Mkuu wa Mkoa wa Dar
es Salaam Mheshimiwa Paul Makonda
ametembelea na kukagua daraja lililoharibika juzi Alhamisi kutokana na kunyesha
mvua kubwa katika eneo la Mbezi Kibanda
cha Mkaa jijini Dar es Salaam.
Ziara hiyo ameifanya
leo tarehe 28 Oktoba 2017 akiwa katika muendelezo wa ziara ya kutembelea maeneo
yaliyoathiriwa na mvua inayoendelea kunyesha
jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa
ziara hiyo Mh. Makonda aliwataka wakazi wa Dar es Salaam kutokubaki katika mazingira
hatarishi sambamba na kutokuchimba
mchanga, na kutokutupa taka kwenye mito.
"Nawaasa wananchi
wa jiji la Dar es Salaam kuchukua
tahadhari mapema kwani wataalamu wa hali ya hewa wanasema tarehe 1 November
2017 kuna mvua kubwa zaidi itakuja kuliko tuliyoiona kwa hiyo tuache
kuchimba mchanga kwenye mito, tuhame kwenye mabonde na tuache kuchafua mito
yetu kwani tusipofanya hivyo yatatokea madhara makubwa" alisema Makonda.
Pia Mh. Makonda
alisema kuna ujenzi wa barabara unakuja mpaka Chalinze na Tanroad washafanya
upembuzi yakinifu na wako mbioni kuanza ujenzi huo.
Mwisho Mh. Makonda
aliwasihi wananchi wachukue tahadhari
mapema ili kuepuka maafa yasiyo ya lazima yatakayosababishwa na mvua kubwa
inayotarajiwa kunyesha kuanzia tarehe moja ya mwezi ujao.
*IMETOLEWA NA*
*KITENGO CHA HABARI NA
UHUSIANO*
*HALMASHAURI YA
MANISPAA YA UBUNGO*










0 Comments