Mratibu wa mashindano kutoka Spanest, Godwell Ole Meing’ataki akiwa
katika picha ya pamoja na baadhi ya wawakilishi wa timu zilizoingia
hatua ya robo fainali ya kombe la Spanest.
Mratibu wa mashindano kutoka Spanest, Godwell Ole Meing’ataki akikabidhi
moja ya seti ya jezi kwa nahodha wa timu ya soka ya kijiji cha Ilolo
Mpya, Esau Mwashambwa.
Mratibu wa mashindano kutoka Spanest, Godwell Ole Meing’ataki akionyesha
kombe ambalo linyakuliwa na bingwa wa mashindano ya kombe la kupiga
vita ujangili la Spanest ofisi kwake.
NA DENIS MLOWE, IRINGA
JUMLA ya timu 8 zimefuzu hatua ya robo fainali ya mashindano
ya kombe la kupiga vita ujangili ya Spanest Cup 2017 kutoka katika tarafa za
Idodi na Pawaga yanayoandaliwa na mradi wa kuboresha mtandao wa hifadhi zilizo
kusini mwa Tanzania (SPANEST) kwa kushirikiana na Hifadhi ya Taifa Ruaha.
Akizungumza wakati wa kutaja timu za vijiji zilizofanikiwa
kuingia hatua ya robo fainali na kuwazipatia vifaa vya michezo, Mratibu wa
mashindano hayo kutoka Spanest, Godwell Ole Meing’ataki alisema kuwa baada ya hatua za kwanza na pili
kumalizika kuna timu za vijiji ambazo zilileta rufaa katika kamati kulalamikia
mechi zaidi ya sita zilizovunjika.
Meing’ataki alisema kuwa mechi zilizovunjika zilitokana na
vurugu za mashabiki, usalama wa waamuzi hivyo kamati ilikaa na kuamua ni timu
gani ambazo zinastahili kuendelea na mashindano kwa kuzipatia pointi timu
ambazo zilistahili kutokana na timu husika kuwa chanzo cha vurugu.
Alisema kuwa kuvunjika kwa baadhi ya michezo hiyo ni
kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo mashabiki wa wa baadhi ya vijiji kuwa
chanzo cha vurugu kutokana na kutokuwa wavumilivu pindi maamuzi yanapokuwa
tofauti.
Aidha alisema kuwa chanzo kingine ni changamoto ya waamuzi
kuonyesha upendeleo kwa baadhi ya timu na kutoa maamuzi ambayo wakti mwingine
husababisha kuamsha hisia kali na kuleta vurugu na baadaye kuvunjika kwa mchezo
husika.
“Natoa wito kwa wachezaji na viongozi na mashabiki
wabadilikena kuzingatia kanuni kwani hatua tuliyofikia tutakuwa wakali zaidi
katika kusimamia kanuni na tunaahidi kuyafanyia kazi baadhi ya malalamiko
yaliyondani ya uwezo wetu yakiwemo ya waamuzi.” alisema
Meng’ataki alizitaja timu ambazo zimeingia katika robo
fainali ya mashindani hayo kutoka Tarafa ya Idodi kuwa ni timu za kijiji cha Mapogolo,
Malinzanga, Mahuninga, na Idodi waliongea kama washindi bora kwa walioshindwa (Best
Loser)
Alizitaja timu ambazo zimeingia robo fainali ya mashindano
hayo kutoka tarafa ya Pawaga kuwa ni Ilolo Mpya, Itunundu, Kinyika na Mboliboli
ambao wanapewa nafasi kubwa ya kuchukua ubingwa kutokana na kiwango chao
walichokionyesha tangu kuanza kwa mashindano hayo.
Aliongeza kuwa kamati imetoa vifaa vingine kwa timu
zilizofanikiwa kuingia hatua ya robo fainali ambayo itaanza rasmi siku ya
jumamosi kwa kupatiwa jezi seti moja kwa kila timu iliyoingia robo fainali.
Meing’ataki alisema kuwa Mashindano hayo ya mpira wa miguu
yameandaliwa kwa lengo la kuimarisha uhifadhi kwa wananchi kupitia mpira wa
miguu kutokana na mwitikio mkubwa hasa katika kutimiza lengo la kuwapatia elimu
ya ujangiri wananchi kuokoa tembo waliopo katika hifadhi za ruaha.
Katika mashindano hayo yanayotarajia kufika kilele chake
Novemba 19 mwaka huu mshindi wa kwanza anatarajia kuondoka na kitita cha
shilingi milioni 1, jezi seti moja,mipira miwili, cheti, medali za dhahabu na
safari ya kutembelea hifadhi ya taifa ya Ruaha.
Mshindi wa pili ataondoka na mpira mmoja, cheti, medali ya
shaba na fedha tasllimu shilingi laki 7 huku mshindi wa tatu akiondoka na mpira
mmoja, cheti, medali na fedha taslimu shilingi laki 5 na mshindi wa nne
ataondoka na mpira mmoja, cheti cha ushiriki na fedha taslimu shilingi laki 3.
Aidha kutakuwa na zawadi kwa ajili ya mfungaji bora atapata
mpira mmoja na fedha laki 1. Muamuzi bora atapata seti ya jezi ya uamuzi na
shilingi laki 1 na zawadi kwa ajili mchezaji bora laki 1.



0 Comments