Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) Bw. Hiiti Sillo
akizungumza na katika mafunzo ya ulinganifu ya viwango vya dawa kwa
wadhibiti wa viwango vya dawa Afrika Mashariki hivi karibuni.
(Picha na Maktaba)
....
(Picha na Maktaba)
....
Na:
Mwandishi Wetu, MAELEZO
Katika kipindi cha
miaka mitano iliyopita, kiwango cha ubora na usalama wa dawa nchini
kimeongezeka kwa zaidi ya asilimia 95.
Mkurugenzi Mkuu wa
Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) Bw. Hiiti Sillo, amemweleza mwandishi wetu
hivi karibuni kuwa kwa sasa usalama wa dawa nchini umeongezeka na kwamba
Taasisi yake imejizatiti kuongeza weledi wa udhibiti.
“Hivi sasa udhibiti ni
mkubwa hivyo dawa zetu ni salama kwa kiwango cha kati ya asilimia 92.5 hadi
asilimia 98” alisema Bw. Sillo.
Aliongeza kuwa hivi
sasa hali ya soko la dawa ni salama na taasisi yake inafuatilia kwa karibu ubora
na usalama wa dawa kwa kutumia mfumo maalum wa ukaguzi.
Bw. Sillo aliongeza
kuwa, mafanikio hayo yanatokana na kuimarika kwa uwezo wa taasisi yake pamoja
na ushirikiano mkubwa kati ya taasisi yake na wadau wakiwemo wananchi.
Mkurugenzi Mkuu huyo,
alibainisha kuwa taasisi yake imeongeza uwezo wake kwa kuajiri watumishi hadi
kufikia zaidi ya 300 kutoka watumishi 53 ilipoanzishwa. Aidha, mbali ya
kufungua ofisi za kanda saba (07), TFDA imeongeza uwezo wa maabara zake za
uchunguzi na zimepata ithibati za umahiri za kimataifa ikiwa ni pamoja na
kutambuliwa na Shirika la Afya la Dunia (WHO).
“Uwezo wetu umekuwa mkubwa
na tuko karibu na maeneo yote ya udhibiti. Hivi sasa mbali ya ofisi zetu za
kanda, lakini pia tuna wawakilishi katika kila Halmashauri nchini” Alisema.
Alifafanua kuwa Halmashauri
zote zina wataalamu ambao wanafanya kazi kwa niaba ya Mamlaka ambapo wanasimamia
na kudhibiti ubora na usalama wa dawa kwa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwa
maelekezo ya TFDA.
Hivi sasa TFDA ina
ofisi za kanda saba ambazo ni Kanda ya Ziwa, Kanda ya Kati, Kanda ya Kaskazini,
Kanda ya Magharibi, Kanda ya Mashariki, Kanda ya Kusini na ya Nyanda za Juu
Kusini.
Mkurugenzi Mkuu huyo
aliwapongeza wataalamu wa taasisi yake kwa kazi nzuri wanayoifanya na
kuwashukuru wadau mbali mbali kwa ushirikiano wao na hasa wananchi ambao
amesema wamekuwa mstari wa mbele kushirikiana na taasisi yake kutoa taarifa
zinazohusu uvunjifu wa sheria.
Kwa mujibu wa takwimu
zilizopo, katika kipindi cha mwaka 2003 hadi Juni, 2017, TFDA imesajili dawa 12,474.
Kwa upande wa dawa
zilizoingizwa na kugundulika kuwa hazina ubora, katika kipindi hicho, TFDA
iliteketeza dawa zenye jumla ya thamani Shilingi bilioni 11.591.

0 Comments