Afisa Elimu Sekondari Wilaya ya Bahi Bw. Patrick Gwivaha akizungumza na wajumbe kutoka Tume ya Utumishi wa Umma (hawapo pichani) walioongozwa na Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA wa Tume hiyo Bi Devotha Gabriel.
Mkuu wa kitengo cha TEHAMA kutoka Tume ya
Utumishi wa Walimu Bi Devotha Gabriel akikabidhi moja ya vitendea kazi wakati
wa ziara yakutembelea Ofisi za Tume hiyo Wilayani Bahi mapema leo.
Mkuu wa kitengo cha TEHAMA kutoka Tume ya
Utumishi wa Walimu Bi Devotha Gabriel akimuelekeza Katibu msaidizi wa Tume hiyo
Wilaya ya Bahi Mkoani Dodoma Bw. Antony
Damiano namna ya kutumia mfumo rasmi wa mawasiliano serikalini kwa njia
ya mtandao, mapema leo katika Ofisi za Tume hiyo Wilayani humo.
Katibu msaidizi wa Tume ya utumishi wa
Walimu Wilaya ya Bahi Mkoani Dodoma Bw.
Antony Damiano akionesha umahiri wake katika kutumia moja ya
mifumo ya TEHAMA itakayounganisha Ofisi za Tume hiyo Wilayani humo na Makao Makuu mapema leo, anayeshuhudia ni Mkuu wa kitengo
cha TEHAMA kutoka Tume ya Utumishi wa Walimu Bi Devotha Gabriel.
Afisa Elimu Sekondari Wilaya ya Bahi Bw. Patrick
Gwivaha akizungumza na wajumbe kutoka Tume ya Utumishi wa Umma (hawapo pichani)
walioongozwa na Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA wa Tume hiyo Bi Devotha Gabriel.
Frank Mvungi- Maelezo – Dodoma
Wadau wa maendeleo wametakiwa kujitokeza kuunga mkono Juhudi
za Serikali ya Awamu ya Tano katika kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya
elimu nchini ili kuongeza tija na kuchochea kasi ya maendeleo ya sekta hiyo na
Taifa kwa ujumla.
Akizungumza katika mahojiano maalum Wilayani Bahi Mkoani
Dodoma Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA kutoka Tume ya Utumishi wa Walimu Bi Devotha
Gabriel amesema kuwa Tume hiyo imejipanga kutatua changamoto zinazowakabili
walimu hapa nchini kwa kujenga mifumo rafiki ya TEHAMA ukiwemo ule utakoondoa
matumizi ya karatasi katika shughuli za kila siku za Tume hiyo (Paperless
system).
“Takribani asilimia sitini ya watumishi wa Serikali ni walimu
hivyo ni muhimu kwa wadau kujitokeza na kuunga mkono juhudi za Tume katika
kujenga mifumo hii ambayo itasaidia kwa
kiasi kikubwa kupunguza gharama za uendeshaji na kuboresha huduma katika ofisi
zetu hasa ngazi ya Wilaya.” Alisisitiza Devota.
Akifafanua Bibi Devota amesema kuwa Tume hiyo imejipanga
vyema kuhakikisha kuwa mifumo itakayojengwa inakuwa rafiki na inasaidia
kufikiwa kwa malengo ya kuanzishwa kwa Tume hiyo.
Kwa upande wake Katibu Msaidizi wa Tume hiyo Wilaya ya Bahi
Bw. Antony Damiano amesema kuwa kuwepo kwa Tume ni ukombozi mkubwa kwa walimu
hapa nchini kwani changamoto zilizokuwa zikiwakabili walimu kama vile kuchelewa
kupandishwa madaraja, kuthibitishwa kazini,Kustaafu na kupatiwa barua za ajira
sasa zimepatiwa ufumbuzi mara baada ya Tume hiyo kuanzishwa.
Kwa sasa huduma zimesogezwa karibu zaidi na walimu hali
inayochochea kuongezeka kwa kiwango cha uzingatiaji wa maadili, sheria na
Taratibu za kazi katika Wilaya ya Bahi.
“Tunapa fursa ya kusisitiza maadili kwa kuwa sasa
tunawatembelea walimu katika maeneo yao ya kazi na kusikiliza changamoto
zinazowakabili na kutafuta ufumbuzi” Alisisitiza Damiano
Pia Damiano alitoa wito kwa Walimu kuzingatia maadili na
kujitoa kikamilifu katika kutekeleza majukumu yao hali itakayosaidia kukuza
sekta ya elimu hapa nchini.
Tume ya utumishi wa Walimu imeanzishwa kwa sheria namba 25 ya
mwaka 2015 na imefanikiwa kuanza kutatua changamoto zinazowakabili walimu hapa
nchini kwanza kwa kuanzisha Ofisi kila Wilaya ili kusogeza huduma zake karibu
na Walimu.





0 Comments