Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania imedhamiria kuanzisha chombo cha kuendesha na kudhibiti
sekta ndogo ya usafiri majini, usalama wa meli na mazingira ya bahari ili kulinda
maslahi mapana ya taifa.
Hayo yameelezwa na
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa wakati akijibu
hoja ya Serikali kuhusu Muswada wa Sheria ya Wakala wa Meli wa Taifa mbele ya
wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kwenye kikao kilichofanyika
kwenye ukumbi wa Pius Msekwa, Bungeni mjini Dodoma.
Prof. Mbarawa amesema
kuwa Serikali ipo kwenye mchakato wa kupeleka Muswada Bungeni wa kutunga sheria
ambayo itaanzisha Shirika la Wakala wa
Meli wa Taifa (NASAC) ambao utasimamia
usalama wa meli na bahari zetu kwa lengo la kuboresha utendaji kazi wa bandari
zetu kama mnavyojua bandarini kumekuwa na changamoto nyingi. “Hivi karibuni
tumeshuhudia upotevu wa mali na vitu vingi pale bandarini kama vile madini na
vitu vingine vinaingia bila utaratibu,” amefafanua Prof. Mbarawa.
Ameongeza kuwa Serikali
imeona ibadilishe mtazamo uliokuwepo zamani kupitia SUMATRA ambayo inasimamia
masuala ya nchi kavu na majini, “Serikali imeona ianzishe chombo kingine ili kiweze
kujikita kusamimia masuala ya usafiri wa majini pekee na masuala nyeti hasa ya
uchumi wetu kama vile madini”.
Chombo kimoja cha kutoa huduma na kudhibiti sio
jambo geni. Hapa nchini tunayo taasisi ya Mamlaka ya Anga Tanzania (TCAA)
ambayo inatoa huduma ya anga na kudhibiti anga, hivyo Serikali inataka kufanya
hivyo pia kwenye sekta ya usafiri wa majini. Hili si jambo geni kwa kuwa
linafanyika kwenye nchi nyingine kama vile ya bandari ya Singapore na nchi
nyingine ya India.
Aidha, Prof. Mbarawa ametoa
wito kwa wadau kushirikiana na Serikali kuanzisha chombo hiki. Pia amefafanua
kuwa SUMATRA haitapokonywa majukumu yake bali nia ya Serikali ni kuitaka
SUMATRA isimamie sekta ya nchi kavu tu kwa maana ya barabara, reli, magari
ambayo ni sehemu kubwa na ina changamoto ambayo inahitajika kutatuliwa hivyo
ijikite huko na sekta hii ndogo ya usafiri wa majini iwe na chombo kingine
tofauti ili sheria iweze kutusaidia kukuza uchumi wa baharini na wa nchi kavu.
Ni imani ya Serikali
kuwa, kwa kuwa na chombo cha udhabiti cha sekta ya nchi kavu ambapo NASAC itaanzishwa
kwa ajili ya sekta ya usafiri wa majini, utaziwezesha sekta hizi za majini na
nchi kavu kukua vizuri hivyo kukuza uchumi wetu, watanzania watapata ajira na
kampuni nyingi za meli zitaingia nchini na kufanya kazi kwa kuwa mahali ambapo
hakuna udhibiti sekta haiwezi kukua, “angalieni sekta nyingine kama ya
mawasiliano ambako kuna udhibiti mzuri na sekta inakua vizuri” amesema Prof.
Mbarawa. Kwa mantiki hiyo, Serikali itawasilisha sheria ya SUMATRA Bungeni ili
kufanyiwa maboresho ili iweze kuchangia vizuri ukuaji wa sekta ya nchi kavu na
iende na wakati.
Katika hatua nyingine,
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Prof. Norman Sigalla
King amesema kuwa azma ya Serikali ni nzuri katika muendelezo wa kuhakikisha
kuwa taasisi zinazoanzishwa zina mgusa mlaji na kwa manufaa ya Serikali kwa
ujumla. Serikali imejibu hoja zote za wadau na Kamati yetu inaendelea kuchambua
hoja hizo ili kuhakikisha kuwa inasimamia
na kuishauri Serikali kwenye Muswada huu. Ni dhamira ya Kamati kuona kuwa biashara
bandarini inaendelea kuimarishwa na kudhibitiwa; na nchi yetu sio pekee yenye
bandari kwenye ukanda huu hivyo ni lengo la Kamati kuhakikisha kuwa Muswada huu
unaopendekezwa unaboreshwa ili kuhakikisha una akisi ushindani. Ameongeza kuwa Rais
wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameelekeza
udhibiti kwenye bandari yetu, hivyo huu ni mlolongo wa kusimamia na kudhibiti
shughuli za uendeshaji wa bandari.
Imetolewa
na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara
ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

0 Comments