Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa akijibu swali la papo kwa papo, leo bungeni mjini Dodoma, Novemba 9, 2017.
(Picha na Ofisi ya Waziri
Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimsikiliza Kiongozi
wa kambi ya upinzani Bungeni Freeman Mbowe, wakati akiuliza swali la papo kwa papo, bungeni
mjini Dodoma,
Novemba 9, 2017.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na
Kiongozi wa kambi ya upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, kabla ya kuanza kikao cha Bunge mjini Dodoma, Novemba 9, 2017.
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesisitiza kwamba
vyombo vya dola vya ndani ya nchi havijashindwa kuchunguza matukio ya kihalifu
yaliyotokea nchini, hivyo amewaomba wananchi waendelee kuwa na subira.
Amesema Serikali hairidhishwi na matukio
mbalimbali ya kihalifu yaliyofanywa na watu wasiolitakia mema Taifa, ambayo yaliyotokea
katika maeneo mbalimbali nchini na baadhi yake yamesababisha vifo na wengine
kujeruhiwa.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi,
Novemba 9, 2017) wakati akijibu swali la Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Bw.
Freeman Mbowe katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu,
Bungeni mjini Dodoma.
Bw. Mbowe alitaka apewe kauli ya Serikali juu
ya hatua zilizochukuliwa kuhusu tukio la kushambuliwa na mbunge wa Singida
Mashariki Bw. Tundu Lissu, ambapo alishauri uchunguzi huo ufanywe na vyombo vya
kimataifa, ambapo Waziri Mkuu amesema suala hilo linashughulikiwa na vyombo vya
ndani vya dola.
“Vyombo vya ndani vya dola vina uwezo mkubwa
wa kusimamia usalama wa nchi na vinaendelea na uchunguzi wa matukio hayo
yaliyofanywa na watu wasiolitakia mema Taifa letu. Nawaomba wananchi waendelee
kuwa na imani na vyombo vyetu vya dola na mara uchunguzi utakapokamilika
taarifa itatolewa.”
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwasihi
wananchi waendelee kushirikiana na Serikali kwa kutoa taarifa mbalimbali juu ya
vitendo vya kihalifu vinavyotokea kwenye maeneo yao kwa lengo la kudumisha
amani na utulivu nchini.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema ahadi ya Rais Dkt. John
Magufuli ya kuboresha maslahi ya watumishi wa umma imeanza kutekelezwa kwa kuwapandisha madaraja watumishi
wanaostahili sambamba na kulipa malimbikizo yao mbalimbali.
Waziri
Mkuu amesema baada ya kumaliza ulipaji wa malimbikizo ndipo Serikali itaendelea
na hatua ya uboreshaji wa mishahara kwa watumishi wote wa umma, hivyo amewaomba
waendelee kuwa na subira na imani na Serikali. Waziri Mkuu ameyasema hayo
alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kilindi, Bw. Omary Kigua aliyetaka kufahamu
ni lini Serikali itapandisha mishahara ya watumishi wa umma.
Pia
Waziri Mkuu amezungumzia changamoto ya masoko kwa mazao ya mbaazi na tumbaku
ambayo yanashughulikiwa na Serikali na tayari baadhi ya nchi zimeanza kuonyesha
nia ya kununua mazao hayo, hivyo amewaomba wananchi waendelee kuwa na uvumilivu.
Waziri
Mkuu ameyasema hayo alipokuwa akijibu swali la mbunge wa Viti Maalumu Bibi
Munde Tambwe aliyeiomba Serikali kumpatia ufafanuzi juu ya kukosekana kwa soko
la tumbaku ambayo imelundikana katika maghala na Bibi Pauline Gekul Mbunge wa
Babati aliyelalamikia kukosekana kwa soko la zao la mbaazi.
Akizungumzia kuhusu zao la tumbaku,
Waziri Mkuu amesema changamoto hiyo imetokana na wakulima wa zao hilo kuongeza
uzalishaji tofauti na makubaliano yaliyofikiwa awali na wanunuzi. “Nawaomba
wakulima waendelee kuwa wavumilivu Serikali inafanya mazungumzo na nchi za
lran, Korea Kusini, Misri na Indonesia ili waweze kununua tumbaku hiyo na
kuwaondolea usumbufu wakulima.”
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
DODOMA.
ALHAMISI, NOVEMBA 9, 2017.




0 Comments