TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema kuwa maandalizi ya vifaa kwa
ajili ya uchaguzi mdogo wa madiwani unaofanyika katika kata 43 yamekamilika na
awamu ya pili ya vifaa vitaanza kusafirishwa leo Ijumaa kwenda katika kata
husika.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC Kailima Ramadhani, alisema kwamba vifaa
vitakavyosafirishwa kuanzia kesho ni maalumu kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa
wasimamizi wa vituo, makarani waongozaji pamoja na mfano wa karatasi
za kupigia kura.
Alisema awamu ya kwanza ya kusafirisha vifaa ulifanywa na tume wakati wa
mafunzo ya wasimamizi wa uchaguzi ambayo yalifanyika mjini Dodoma ambavyo
vilitumika wakati wa uteuizi wa wagombea udiwani katika kata zote.
“Napenda kuwahakikishia umma kwamba tume imejipanga vizuri kwa ajili ya
uchaguzi huu na maandalizi ya kupeleka vifaa katika husika yako vizuri na awamu
ya pili ya upelekaji wa vifaa itapaelekwa kesho (leo),”alisema Ramadhani.
Alisema awamu ya tatu ya usafirishaji wa vifaa
itahusisha vifaa vichache ambavyo ni karatasi za kupigia kura pamoja
na fomu za kutangazia washindi ngazi ya kituo na ngazi ya kata.
Naye Mkurugenzi wa Manunuzi, Ugavi na Logistiki wa NEC Eliud Njaila, alisema
kwamba NEC imepeleka vifaa vya kutosha katika vituo vyote
893 vilivyoko katika kata 43 na hakutakuwa na upungufu wowote.
Alisema kwamba katika awamu ya pili ya upelekaji wa vifaa, wameweka na
mfano wa karatasi za kupigia kura ili wadau ambavyo ni vyama vya siasa
vijiridhishe kuhusu karatasi hivyo zitakavyokuwa pamoja na kufanya uhakiki wa
majina wa wagombea wao.
“Tunaamini kwamba vyama vya siasa vitahakiki majina ya wagombea wao kwa
kila kata ili kama kuna masahihisho wayalete mapema na NEC iweze kufanya
masahihisho haraka wakati wa kuchapa karatasi halisi za kupigia kura,” alisema
Njaila.
Njaila pia aliwataka wasimamizi wa uchaguzi wa wilaya kuwatumia maafisa
boharia katika kupokea na kutunza vifaa hivyo. Alisema wataalamu hao pia ndio
watumike pia kusafirisha vifaa hivyo kwa kuwa wao wana ujuzi wa namna ya
kutunza na kugawa vifaa.
Aliongeza kuwa iwapo wasimamizi wa uchaguzi watawatumia maafisa ugavi ni
wazi kuwa hakutakuwa na malalamiko ya kupungua kwa vifaa katika vituo vya
kupigia kura.
Naye Ofisa Uchaguzi wa NEC Sada Kangeta, alisema kuwa tayari
wameshafanya uhakiki wa vifaa vya uchaguzi na wamejiridhisha kuwa vifaa vyote
vipo kama inavyopaswa na kwamba hatua itakayofuata ni usafirishaji wa vifaa
hivyo katika maeneo husika.
Aidha aliwataka wapiga kura wote wa maeneo husika, wagombea wa vyama
vyote vya siasa na wadau wa siasa kutokuwa na hofu juu ya vifaa hivyo kwa madai
kuwa hakuna upungufu wowote utakaojitokeza.

0 Comments