Asema asilimia 45 ya
wagonjwa wa Saratani nchini ni wanawake wanaougua
Saratani ya Matiti na
ya Mlango wa Kizazi.
Asilimia 80 ya
wagonjwa hawa hufika Hospitalini ugonjwa ukiwa hatua za mwisho.
Aweka lengo la
kuchunguza wanawake milioni 3 nchi nzima ifikapo Desemba 2018.
Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu ametumia mamlaka
aliyonayo kuagiza Vituo vya Afya (Health Centres) na Hospitali zote za Serikali
nchini kutenga Siku moja kila mwezi kwa ajili ya kuwapima wanawake
Saratani ya Matiti na ya Mlango wa
Kizazi ili kuwezesha ugunduzi wa mapema wa saratani na hivyo kuokoa maisha ya
wanawake hasa wa vijijini na wa kipato cha chini.
Mhe Ummy ametoa agizo
hilo leo katika Hospitali ya Ocean Road jijini Dar es salaam wakati wa
kukamilisha Matembezi ya kuhamasisha wanawake kupima Saratani ya Matiti. Octoba
kila mwaka, jumuiya ya kimataifa hutumia mwezi huu kuhamasisha upimaji wa
Saratani ya Matiti.
Mhe Ummy ameeleza kuwa
Saratani inazidi kutafuna maisha ya watanzania hasa wa kipato cha chini. Na
idadi ya wagonjwa na vifo itaongezeka mara mbili ifikapo mwaka 2020 endapo
Serikali, wadau na wananchi hawatachukua hatua zaidi za
kupambana na ugonjwa huu.
"Kinachoniumiza zaidi ni kuona kuwa asilimia 80
ya wagonjwa wote wanaofika Hospitalini
kupata huduma za matibabu ya Saratani
nchini wengi wakiwa ni wanawake wenzangu hufika ugonjwa ukiwa katika hatua za
mwisho za ugonjwa na hivyo kufanya matokeo
ya matibabu kutokuwa mazuri" alisema mhe Ummy.
Saratanizinazoongoza hapa
nchini ni; Saratani ya mlango wa kizazi (34%), Saratani ya Ngozi (kaporsis
Sarcoma)(13%), Saratani ya matiti (12%), Saratani ya mfumo wa njia ya chakula
(10%), Saratani ya Kichwa na shingo (7%), Saratani ya Matezi (6%), Saratani ya
Damu (4%), Saratani ya Kibofu cha mkojo (3%),Saratani ya ngozi (3%), Saratani
ya Macho (2%), na saratani ya tezi dume (2%).
Mhe Ummy ameeleza kuwa
Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais, Mhe Dr John Pombe Magufuli
imedhamiria kuhakikisha wananchi
wanapata huduma za uchunguzi na matibabu ya Saratani kwa urahisi, haraka na
bila malipo yoyote. *Hivyo, Serikali imeongeza Bajeti ya Dawa za Saratani
kutoka shs milioni 700 mwaka 2015 hadi kufikia shilingi bilioni 7 mwaka
2017.
Na kwa kuwa asilimia
kubwa ya wagonjwa wa Saratani ni wanawake, mhe Ummy ameeleza kuwa mwaka huu
2017, *Serikali kupitia Wizara ya Afya imeongeza Vituo vya Uchunguzi na
Matibabu ya Awali ya Saratani katika Vituo vinavyomilikiwa na Serikali kutoka
343 mwaka 2016 hadi 443 mwaka 2017.
Lengo la hatua hii ni kuhakikisha wanawake
wenye saratani wanagunduliwa mapema ili waweze kupata huduma za matibabu na
kupona kabisa. Mhe Ummy amesema amejiwekea lengo la kuhakikisha wanawake
milioni 3 nchini wanafikiwa na huduma za uchunguzi wa Saratani ya Matiti na ya
Mlango wa Kizazi ifikapo Desemba 2018.* Hivyo, amewataka wanawake kujitokeza
kupima.
Na kila Mkoa kujiwekea lengo la kupima angalau asilimia 20 ya wanawake
wa umri wa kuzaa (miaka 15 - 49) katika mikoa yao. Saratani Inatibika endapo
itagunduliwa mapema! Wakati ni Sasa! Tunao wajibu wa kuokoa maisha! Alisema mhe
Ummy.

0 Comments