika picha ya pamoja na wasichana wa kabila la Datoga na kusisitiza
Watanzania kuenzi utamaduni wetu kwa kuurithisha kwa vijana wetu. Wa nne
kushoto ni Mbunge wa Mbulu Vijijini Flatei Massay.
Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa
na Michezo Anastazia Wambura (wa pili kushoto) akisalimiana na baadhi ya viongozi
wa Ulinzi na Usalama mara baada ya kuwasili Wilayani Mbulu kwa ziara ya kikazi ya
siku mbili wilayani humo.
(Picha na Eleuteri
Mangi, WHUSM, Mbulu)
...
Na Eleuteri Mangi, WHUSM, Mbulu
Watanzania wametakiwa kuenzi mila na desturi ambazo ni chanya wazitunze
na kuzitumia ili kujenga jamii yenye maadili mema nchini kwa manufaa ya kizazi
cha sasa na baadaye.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Wizara ya Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo Anastazia Wambura alipotembelea Kituo cha Pembe Nne za Utamaduni (4CCP) Haydom
wilaya Mbulu mkoani Manyara ambapo amejionea utajiri wa kiutamaduni wenye fursa za utalii wa kiutamaduni.
“Nimetembelea nyumba za asili zilizopo hapa katika kituo hiki
nimefurahishwa sana na utajiri wa kiutamaduni uliopo hapa, wazee walizingatia
maadili katika kuwalea watoto wao kulingana na mila na desturi zao, ni vema tuenzi
utamaduni wetu, huo ni msingi wa maadili mema ya jamii” alisema Naibu Waziri
Wambura
Akitolea mfano wa maadili mema yanayopaswa kurithishwa aliyojionea
katika kituo cha 4CCP na namna ambavyo watoto waliheshimu nyumba za wazazi wao,
Naibu Waziri Wambura amesema kuwa kwa mujibu wa mila na desturi za Kitanzani suala
la ulevi na utumiaji wa tumbaku kwa vijana ilikuwa ni mwiko hadi kijana afikie
umri wa utu uzima ambapo anaweza kuwa na maamuzi sahihi katika maisha yake yenye
kuwa na tija kwa familia.
“Kabla ya kuoa kijana alikuwa haruhusiwi kutumia tumbaku na kunywa
pombe, bali kijana akioa na kuwa na watoto wawili kwa mujibu wa mila za
makabila ya yaliyopo Mbulu aliruhusiwa kuingia katika kundi la watu wazima na
kuruhusiwa kutumia vitu mbalimbali ikiwemo tumbaku na kinywaji cha pombe. Hapa
kuna jambo la Watanzania kujifunza na kutunza ili kuondokana na mmomonyoko wa
maadili” alisema Naibu Waziri Wambura.
Mila za jamii zilizo njema zinapaswa kutunzwa na kuendelezwa ili
ziweze kusaidia vijana na jamii kwa ujumla kuweka mawazo yao katika shughuli za
maendeleo pamoja na kupatia familia zao mahitaji ya kila siku.
Naibu Waziri Wambura alisisitiza kuwa mila hizo hazitakiwi kuachwa
bali zainatakiwa kuenziwa, kutunzwa, kuendelezwa na kuhifadhiwa kwa manufaa ya
sasa ziweze kuchangia katika kukuza utalii wa kiutamaduni ambao ni moja ya
vyanzo vya mapato kwa wanajamii na taifa kwa ujumla.
Aidha, Naibu Waziri Wambura alisema kuwa wilaya ya Mbulu ni tajiri
katika masuala ya utamaduni na kuongeza kuwa wilaya hiyo ni mdau muhimu katika
sekta ya michezo na utamaduni ambazo zinapaswa kuendelezwa kwa manufaa ya
taifa.
Kwa upande wake Mbunge wa Mbulu Vijijini Flatei Massay amesema kuwa
wilaya hiyo imekuwa na utamaduni wa kufanya tamasha la utamaduni kila mwaka
ambapo mwaka huu lilifanyika tarehe 21 hadi 23 mwezi Septemba na inaedelea
kuimarisha umoja, mshikamano na ushirikiano miongoni mwa jamii katika masuala
mbalimbali ya maendeleo hatua inayopelekea makabila yote kuwa mstari wa mbele
katika kudumisha amani ya nchi.
Mbunge huyo aliyataja makabila yanayotokana na makundi makuu manne yanayopatikana
wilaya ya Mbulu kuwa ni pamoja na Wairaqw ambao ni jamii ya Wakushi, Wahadzabe
jamii ya Khoisan, Wanyiramba na Wanyisanzu jamii ya wabantu na Wadatooga jamii
ya Kiniloti.
Naye Mkuu wa wilaya ya Mbulu Chelestino Mofuga amemhakikishia Naibu Waziri
Wambura kuwa wilaya hiyo itaendelea kuenzi sekta ya utamaduni kwa kuwa na
tamasha la utamaduni linalokutanisha makabila yote wilyani humo wakati wa maadhimisho
ya Siku ya Uanuwai wa Utamaduni duniani ambayo hufanyika mwezi Mei tarehe 21 kila
mwaka.
Hatua hiyo inatokana na Tanzania kusaini mkataba wa azimio la Umoja wa
Mataifa (UN) kuenzi
utamaduni na kuheshimu tamaduni za watu wengine chini unaosimamiwa na
Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na
Utamaduni (UNESCO).
Mwaka 2002 Umoja wa Mataifa uliamua kuanzisha maadhimisho ya siku ya
Utamaduni Duniani kutokana na kuongezeka kwa migogoro, mapigano na kupotea kwa
maisha ya watu na mali zao iliyokuwa inatokea sehemu mbalimbali duniani
mwishoni mwa miaka ya 1990.








0 Comments